- Ukitumia macho ya ubongo unaona "Wallet" zetu hazijabeba pesa, bali vitu tofauti
- Ikiwa biashara yako wewe ni kufuga na kuuza kuku, “basi elfu kumi yako ni kuku”
Ilikuwa siku ya jumanne ya tarehe 30/06/2015, kwenye kipindi cha
tuongee asubuhi kinachorushwa na ITV kila siku mara baada ya kusoma magazeti
asubuhi. Zamu hii, alikuwa akihojiwa kiongozi mmoja wa dini, ambaye alikuwa
akijaribu kuelezea jinsi walivyojipanga katika kuandaa na kukamilisha siku ya
mkesha wa kuombea uchaguzi mkuu wa Tanzania mwaka huu, na akasisitiza kuwa
maombi yatafanyika mkesha wa 8/8/2015. Katika mazungumzo yake akagusia jambo
moja muhimu kuwa kwa sasa watu wengi wanatanguliza pesa mbele hata kabla ya
kufanya kazi na wengine wanadai walipwe pesa, ndipo wapige kura za ndiyo kwa
wagombea, hasa katika kipindi hiki tunapoelekea uchaguzi mkuu. Kiongozi huyu,
alitumia fursa hiyo kuwahasa watanzania kujiepusha na tabia ya kupenda
kutanguliza pesa mbele. Katika kuweka msisitizo wa kuonyesha ni kwa jinsi gani
pesa siyo kitu halisi; alirejea maandiko kutoka katika vitabu vitakatifu
yanayosema kuwa “Pesa ni Sanamu”. Kitendo
cha watu wengi kushindwa kutambua usanamu uliopo juu ya pesa, ndicho chanzo cha
kuwepo kwa changamoto nyingi zinazotukabili leo hii kama watu binafsi na taifa
kwa ujumla.
Dhana hii ya “pesa ni sanamu” ni muhimu tukaijua na kuielewa vizuri, ili hatimaye mimi na wewe tupate kujinusuru kwa
kutoka kwenye kundi kubwa la watu wanaotafuta pesa kama “sanamu”. Yawezekana
leo hii hatupati pesa ya kutosha na unaangaika sana, kwasababu fikra na
mitazamo yako ni ile ile ya kudhania kuwa pesa ni kitu halisi kumbe ni
“sanamu”. Tafsiri ya neno “pesa ni sanamu” inamaanisha kwamba, pesa siyo kitu
halisi bali ni mfano au kivuli cha bidhaa na huduma mbalimbali, ambazo
hazionekani kwa macho yetu ya kawaida. Kwa maana nyingine, pesa ni kitu ambacho
husimama badala ya bidhaa na huduma mbalimbali hasa wakati wa zoezi zima la
ubadilishanaji vitu kati ya muuzaji na mnunuzi.
Usanamu wa pesa unatokana na ukweli kwamba, pesa uliyonayo mfukoni
imetokana na wewe kuwapa watu wengine bidhaa au huduma ulizokuwa nazo; na wao
kwa hiari yao wakaamua kukupa vithibitisho ambavyo ni kama stakabadhi zinazothibitisha
uwepo wa makabidhiano ya bidhaa/huduma kati yako na watu wengine. Kwahiyo,
unapoangalia pesa uliyonayo mfukoni ujue una mfano tu wa vitu vilivyofanya pesa
kiasi fulani ije kwako. Kwenye wallet zetu hatuna pesa bali tuna vitu tofauti
tofauti. Mfano: utakuta mtu mwingine kwenye wallet yake ameweka huduma ya mapambo,
usafiri, ufundi, elimu, kuchangia mawazo kwenye vikao n.k. Wengine wallet zao
utakuta bidhaa kama vile chakula, nguo, dawa, jiko, taa, simu, mafuta n.k. Ukiamua
kutumia macho ya ubongo wako utakubaliana na mimi kuwa, pesa tulizonazo kwenye
wallet zetu hazifanani.
Wote tunaweza kuwa na noti ya shilingi elfu kumi za kitanzania, ambazo kwa
macho ya kawaida zinafanana, lakini kwa macho ya ubongo, wallet zetu hazijabeba
pesa bali zimebeba vitu tofauti mtofauti kabisa. Kwahiyo, ikiwa wewe biashara
yako ni kufuga na kuuza kuku basi elfu kumi yako ni kuku; kama wewe ni
mwandishi basi elfu kumi yako ni habari, gazeti au kitabu na ikiwa wewe ni mshereheshaji
basi elfu kumi yako ni ushereheshaji, ualimu, uchoraji n.k. Mifano hii michache
inatuonyesha kuwa, pesa zote tulizonazo hazifanani kabisa, isipokuwa bidhaa na
huduma tunazozalisha ndizo hubadilika na kuwa kitu kimoja ambacho ni sanamu
yaani “pesa” inayoonekana kwa macho yetu ya kawaida.
Kwa wale wote wanaoamini kuwa pesa siyo sanamu, maana yake ni kwamba
vitu vyote vinavyotengeneza pesa waliyonayo, hawawezi kuviona kwasababu macho
yao ya ubongo yamepofuka na hivyo wamebakia kutumia macho ya kawaida peke yake.
Ukiangalia pesa kwa macho ya kawaida (kwa mujibu wa kinachonekana), kiukweli
wewe utaishia tu kuona noti za elfu 10, 5, 2, 1 n.k. ikiwa kuona kwako
kutaishia hapo, basi na wewe ni mmojawapo wa watu hawaoni pesa bali wanaona “sanamu”. Mtu anayeona sanamu kila
wakati, hawezi kujua mahali kitu halisi kilipo na wala hatajua hiyo pesa
ilikotoka. Ndiyo maana inapotokea mtu akapata pesa na baadae kuishiwa, ni
vigumu kuzipata tena kwa haraka kwasababu, anakuwa tayari ameishasahau
zilikotoka. Na kwa yule anayetambua kuwa pesa aliyonayo kwenye wallet ilitokana
na mkusanyiko wa bidhaa na huduma mbalimbali; ni rahisi sana kwake yeye
kuzipata pesa kwa muda mfupi, kwasababu chanzo chake kinajulikana na kimekuwa
kikitunzwa na kuimarishwa mara kwa mara.
Kwenye jamii yetu kwasasa, bado watu wengi wanaishi kwenye ulimwengu wa
vitu vinavyoonekana kwa macho ya kawaida. Tunahitaji kujifunza kutumia macho
yetu ya ubongo katika kuona vitu vinavyoonekana
na visivyooekana na hapo ndipo tutaweza kuiona pesa halisi badala ya sanamu
tunayoiona sasa. Ni wakati muhafaka sasa kwa watu wote wanaotaka mafanikio
makubwa kugeukia kile kinachofanya pesa ije kwenye wallet zao; kwani hicho
ndicho kitu halisi. Ni muhimu, juhudi na maarifa yetu yote yakaelekezwa kwenye
kuzalisha thamani kupitia vitu na huduma mbalimbali ili kukidhi mahitaji ya
watu wengine na jamii kwa ujumla. Na tuyafanye yote haya, huku tukiamini
kufanikiwa na hakika tutafanikiwa.
Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO.
No comments:
Post a Comment