Saturday, August 29, 2015

Uhuru wa Kipato Unaletwa na Mchakato Siyo Shughuli



  •  Ukifanya kazi ki-shughuli ni sawa na mtu anaye sukuma mkokoteni kwa kulizunguka duara
  • Uhuru wa kipato (pesa) unawezekana tu kama utafanya kazi zako “Ki-mchakato

Watu wenye busara waliwahi kusema kuwa “maisha ni safari ndefu”, na kawaida ya safari ya maisha, ni pamoja na kukutana na vitu vingi njiani. Bila kuwa tumejipanga, vitu vingi tunavyokutana navyo safarini, vina uwezo mkubwa sana wa kutukwamisha na hatimaye kushindwa kufikia mwisho wa safari yetu.

Ili tuweze kumudu safari yetu maisha na hatimaye kufikia yale maisha ya ndoto zetu; kitu kimoja muhimu ni namna gani tunavyojipanga pamoja na mitazamo yetu juu ya kile tunachofanya kila siku.

Ukiangalia utaratibu mzima ambao watu wanautumia katika kufanya kazi zao, utaona makundi ya aina mbili. Aina ya kwanza ni kundi linalofanya kazi “ki-shughuli” na kundi la pili ni wale wanaofanya kazi “ki-mchakato. Kwa maana nyingine makundi haya mawili yanafanya kazi kwa kufuata mitazamo tofauti, ndiyo maana leo hii tuna watu wachache waliofanikiwa huku wengine wengi wakibakia pale pale miaka yote ya maisha yao.

Shughuli Hasa ni Kitu Gani? Shughuli ni kitendo kinachotakiwa kufanyika au kinachofanyika ili kukamilisha sehemu fulani ya kazi. Pia, shughuli inasimama kama kitu kimoja na ni cha kipekee, ikimalizika imemalizika, huna haja ya kuirudia. Ukiweza kufanya na kukamilisha shughuli moja peke yake haitoshelezi kutoa bidhaa husika. Lazima zifanyike shughuli zaidi ya moja ndipo bidhaa iliyokusudiwa iweze kupatikana.

Mfano: kama wewe shida yako ni kula chakula, lazima ujue kuwa, ili chakula chako kiwe tayari, lazima shughuli zaidi ya moja zifanyike, kutegemea mtu na mtu. Kuna mwingine ataanza kwa kununua mkaa, mwingine ataanza kwa kuwasha moto, na mwingine ataanza kwa kununua mchele n.k.; mpaka shughuli ya kupakua na hatimaye shughuli ya mwisho ya kula chakula.

Kwahiyo, endapo utakamilisha kufanya shughuli mojawapo na ukaishia hapo ni wazi kwamba hutaweza kula, kwasababu chakula kitakuwa hakijawa tayari. Kwa maana nyingine tunaweza kusema kwamba, hakuna bidhaa inayoweza kupatikana kwa kukamilisha shughuli moja peke yake, lazima shughuli zote muhimu zikamilike, ndipo matokeo au bidhaa tarajiwa ipatikane.

Kwa malengo ya kupata matokeo tarajiwa, inakubidi hujitahidi kukamilisha shughuli zako zilizopangwa, ili kupata matokeo tarajiwa. Endapo utaishia kukamilisha shughuli moja kati ya zote zinazotakiwa kufanyika, basi ujue kuwa hutaweza kupata au kuzalisha kitu chochote chenye thamani inayokusudiwa na wateja.

Mchakato Hasa ni Kitu Gani? Mchakato ni  mpangilio maalumu wa matukio au shughuli zaidi ya moja kwaajili ya kutoa/kuleta matokeo yanayokusudiwa. Ili mchakato uwepo, ni lazima shughuli husika ziwe na uhusiano wa karibu. Shughuli moja ikikamilika inakuwa ndio kianzio cha shughuli inayofuata na hatimaye kunakuwa na mwendelezo maalum hadi kufikia matokeo tarajiwa.

Kwahiyo, uzalishaji wa bidhaa yoyote unafuata utaratibu wa ki-mchakato. Ili uweze, kukamilisha kazi fulani au uweze kuzalisha bidhaa fulani, kunakuwapo na matukio au shughuli zaidi ya moja ambazo ziko kwenye aina fulani ya mnyororo. Na mnyororo huo ndio unakuwa na vipingiri pingiri ambavyo kila kipingiri, unaweza kusema ni shughuli au tukio moja. Kwa maana nyingine ni mchakato tu ndio una uwezo wa kukamilisha bidhaa.

Kazi ya kusaka mafanikio makubwa na hasa uhuru wa kipato (pesa) inawezekana tu kama utafanya au kuratibu kazi zako “Ki-mchakato  badala ya kuendelea na mfumo wa watu waliowengi, ambao utafuta eti! maisha bora “Ki-shughuli”. Na shughuli nyingi za utafutaji tunazofanya hazina uhusiano, mpangilio wala mwendelezo wenye tija.

Pia, shughuli hizi, hazina uratibu wowote wala uhusiano na ndoto zetu au malengo yetu ya muda mrefu. Matokeo yake tumejikuta tunapata matokeo hafifu, hali ambayo imeendelea kutukatisha tamaa na kudhania kuwa kupata uhuru wa kipato au pesa ni jambo ambalo haliwezekani na kama likiwezekana basi ni bahati.


Weka mpango wa kufikia malengo yako: Unapoanza safari yako ya kutafuta uhuru wa kipato (pesa) ni lazima ujipange, ikiwa ni pamoja na kufikiri kwa kina juu ya maisha yale unayotamani kuyaishi. Ukishajua ndoto yako ni ipi au mafanikio unayotarajia ni yapi, basi inakuwa rahisi kufahamu mchakato utakaopitia hadi kufikia kile unachotaka.

Ubainishaji wa mchakato kwaajili ya safari yako ya kwenda kwenye ndoto zako, unaambatana na zoezi la kuainisha shughuli zote muhimu zitakazotakiwa kufanyika hadi kufikia maisha ya ndoto yako. Pia, inakupa fursa ya kuweza kufahamu ni muda gani utautumia kufika hapo unapotaka kwenda.

Ukifanya kazi ki-mchakato ni rahisi sana kutathimini maendeleo ya kazi yako na unaweza kupima na kuona uko mbali au karibu kiasi gani na ndoto zako. Kwahiyo, inatosha kusema kwamba “mafanikio yoyote ni mchakato”. Na mchakato ndio unazaa mpango kazi, ambao ukifuatwa una uwezo wa kukutoa pale ulipo hadi pale unapotaka kwenda.

Ukifanya kazi ki-shughuli ni sawa na mtu anayesukuma mkokoteni kwa kulizunguka duara. Kwa mtu yeyote anayezunguka duara, siyo rahisi kufika anapotaka kwenda, kwani muda wote atakuwa anazunguka na kurudi aliko toka. Kwahiyo, maisha ya kufanya kazi ki-shughuli ni sawa na mtu anayezunguka mduara.  

Ndiyo maana unaweza ukakuta mtu kwa mfano anafanya biashara ya kununua na kuuza vitu na unakuta miaka nenda rudi yuko pale pale wakati kila siku anakwenda ananunua vitu na vinanunuliwa basi.

Sababu inayomfanya awe hivyo ni kwamba mtu huyo anafanya biashara yake kama shughuli na anajikuta kila mara anarudia shughuli ile ile miaka yote bila kupiga hatua yoyote. Yote haya yanatokea kwasababu “mtazamo wa biashara yako ni wa ki-shughuli badala ya mtazamo wa ki-mchakato”.

Unapoanza kufanya kazi au biashara yako kwa mtazamo wa ki-mchakato inakusaidia sana kupambana na changamoto. Lakini pia uvumilivu pale matatizo yanapojitokeza, ni rahisi kuvumilia kwakuwa unakuwa unafahamu ni wapi unaenda na utafanya kila liwezekanalo, ili kuweza kufikia malengo au ndoto zako. Ukiwa na mchakato wako ambao umeandikwa, unakusaidia kutokuangalia wengine wanachofanya badala yake, wewe unakomaa na jambo moja tu la kukamilisha mchakato wako.

Kufanya kazi Ki-mchakato kunahitaji umakini mkubwa sana, na umakini huu hauji hivi hivi, bali ni kwa kujenga tabia ya kujisomea vitabu na kujifunza kutokana na watu waliofanikiwa. 

Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO

KARIBU TWENDE KAZI PAMOJA

Friday, August 21, 2015

Sumu ya Umaskini ni Kufanya Kazi


Ni ukweli usiopingika kuwa umasikini ni kero kubwa hapa kwetu Tanzania na umekuwa kikwazo cha maendeleo ya watanzania kwa muda mrefu. Imefika mahali, watu wengine wamekata tamaa na wengine wanahisi kuwa labda Mungu ameamua wawe hivyo. Kosa kubwa lililofanyika na linaloendelea kufanyika ni tabia au utamaduni wa watu kuukubali umaskini na kuuona umaskini kama sehemu yao ya maisha.

Ndiyo maana hadi leo watu unawasikia wakisema na kujivunia wingi wao kama walalahoi au watu maskini. Kitendo cha kuukubali umaskni na kuufanya huwe kitu cha kawaida,  ndiyo sababu ya watu wengi kukosa ari, nguvu, ubunifu, shauku, juhudi na MAARIFA ya kufanya kazi ambazo matunda yake yatakuondolea umaskini. Kwahiyo, inatosha kusema kwamba, matunda ya kazi ndiyo yenye uwezo wa kipekee wa kumuondoa mtu yeyote kwenye mduara wa umaskini.

Lakini pamoja na hofu ya kushindwa kuondoa umaskini, dawa ni moja tu nayo ni kufanya KAZI. Ni vizuri kukumbuka kuwa tunaposema KAZI hatumaanishi ajira, bali tunamaanisha utumiaji wa akiri pamoja na nguvu ya mwili kwenye rasilimali kama ardhi, maliasili, ujuzi, pesa n.k.), ili kupata mali au bidhaa kwaajili ya watu wengine. Ukishapata bidhaa zenye manufaa (thamani) kwa watu wengine, basi mara moja watakuletea pesa kwa kubadilishana na bidhaa yako. Kadiri utakavyotengeneza bidhaa nyingi ndivyo utakavyopata pesa nyingi.

Wakati tunapofanya kazi, ni muhimu kufahamu kuwa, inahitajika kutumia nguvu zote mbili, yaani nguvu ya mwili na akiri (fikra). Mara nyingi, kwenye harakati za kupambana na umaskini, watu wengi tumeshindwa kupata mafanikio na sababu mojawapo imekuwa ni utumiaji wa nguvu ya mwili zaidi kuliko nguvu ya akiri (nguvu katika hali ya kufikiri na ubunifu).

Matumizi ya nguvu ya akiri katika KAZI yanahusisha zaidi kujitambua na kufahamu ni kitu gani unatakiwa kufanya na kwasababu gani, kutambua mahitaji ya watu wengine, kuongeza thamani na kufanya bidhaa kuwa bora zaidi, kuwa mbunifu kwa kila kazi unayofanya bila kujali ukubwa wake n.k.

Nguvu ya akiri na mwili ilibadilisha makapi ya ngano kuwa chakula cha mifugo: Miaka ya nyuma kidogo, kiwanda cha bia jijini Mwanza kilikuwa kikitupa makapi ya ngano kwenye madampo ya takataka, kutokana na ukweli kwamba hakuna aliyetambua na kuthamini hicho kilichokuwa kikitupwa. Watu wengi hawakuthamini makapi haya, kwasababu walikuwa hawajatumia nguvu ya akiri kuona makapi ya ngano kama kitu cha thamani.

Baada ya baadhi ya watu kutumia nguvu ya akiri, ndipo baadhi yao wakaanza kutengeneza chakula bora cha mifugo ambacho mahitaji yake kwa wafugaji ni makubwa sana. Leo hii tunashuhudia watu hawa wakitajirika baada ya kutumia nguvu ya akiri na mwili kugeuza makapi ya ngano (rasilimali) na kuwa chakula cha mifugo (mali) yenye thamani kubwa.

Mapanki ya samaki: Mwanzoni kabisa mapanki ya samaki, yalikuwa yanatupwa kwenye madampo ya takataka. Tofauti na makapi ya ngano, haya yalitoa harufu mbaya hasa pale yalipoanza kuoza na hali hii ilisababisha kero na uchafuzi wa mazingira hasa kwa wakazi waliokuwa wakiishi karibu na madampo hayo.

Lakini, watu walipoamua kuutmia nguvu yao ya akiri ndipo wakagundua kuwa kuna uwezekano wa kugeuza mapanki haya yakawa mboga (supu) au chakula kwa binadamu. Lakini zoezi la kubuni na kuongeza thamani halikuishia hapo, badala yake, watu walianza kutengeneza chakula cha mifugo hasa kuku.

Leo hii, watu walioajiriwa na kujiajiri kwenye bidhaa zitokanazo na mapanki ni wengi sana na wanapata kipato kwaajiri ya kuendesha familia zao. Kutokana na KAZI ya kuongeza thamani kwenye mapanki ya samaki, ni wazi kwamba wameweza kupunguza umaskini wao tofauti na huko nyuma walipokuwa hawajaanza kutumia nguvu yao ya mwili na akiri.

Kufanya kazi kunahitaji nidhamu ya hali ya juu. Mwanzoni mwa miaka ya sitini, Tanzania ilikuwa ina hali ya kiuchumi sawa na nchi nyingi za Asia; mfano: Singapore, Indonesia, Korea, China n.k. lakini cha ajabu ni kwamba leo hii nchi hizi ndizo zimekuwa wadau wetu wakubwa wa kutupatia misaada ya aina mbalimbali.

Tofauti ya maendeleo kati ya Tanzania na nchi hizi za Asia, ni nidhamu ya kufanya kazi. Wote tuliongozwa na siasa za ujamaa na umoja LAKINI sisi pamoja na kufanikiwa kuwa wamoja na wajamaa, tumekuwa na nidhamu ndogo ya KAZI, ambapo wengi wanategemea kupata huduma za bure kutoka serikalini bila wao kufanya kazi. Matokeo ya kutofanya kazi kwa bidii ni kwamba hapa Tanzania kila kukicha umaskini unaongezeka.

Wakulima wengi Tanzania wanakwenda shambani saa mbili asubuhi na kutoka kati ya saa tano hadi saa sita mchana. Kwa maana nyingine watu hawa kwa wastani wanafanya kazi masaa 3 hadi 4 kwa siku. Kuna wachache baadhi ya wakulima wanafanya kazi masaa 6 hadi 8 kwa siku. Hawa wanafanya kazi masaa matatu hadi manne zaidi ya wenzao. Wakulima wanaofanya kazi masaa mengi ni wazi kwamba wanapata mavuno mengi – na hapa wanaambiwa kuwa wametumia uchawi LAKINI kilicholeta tofauti ni yale masaa 3-4 waliyofanya kazi zaidi ya wenzao.

Kufanya kazi ni suala la mtu mmoja mmoja: Umaskini utaondoka kama kila mmoja atalichukulia suala la KAZI kuwa la binafsi badala ya kulichukulia kuwa ni la ujumla. Inatupasa kila mmoja, ajitathimni mwenyewe na ujiulize iwapo maisha anayoishi hivi sasa kama anayafurahia au la!.
Baada ya hapo kila mmoja kwa nafasi yake awekeza juhudi na MAARIFA kwenye kazi. Tukumbuke pia kuwa KAZI ni sheria ya Mungu na bila kufanya kazi hatuwezi tukaishi maisha mazuri.

Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO

KARIBU TWENDE KAZI PAMOJA

Wednesday, August 12, 2015

Bila Maboresho Imani Yako Inaweza Kukuangusha



  • Kila binadamu anapendelea kufanya kitu kadiri anavyotumwa na imani yake

  • Imani Mbaya = Matokeo Mabaya

Uzoefu katika maisha ya binadamu umeonyesha kuwa kile unachoamini zaidi ndicho ukuletea mafanikio uliyonayo. Siku za nyuma kidogo nilichukua likizo yangu ya mwaka, wakati nikiwa likizo nilibahatika kwenda Entebbe Uganda, nikiwa huko nilitembelea hoteli ya Imperial Botanical Beach, lengo langu lilikuwa ni kuamsha upya mwili na fikra zangu ndiyo maana niliweka jitihada za kuuzuria mafunzo ya jinsi ya kujenga na kutunza afya ya mwili. Hakika nilipata nilipata somo la thamani kubwa kwa maisha yangu yote.

Kila binadamu anapendelea kufanya kitu kadiri anavyotumwa na imani yake: Siku ya kwanza nilipokutana na mtaalamu wa mazoezi ya viungo na afya, aliniuliza kuhusu tabia na utaratibu wangu kwa ujumla juu ya ulaji wangu wa chakula kwa siku. Nilimwambia kuwa, mara nyingi huwa ninakula milo miwili kwa siku; yaani kifungua kinywa na au chakula cha mchana na usiku. Wakati nikimueleza hayo nilifanya hivyo huku nikiangalia saa yangu ya mkononi, ndipo nikashitukia ni saa kumi na mbili jioni na baadae kugundua kuwa sijala chochote kwa siku nzima. LAKINI bado nilijisemea kimoyomoyo “Kwangu mimi kula siyo kipaumbele ”.

Baada ya mtaalamu kusikia kuwa huwa na kula mara mbili kwa siku aliniangalia na kuonyesha kusikitika kidogo, lakini aliendelea kusema, “Unatakiwa kula milo mitatu kwa siku.”
Kusikia hivyo nilimjibu kwamba, habari hiyo ya milo mitatu kwa siku nilikwishaiskia kabla. Lakini pamoja na kusikia habali hiyo, mimi imani yangu ni kwamba, iwapo nitakula milo mitatu kila siku, unene wangu utaongezeka sana. 

Mtaalamu wangu alicheka, na akazidi kusisitiza kuwa ninatakiwa kula zaidi wakati wa mchana kwasababu mwili unakuwa unafanya kazi sana. Kwahiyo, miili yetu uhitaji chakula cha kutosha nyakati za asubuhi, na mapema kabla ya saa za mchana (adhuhuri), na pia tunahitaji chakula kidogo nyakati za usiku, kwani muda wa usiku mwili unakuwa na kazi kidogo sana kwa maana nyingine unakuwa umepumzika.
Niliambiwa kwamba kwa mtu ambaye bado yuko vizuri kiafya, asipokula chakula cha kutosha ni kwamba badala ya mwili kuunguza mafuta, mwili utaunguza misuli na ikitokea hali hii basi ujue hutakaa huwe na kiwango cha uimara wa mwili unaoutaka.

Mimi nilikuwa ninaendelea kupigana na imani yangu iliyozidikuniambia kuwa, milo mitatu kwa siku itaongeza kilo moja ya uzito. Lakini kwakuwa nilienda kwa mtaalamu kwaajiri ya afya yangu, nilijifikiria na kuamua kufuata ushauri niliopewa na mtaalamu.
Wasikilize wataalamu: Kwa muda wa siku sita, nilianza kufanyia kazi imani mpya na kuanzia siku ya kwanza nikaanza kupata milo mitatu kwa siku. Niliamua kufuata masharti kama nilivyoelekezwa na mtaalamu kwa kuanza kula milo mitatu kwa siku. Kitu kimoja kilichojitokeza ni kwamba nguvu ya mwili iliimarika zaidi. Kuanzia nyakati za asubuhi, nilijisikia mwenye nguvu ya kutosha siku nzima. Niliendelea na mpango huu mpaka mwisho wa siku ya sita, siyo tu kwamba sikuongezeka uzito, bali badala yake nilipugua kilo kadhaa.
Kitendo cha kuamua kuachana na imani yangu juu ya idadi ya milo kwa siku, na kuamua kumsikiliza mtaalamu, kilinisaidia sana kufikia malengo yangu ambayo nisingeyatimiza hata siku moja kama ningeendelea kufanya yale niliyoamini miaka yote.

Imani mbaya = matokeo mabaya: Hoja muhimu juu ya stori hii ni kwamba, nilikuwa na imani potofu ambayo ilijengeka siku nyingi na imani hii kimsingi ilinizuia kusonga mbele na hatimaye kushindwa kutimiza malengo yangu ya kiafya. Pamoja na kwamba nimesikia tangu nikiwa mdogo, kwamba mtu mzima anatakiwa kupata milo mitatu kwa siku, sikuwahi kuamini kama faida zitokanazo na kula milo mitatu kwa siku zilikuwa za kweli. Nilikuwa na taarifa, lakini, faida hizi sikuzipata mpaka pale nilipoamua kufunguka na kuamua kujaribu yale niliyoelekezwa na mtaalamu —ndipo nilipopata uzoefu na elimu ya kweli juu ya kile kilichoonekana kufanya vizuri kwangu.

Kwa vyovyote vile, ukweli huu ni rahisi na unaweza kutumika kwenye hali yoyote katika maisha. Sasa swali kwako, “ni imani zipi zinazokurudisha nyuma kiasi cha kushindwa kufikia mafanikio ya kipesa au ndoto zako? Na utafanya nini kuondoa imani hizo?


Iwapo utapenda kujifunza jinsi ya kutambua na kuondokana na imani ambazo siku zote zimekurudisha nyuma pale ulipojaribu kutafuta uhuru wa kipato na mafanikio kimaisha, bonyeza KUJIUNGA NA PROGRAMU kisha weka barua pepe yako, kushiriki mafunzo juu ya mafanikio ya kifedha. 

Mafunzo haya yatatolewa bure kupitia barua pepe utakayosajiri KUJIUNGA NA PROGRAMU

Mafunzo yataanza tarehe 15/Septemba/2015 hadi 30/Septemba/2015.  Kwa kujiunga na mafunzo haya utapata thamani kubwa sana, ikiwa ni pamoja na kubadili mitazamo hasi uliyonayo juu ya kupata pesa. Pia utapata kujua mbinu na njia za uhakika utakazozitumia kufikia maisha ya ndoto yako kwa uhakika na kwa muda mfupi zaidi. Kama unafikiri program yetu haikufai huko sahihi; LAKINI bado ninakushauri ujitahidi kutafuta mtu, ambaye atakufundisha na kukupa mwongozo wa jinsi ya kufikia uhuru wa kipato.

Kwa maelezo zaidi juu ya prograu hii ya mafunzo whatsApp: +255 788 855 409 au E-mail: mchumieconomist2009@gmail.com.


KARIBU TWENDE KAZI PAMOJA