- Ukifanya kazi ki-shughuli ni sawa na mtu anaye sukuma mkokoteni kwa kulizunguka duara
- Uhuru wa kipato (pesa) unawezekana tu kama utafanya kazi zako “Ki-mchakato”
Watu wenye busara
waliwahi kusema kuwa “maisha ni safari ndefu”, na kawaida ya safari ya maisha,
ni pamoja na kukutana na vitu vingi njiani. Bila kuwa tumejipanga, vitu vingi
tunavyokutana navyo safarini, vina uwezo mkubwa sana wa kutukwamisha na
hatimaye kushindwa kufikia mwisho wa safari yetu.
Ili tuweze kumudu safari
yetu maisha na hatimaye kufikia yale maisha ya ndoto zetu; kitu kimoja muhimu ni
namna gani tunavyojipanga pamoja na mitazamo yetu juu ya kile tunachofanya kila
siku.
Ukiangalia
utaratibu mzima ambao watu wanautumia katika kufanya kazi zao, utaona makundi
ya aina mbili. Aina ya kwanza ni kundi linalofanya kazi “ki-shughuli” na
kundi la pili ni wale wanaofanya kazi “ki-mchakato”. Kwa maana
nyingine makundi haya mawili yanafanya kazi kwa kufuata mitazamo tofauti, ndiyo
maana leo hii tuna watu wachache waliofanikiwa huku wengine wengi wakibakia
pale pale miaka yote ya maisha yao.
Shughuli Hasa ni Kitu Gani? Shughuli ni kitendo kinachotakiwa
kufanyika au kinachofanyika ili kukamilisha sehemu fulani ya kazi. Pia,
shughuli inasimama kama kitu kimoja na ni cha kipekee, ikimalizika imemalizika,
huna haja ya kuirudia. Ukiweza kufanya na kukamilisha shughuli moja peke yake haitoshelezi
kutoa bidhaa husika. Lazima zifanyike shughuli zaidi ya moja ndipo bidhaa
iliyokusudiwa iweze kupatikana.
Mfano: kama wewe shida yako ni kula chakula, lazima ujue kuwa, ili chakula chako
kiwe tayari, lazima shughuli zaidi ya moja zifanyike, kutegemea mtu na mtu. Kuna
mwingine ataanza kwa kununua mkaa, mwingine ataanza kwa kuwasha moto, na
mwingine ataanza kwa kununua mchele n.k.; mpaka shughuli ya kupakua na hatimaye
shughuli ya mwisho ya kula chakula.
Kwahiyo, endapo
utakamilisha kufanya shughuli mojawapo na ukaishia hapo ni wazi kwamba hutaweza
kula, kwasababu chakula kitakuwa hakijawa tayari. Kwa maana nyingine tunaweza
kusema kwamba, hakuna bidhaa inayoweza kupatikana kwa kukamilisha shughuli moja
peke yake, lazima shughuli zote muhimu zikamilike, ndipo matokeo au bidhaa
tarajiwa ipatikane.
Kwa malengo ya
kupata matokeo tarajiwa, inakubidi hujitahidi kukamilisha shughuli zako
zilizopangwa, ili kupata matokeo tarajiwa. Endapo utaishia kukamilisha shughuli
moja kati ya zote zinazotakiwa kufanyika, basi ujue kuwa hutaweza kupata au
kuzalisha kitu chochote chenye thamani inayokusudiwa na wateja.
Mchakato Hasa ni Kitu Gani? Mchakato ni mpangilio maalumu wa matukio au shughuli zaidi
ya moja kwaajili ya kutoa/kuleta matokeo yanayokusudiwa. Ili mchakato uwepo, ni
lazima shughuli husika ziwe na uhusiano wa karibu. Shughuli moja ikikamilika
inakuwa ndio kianzio cha shughuli inayofuata na hatimaye kunakuwa na mwendelezo
maalum hadi kufikia matokeo tarajiwa.
Kwahiyo, uzalishaji
wa bidhaa yoyote unafuata utaratibu wa ki-mchakato. Ili uweze, kukamilisha kazi
fulani au uweze kuzalisha bidhaa fulani, kunakuwapo na matukio au shughuli
zaidi ya moja ambazo ziko kwenye aina fulani ya mnyororo. Na mnyororo huo ndio
unakuwa na vipingiri pingiri ambavyo kila kipingiri, unaweza kusema ni shughuli
au tukio moja. Kwa maana nyingine ni mchakato tu ndio una uwezo wa kukamilisha
bidhaa.
Kazi ya kusaka
mafanikio makubwa na hasa uhuru wa kipato (pesa) inawezekana tu kama utafanya
au kuratibu kazi zako “Ki-mchakato” badala ya kuendelea na mfumo wa watu
waliowengi, ambao utafuta eti! maisha bora “Ki-shughuli”.
Na shughuli nyingi za utafutaji tunazofanya hazina uhusiano, mpangilio wala mwendelezo
wenye tija.
Pia, shughuli
hizi, hazina uratibu wowote wala uhusiano na ndoto zetu au malengo yetu ya muda
mrefu. Matokeo yake tumejikuta tunapata matokeo hafifu, hali ambayo imeendelea
kutukatisha tamaa na kudhania kuwa kupata uhuru wa kipato au pesa ni jambo
ambalo haliwezekani na kama likiwezekana basi ni bahati.
Weka mpango wa kufikia malengo yako: Unapoanza safari yako ya kutafuta uhuru wa
kipato (pesa) ni lazima ujipange, ikiwa ni pamoja na kufikiri kwa kina juu ya
maisha yale unayotamani kuyaishi. Ukishajua ndoto yako ni ipi au mafanikio unayotarajia
ni yapi, basi inakuwa rahisi kufahamu mchakato utakaopitia hadi kufikia kile
unachotaka.
Ubainishaji wa
mchakato kwaajili ya safari yako ya kwenda kwenye ndoto zako, unaambatana na
zoezi la kuainisha shughuli zote muhimu zitakazotakiwa kufanyika hadi kufikia
maisha ya ndoto yako. Pia, inakupa fursa ya kuweza kufahamu ni muda gani
utautumia kufika hapo unapotaka kwenda.
Ukifanya kazi
ki-mchakato ni rahisi sana kutathimini maendeleo ya kazi yako na unaweza kupima
na kuona uko mbali au karibu kiasi gani na ndoto zako. Kwahiyo, inatosha kusema
kwamba “mafanikio yoyote ni mchakato”.
Na mchakato ndio unazaa mpango kazi, ambao ukifuatwa una uwezo wa kukutoa pale
ulipo hadi pale unapotaka kwenda.
Ukifanya kazi
ki-shughuli ni sawa na mtu anayesukuma mkokoteni kwa kulizunguka duara. Kwa mtu
yeyote anayezunguka duara, siyo rahisi kufika anapotaka kwenda, kwani muda wote
atakuwa anazunguka na kurudi aliko toka. Kwahiyo, maisha ya kufanya kazi
ki-shughuli ni sawa na mtu anayezunguka mduara.
Ndiyo maana unaweza
ukakuta mtu kwa mfano anafanya biashara ya kununua na kuuza vitu na unakuta
miaka nenda rudi yuko pale pale wakati kila siku anakwenda ananunua vitu na
vinanunuliwa basi.
Sababu inayomfanya
awe hivyo ni kwamba mtu huyo anafanya biashara yake kama shughuli na anajikuta
kila mara anarudia shughuli ile ile miaka yote bila kupiga hatua yoyote. Yote
haya yanatokea kwasababu “mtazamo wa biashara
yako ni wa ki-shughuli badala ya mtazamo wa ki-mchakato”.
Unapoanza kufanya
kazi au biashara yako kwa mtazamo wa ki-mchakato
inakusaidia sana kupambana na changamoto. Lakini pia uvumilivu pale matatizo
yanapojitokeza, ni rahisi kuvumilia kwakuwa unakuwa unafahamu ni wapi unaenda
na utafanya kila liwezekanalo, ili kuweza kufikia malengo au ndoto zako. Ukiwa
na mchakato wako ambao umeandikwa, unakusaidia kutokuangalia wengine
wanachofanya badala yake, wewe unakomaa na jambo moja tu la kukamilisha mchakato
wako.
Kufanya kazi
Ki-mchakato kunahitaji umakini mkubwa sana, na umakini huu hauji hivi hivi,
bali ni kwa kujenga tabia ya kujisomea vitabu na kujifunza kutokana na watu
waliofanikiwa.
Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO.
KARIBU TWENDE KAZI PAMOJA
No comments:
Post a Comment