Sunday, July 19, 2015

Mafanikio Yako Yamejificha Ndani ya Thamani

Mafanikio Yako Yamejificha Ndani ya Thamani

    • Kadiri utakavyozidi kutengeneza thamani nyingi kwaajiri ya watu wengine, ndivyo utakavyozidi kupata pesa nyingi.

    • Kwa mtu ambaye ni mjasiriamali mahili, kitu thamani ni bora kuliko pesa!
    Siku watu wengi wakigundua kuwa thamani ndiyo pesa yenyewe wataanza kuthamini sana “thamani” kuliko “pesa”; na ndipo kila mmoja atawekeza juhudi na maarifa katika kusaka thamani kwaajiri ya jamii, kuliko hivi sasa ambapo watu wengi wanakesha wakitafuta pesa. Iwapo, watu watajihusisha zaidi na kusaka thamani badala ya pesa, ni wazi kwamba dunia itajaa bidhaa na huduma bora zenye kukidhi mahitaji yote ya binadamu (maisha bora), na dunia itakuwa ni mahali pazuri pa kuishi. 

    Je uliwahi kujiuliza hiki kitu kinachoitwa thamani ni nini hasa? Au na wewe unaendelea kukutana nalo kwenye maandishi au mazungumzo basi! Maana ni kawaida kusikia watu wengi wakiongea juu ya suala zima la kuongeza thamani. Unapowauliza watu juu ya maana yake, jibu la haraka haraka unaambiwa kwa kingereza, yaani “Value” ukiuliza tena maana ya “value” anaambiwa ni “thamani” mwisho inakuwa kama ule mchezo wa kuku na yai ni kipi kilitangulia!.

    Mara nyingi, neno “thamani” linapewa tafsiri na maana ya juu juu, kiasi cha kuwafanya watu kushindwa kupata picha halisi juu ya umuhimu, ukubwa na upekee wa “thamani” katika maisha. Kutokana na tafsiri ya juu juu sana, thamani kama kitu halisi, imekuwa haithaminiwi kama ilivyo pesa.  Sababu mojawapo za kutothamini thamani ni kutokana na ukweli kwamba, thamani ni kitu ambacho hakionekani kwa macho na hakishikiki mkononi, hali ambayo huwafanya watu wengi kushindwa kutambua kuwa, pesa zote halali walizonazo zinatokana na thamani. Kwa maneno mengine “thamani ndiyo kila kitu” ambacho binadamu utumia kumaliza kero na changamoto mbalimbali za kimaisha”. 

    Thamani ni kile kiwango cha umuhimu uliomo ndani ya bidhaa au huduma. Pia thamani ni ubora ambao huifanya bidhaa/huduma fulani kupendeka au kuhitajika. Kwa maneno mengine, thamani ni ule uhitaji, umuhimu, faida, urahisi ambao mara nyingi huwekwa kwenye bidhaa au huduma fulani fulani. Thamani ndani ya bidhaa au huduma ndiyo hasa huwafanya watu kutoa pesa yao waliyoitolea jasho kwa hiari, kwa lengo la kujipatia thamani ili kukidhi mahitaji. Kwahiyo, thamani ni matokeo ya kile akipatacho mtu baada ya kuwa ametumia bidhaa au huduma yako.


    Kwa mtu ambaye ni mjasiriamali mahili, kitu thamani ni bora kuliko pesa, kwasababu kiasi cha pesa ambacho mtu ukipata, lazima kilinganishwe na thamani iliyoko ndani ya bidhaa au huduma. Watu wengi waliofanikiwa wanaangalia zaidi thamani ya vitu walivyotengeneza, tofauti na kwetu hapa ambapo wengi wanaangalia pesa tu!. Mwazoni kabla ya kutengeneza bidhaa, thamani yake inakuwa bado iko kichwani mwa mjasiriamali. Kinachotakiwa ni wewe kuitoa ndani yako na kuiweka katika hali ile ambayo unaweza kuwapa au kuwasaidia watu wengine ili watimize matakwa na haja zao. 

    Kadiri utakavyozidi kutengeneza thamani kubwa kwaajiri ya watu wengine, ndivyo utakavyozidi kupata pesa nyingi. Na ukiona unapata pesa kidogo usianze kutafuta mchawi, bali jiulize maswali ya kwamba wewe umetoa thamani ya kiwango gani kwa watu wengine? Kwahiyo, wewe jikite katika kutoa thamani ya kiwango kikubwa kwa watu wengine. Thamani unayotengeneza na kuwapa watu wengine inawasaidia kukidhi mahitaji yao mbalimbali. Kwa mjasiriamali yeyote, ni muhimu kutambua kuwa kila unapofirkiria kutengeneza thamani yoyote ile, hakikisha hisiwe ni kwaajiri yako peke yako, bali iwe ni kwaajiri ya watu wengine. Endapo utatengeneza thamani inayokulenga wewe peke yako, basi ujue kuwa, hakuna atakayekuletea pesa yake, kwasababu thamani uliyonayo haimfai chochote mtu mwingine. 

    Watu wengi wanaendelea kuishi maisha duni, kwasababu wanatumia muda wao mwingi kutengeneza thamani kwaajiri yao peke yao, na wala si kwa watu wengine. Kumbuka kuwa watu mpaka watume pesa kwako ni lazima kuwe na thamani fulani kwako. Ukweli ni kwamba, pesa aliyonayo mtu, mara nyingi ameitolea jasho kuipata, lakini mtu huyo yuko tayari kuiachia kwa hiari, iwapo kitu anachokitaka kutoka kwako kina thamani kubwa kuliko kiasi cha pesa unachomtaka atoe. Kwahiyo, tukitaka kutengeneza pesa kwa urahisi, ni lazima tujikite katika kutengeneza thamani kwa wengine. Na endapo utakuwa umechangia thamani yoyote kwa maisha ya watu wengine, na thamani hiyo ikawa na faida kubwa kwao, basi wewe tunastahili malipo. 

    Binadamu siku zote huwa anatafuta thamani kwaajiri ya kukidhi mahitaji yake ya kimaisha. Kwahiyo, kwa yeyote yule atakayeweza kutengeneza thamani, ni wazi kwamba kila mara pesa itakuwa inamfuata alipo. Watu mara zote wananunua thamani kupitia bidhaa au huduma mbalimbali. Wewe kama mjasiriamali, ni muhimu ukatambua kuwa, watu wanaponunua bidhaa, kinachonunuliwa siyo bidhaa kama bidhaa bali ni thamani yake. Thamani ya kitu, ndiyo huwasukuma watu wengine kutuma pesa zao kwako wewe uliye na thamani fulani. Wajasiriamali tunatakiwa kutambua kuanzia mwanzo wa utengenezaji bidhaa kuwa, thamani iliyoko ndani ya bidhaa ndiyo wateja wanatafuta. Kwa mfano; unapoona mteja amekuja kwenye salooni yako usifikiri amekuja kusuka, kuseti au kunyoa nywele bali anacholenga ni kupendeza na kupendeza ndiyo thamani halisi ya kusuka au kunyoa nywele. 

    Katika zama hizi tulizomo na huko mbele tuendako, maisha mazuri pamoja na ukuaji wa uchumi vitategemea sana uwezo na ujasiri wa watu katika kuhamisha thamani zote zilizoko ndani yao na kuziweka ndani ya bidhaa na huduma mbalimbali. Katika uwekaji wa thamani kwenye bidhaa, tulenge zaidi zile thamani ambazo zinatatua kero sugu kwenye jamii. Endapo thamani zilizotengenezwa zitatoa suluhisho la changamoto kwa watu waliowengi, moja kwa moja watu watakuwa tayari kutoa pesa yao kwa hiari kwenda kwa yule aliyetengeneza thamani.  Jambo la msingi hapa ni watu kuendelea kuelekeza nguvu na maarifa yao, katika kutengeneza na kuzalisha thamani nyingi kadiri inavyowezekana, kwani kwa kufanya hivyo, uchumi wa kaya na taifa kwa ujumla utakuwa sana na Tanzania itaendelea kuwa mahali pazuri pa kuishi.

    Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO

    2 comments:

    AKIM said...

    Hakika nimejifunza kitu kutoka hapa. Kuna maarifa mengi ambayo yamejificha AMA yapo, japo hatuyapati darasani.
    Asante Kwa shule hii isiyo na ada

    MUSHONGI said...

    Aksante Bw. Eliud.
    Endelea kujifunza zaidi kupitia makala nzuri, kwa kutembelea BLOG hii: http://maarifashop.blogspot.com