Ni ukweli usiopingika kuwa umasikini ni kero kubwa
hapa kwetu Tanzania na umekuwa kikwazo cha maendeleo ya watanzania kwa muda
mrefu. Imefika mahali, watu wengine wamekata tamaa na wengine wanahisi kuwa
labda Mungu ameamua wawe hivyo. Kosa kubwa lililofanyika na linaloendelea
kufanyika ni tabia au utamaduni wa watu kuukubali umaskini na kuuona umaskini
kama sehemu yao ya maisha.
Ndiyo maana hadi leo watu unawasikia wakisema na
kujivunia wingi wao kama walalahoi au watu maskini. Kitendo cha kuukubali
umaskni na kuufanya huwe kitu cha kawaida,
ndiyo sababu ya watu wengi kukosa ari, nguvu, ubunifu, shauku, juhudi na
MAARIFA ya kufanya kazi ambazo
matunda yake yatakuondolea umaskini. Kwahiyo, inatosha kusema kwamba, matunda
ya kazi ndiyo yenye uwezo wa kipekee wa kumuondoa mtu yeyote kwenye mduara wa
umaskini.
Lakini pamoja na hofu ya kushindwa kuondoa umaskini,
dawa ni moja tu nayo ni kufanya KAZI.
Ni vizuri kukumbuka kuwa tunaposema KAZI
hatumaanishi ajira, bali tunamaanisha utumiaji wa akiri pamoja na nguvu ya mwili
kwenye rasilimali kama ardhi, maliasili, ujuzi, pesa n.k.), ili kupata mali au
bidhaa kwaajili ya watu wengine. Ukishapata bidhaa zenye manufaa (thamani) kwa
watu wengine, basi mara moja watakuletea pesa kwa kubadilishana na bidhaa yako.
Kadiri utakavyotengeneza bidhaa nyingi ndivyo utakavyopata pesa nyingi.
Wakati tunapofanya kazi, ni muhimu kufahamu kuwa,
inahitajika kutumia nguvu zote mbili, yaani nguvu ya mwili na akiri (fikra).
Mara nyingi, kwenye harakati za kupambana na umaskini, watu wengi tumeshindwa
kupata mafanikio na sababu mojawapo imekuwa ni utumiaji wa nguvu ya mwili zaidi
kuliko nguvu ya akiri (nguvu katika hali ya kufikiri na ubunifu).
Matumizi ya nguvu ya akiri katika KAZI yanahusisha zaidi kujitambua
na kufahamu ni kitu gani unatakiwa kufanya na kwasababu gani, kutambua mahitaji
ya watu wengine, kuongeza thamani na kufanya bidhaa kuwa bora zaidi, kuwa
mbunifu kwa kila kazi unayofanya bila kujali ukubwa wake n.k.
Nguvu
ya akiri na mwili ilibadilisha makapi ya ngano kuwa chakula cha mifugo:
Miaka ya nyuma kidogo, kiwanda cha bia jijini Mwanza kilikuwa kikitupa makapi ya
ngano kwenye madampo ya takataka, kutokana na ukweli kwamba hakuna aliyetambua
na kuthamini hicho kilichokuwa kikitupwa. Watu wengi hawakuthamini makapi haya,
kwasababu walikuwa hawajatumia nguvu ya akiri kuona makapi ya ngano kama kitu
cha thamani.
Baada ya baadhi ya watu kutumia nguvu ya akiri, ndipo
baadhi yao wakaanza kutengeneza chakula bora cha mifugo ambacho mahitaji yake
kwa wafugaji ni makubwa sana. Leo hii tunashuhudia watu hawa wakitajirika baada
ya kutumia nguvu ya akiri na mwili kugeuza makapi ya ngano (rasilimali) na kuwa
chakula cha mifugo (mali) yenye thamani kubwa.
Mapanki
ya samaki: Mwanzoni kabisa mapanki ya samaki, yalikuwa
yanatupwa kwenye madampo ya takataka. Tofauti na makapi ya ngano, haya yalitoa
harufu mbaya hasa pale yalipoanza kuoza na hali hii ilisababisha kero na
uchafuzi wa mazingira hasa kwa wakazi waliokuwa wakiishi karibu na madampo
hayo.
Lakini, watu walipoamua kuutmia nguvu yao ya akiri
ndipo wakagundua kuwa kuna uwezekano wa kugeuza mapanki haya yakawa mboga
(supu) au chakula kwa binadamu. Lakini zoezi la kubuni na kuongeza thamani
halikuishia hapo, badala yake, watu walianza kutengeneza chakula cha mifugo
hasa kuku.
Leo hii, watu walioajiriwa na kujiajiri kwenye bidhaa
zitokanazo na mapanki ni wengi sana na wanapata kipato kwaajiri ya kuendesha
familia zao. Kutokana na KAZI ya
kuongeza thamani kwenye mapanki ya samaki, ni wazi kwamba wameweza kupunguza
umaskini wao tofauti na huko nyuma walipokuwa hawajaanza kutumia nguvu yao ya
mwili na akiri.
Kufanya kazi kunahitaji nidhamu ya hali ya juu.
Mwanzoni mwa miaka ya sitini, Tanzania ilikuwa ina hali ya kiuchumi sawa na
nchi nyingi za Asia; mfano: Singapore, Indonesia, Korea, China n.k. lakini cha
ajabu ni kwamba leo hii nchi hizi ndizo zimekuwa wadau wetu wakubwa wa
kutupatia misaada ya aina mbalimbali.
Tofauti ya maendeleo kati ya Tanzania na nchi hizi
za Asia, ni nidhamu ya kufanya kazi. Wote tuliongozwa na siasa za ujamaa na
umoja LAKINI sisi pamoja na kufanikiwa kuwa wamoja na wajamaa, tumekuwa na nidhamu
ndogo ya KAZI, ambapo wengi
wanategemea kupata huduma za bure kutoka serikalini bila wao kufanya kazi.
Matokeo ya kutofanya kazi kwa bidii ni kwamba hapa Tanzania kila kukicha
umaskini unaongezeka.
Wakulima wengi Tanzania wanakwenda shambani saa
mbili asubuhi na kutoka kati ya saa tano hadi saa sita mchana. Kwa maana
nyingine watu hawa kwa wastani wanafanya kazi masaa 3 hadi 4 kwa siku. Kuna
wachache baadhi ya wakulima wanafanya kazi masaa 6 hadi 8 kwa siku. Hawa
wanafanya kazi masaa matatu hadi manne zaidi ya wenzao. Wakulima wanaofanya
kazi masaa mengi ni wazi kwamba wanapata mavuno mengi – na hapa wanaambiwa kuwa
wametumia uchawi LAKINI kilicholeta tofauti ni yale masaa 3-4 waliyofanya kazi
zaidi ya wenzao.
Kufanya
kazi ni suala la mtu mmoja mmoja: Umaskini utaondoka
kama kila mmoja atalichukulia suala la KAZI kuwa la binafsi badala ya kulichukulia
kuwa ni la ujumla. Inatupasa kila mmoja, ajitathimni mwenyewe na ujiulize iwapo
maisha anayoishi hivi sasa kama anayafurahia au la!.
Baada ya hapo kila mmoja kwa nafasi yake awekeza
juhudi na MAARIFA kwenye kazi. Tukumbuke
pia kuwa KAZI ni sheria ya Mungu
na bila kufanya kazi hatuwezi tukaishi maisha mazuri.
Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO.
KARIBU TWENDE KAZI PAMOJA
No comments:
Post a Comment