- Waajiriwa wengi wanauza nguvukazi ikiwa bado “ghafi”
- Ukiuza nguvukazi ghafi umeuza “mtaji” na kuuza mtaji ni “kufirisika” jumla
Umaskini ndani ya
kundi la wasomi unazidi kuingia kwa kasi ya ajabu kadili siku zinavyozidi
kwenda. Kundi la watu ambao wako kwenye hatari kubwa zaidi ni hasa wale tulioko
kwenye “ajira”. Ukweli ni kwamba watu
wengi walioko kwenye ajira, kitu pekee wanachouza ili kupata kipato ni “nguvukazi” tena ambayo bado ni “ghafi”.
Uzoefu unaotokana na
tafiti zilizofanywa, unathibitisha kuwa zipo sababu nyingi zinazosababisha waajiriwa
na hasa wasomi wengi kuwa maskini. Lakini kubwa zaidi ni utamaduni wa wasomi
kuendelea kuuza nguvukazi ikiwa bado ni “ghafi” (nguvukazi ambayo haijachakatwa). Katika ulimwengu wa “uwekezaji” nguvukazi ghafi ni mtaji muhimu
sana, ambao ukichanganywa na mitaji mingine kama vile mashine, una uwezo wa
kuzalisha bidhaa na huduma zenye thamani kubwa kwa watu wengine.
Ukiuza nguvukazi
ghafi unakuwa umeuza “mtaji” wako: Waajiriwa wengi
tumeendelea kukumbwa na adha kubwa ya umasikini kutokana na kushindwa kutambua
ukweli kwamba mara nyingi kwenye maisha yetu ya ajira tumekuwa tukifanya zaidi
biashara ya kuuza mtaji tulionao (nguvukazi) kwa matajiri wenye hitaji la
mitaji.
Ikumbukwe kuwa, ili
uweze kuzalisha bidhaa na huduma unahitaji mitaji ya aina mbalimbali ikiwemo
nguvukazi ghafi. Ndiyo maana matajiri wengi wanapendelea zaidi kununua mitaji
kwaajili ya kuzalisha bidhaa na huduma, ambazo huwapatia faida kubwa sana.
Katika biashara
yoyote duniani, kuuza mtaji ni kufirisika
jumla. Kwahiyo, umasikini tulionao umetokana na kuuza mtaji wetu kila siku
tunapotumikia ajira zetu. Kwa maana nyingine waajiriwa wengi tunafirisika kila
siku ya Mungu tunapokwenda kazini.
Watu wanaouza zaidi nguvukazi
ghafi wanabaki kuwa maskini kutokana na ukweli kwamba thamani ya nguvukazi
ghafi huwa ni ndogo sana, kwasababu inapatikana kwa wingi na haina usumbufu
kuipata. Kwa mfano: ukijifanya kutoza
bei kubwa nguvukazi yako; waajiri wengi watakukimbia na chapuchapu watapata
watu wengine wenye kuuza nguvukazi ile ile kwa bei nafuu sana.
Hivi
ndivyo unavyouza nguvukazi ghafi: Unauza nguvukazi
ghafi pale unapotumia nguvu yako kufanyakazi ya kuzalisha bidhaa na huduma
ambazo siyo mali yako bali ni mali ya mtu aliyekuajiri (mwajiri). Unahitaji kufahamu kuwa, mwajiri amekuajiri ili umpatie
(umuuzie) nguvukazi ambayo ni mtaji wa kuzalisha bidhaa na huduma ambazo ni
mali yake binafsi.
Kwakuwa bidhaa
zinazozalishwa ni za thamani kwa watu wengine, basi ni wazi kwamba watu hao
watampatia pesa mwajiri wako ili kupata bidhaa; LAKINI hawatakupatia pesa wewe,
kwasababu wewe unayo nguvukazi peke yake, ambayo siyo hitaji muhimu kwa wateja
wenye pesa zao.
Ukiuza nguvukazi ghafi
unauza “muda” wako: Kwakuwa umeajiriwa kwa madhumuni
ya kutoa nguvukazi kwa mwajiri wako, basi thamani yako inapimwa kwa kuangalia muda
unaoutumia kufanya kazi. Ili uweze kulipwa ni lazima kila siku ufike kazini na kusajiri
muda wako. Usipoonekana kazini hakuna malipo yoyote, kwasababu muda wako utakuwa
hujauwekeza kwa mwajiri.
Kwahiyo, unapouza
nguvukazi ghafi basi ujue umeuza “muda” na binadamu wa kawaida hawezi kufanya
kazi zaidi ya masaa nane kwa siku. Masaa yote haya unafanya kazi bila kupumzika
na kuzalisha vitu vyenye thamani kubwa kuliko mshahara unaolipwa na mwajiri
wako.
Haijalishi, thamani
ya vitu vilivyozalishwa ni kubwa kiasi gani, mshahara wako unaolipwa unaendelea
kubaki pale pale kila mwezi. Hali hii ndiyo inakufanya wewe mwajiriwa kukosa
muda wa kufanya vitu vyenye kukuletea faida kubwa na mafanikio maishani, na
hivyo kuzidi kuwa maskini kadiri umri wako unavyoongezeka.
Ukiuza nguvukazi ghafi
huna cha kurithisha familia yako: Kama unauza
nguvukazi ghafi siyo rahisi kuirithisha kwa watu wako wa karibu, kwasababu nguvukazi
kama ilivyo haihamishiki kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine. Kama kitu
hakihamishiki ni vigumu pia kukibadilisha kwa urahisi kuwa pesa.
Hali hii inazidi
kutukumba wasomi na waajiriwa tuliowengi kutokana na ukweli kwamba unakuta
umeajiriwa kwenye kampuni kubwa na una cheo kikubwa lakini ukifukuzwa au
kufariki, haitokei mke au mtoto wako akapewa nafasi kama uliyokuwa nayo na wala
familia haiwezi kutumia vyeti vyako vya elimu kuomba kazi. Lakini kama ungekuwa
kwa mfano umeandika vitabu, hata ukifa hakimiliki ya kuendelea kuvichapisha na
kuviuza inahamishiwa kwa warithi wako na wanaendelea kufaidi sawa na wewe
ulivyokuwa ukifaidi.
Ukiuza nguvukazi
ghafi unapata hasara: Hasara kubwa unayoipata kutokana
na kuuza nguvukazi ni pale unapoishia kuuza kitu kimoja tu! Nacho ni nguvukazi.
Hali hii inakubana kiasi kwamba unajikuta unalazimika kumtegemea mteja mmoja
ambaye ni “mwajiri” na inakuwa siyo
rahisi kubadilisha mteja kadiri unavyotaka.
Endapo ukiamua
kuchakata nguvukazi yako na hatimaye kuzalisha bidhaa na huduma za thamani ni
rahisi kupata wateja wengi, ambao ndio huleta mapato makubwa.
Hasara nyingine
unayopata pindi unapouza nguvukazi ghafi ni kuendelea kubaki kwenye kundi la
watu maskini ambao wanapata kipato hai (active income), yaani unapata pesa
unapofanya kazi tu, ukiacha pesa hakuna. Endapo, ikitokea unaumwa au umesafiri
basi ujue hakuna pesa itakayoingia.
Ndiyo maana unakuta
mtu ni tajiri leo kwasababu anafanya kazi ya kibarua, lakini baada ya muda
mfupi unakuta ni maskini na kwa waajiriwa ni hivyo hivyo wanakuwa na pesa
wakiwa bado kazini LAKINI wanapostaafu ajira wanarudia kwenye hali ya umaskini
jambo ambalo huwafanya watu wengi kufa miaka michache baada ya kustaafu.
Washindi dhidi ya
umaskini ni wale walioamua kuchakata nguvukazi yao:
Ukweli ni kwamba kila mchakato wowote lazima utoe matokeo. Matokeo ya kuchakata
nguvukazi ghafi ni “bidhaa au huduma”
zenye thamani kubwa kwa watu wengine. Kitendo cha kuchakata nguvukazi kinatokana
na matumizi ya nguvu ya akiri pamoja na nguvu ya mwili kwenye rasilimali kama
ardhi, maliasili, ujuzi, pesa n.k, kwa lengo la kupata mali au bidhaa kwaajili
ya watu wengine.
Ukishapata bidhaa
zenye thamani (manufaa) kwa watu wengine, basi mara moja watakuletea pesa ili kujipatia
bidhaa na huduma muhimu kutoka kwako. Kadiri utakavyotengeneza bidhaa nyingi na
zenye thamani kubwa ndivyo utakavyopata pesa nyingi ambayo haina kikomo.
Ni wakati sasa tuamke
na tujibidishe sana kwa kuandaa mazingira yatakayotuwezesha hasa sisi wataka
mafanikio kuuza “matokeo” ya
nguvukazi badala ya utamaduni wa sasa wa kuuza nguvukazi ghafi. Ukweli ni
kwamba, unapokuwa mtu wa kuuza matokeo ya nguvukazi ambayo ni bidhaa na huduma
mbalimbali, tayari unakuwa umemaliza kazi, kinachofuatia ni kuendelea kuuza
bidhaa hizo na wakati huo huo unakwenda kuwekeza muda wako huo kwenye kuzalisha
vitu vingine, huku akiendelea kufaidi matunda ya kazi aliyoifanya mwanzo.
Kwa watu wote na hasa
waajiriwa tunaotaka mafanikio makubwa, ni lazima kila mmoja wetu ajiwekee tarehe
ya mwisho ya kuacha kuuza nguvukazi ghafi. Kila mmoja akifikia tarehe yake ya
mwisho kuuza nguvukazi ghafi, mara moja aanze kujikita katika kubadili nguvu ya
akiri na hisia kuwa bidhaa na huduma zenye kuwa suruhisho la kudumu kwa matatizo
na changamoto mbalimbali zinazowakabili watu wengine.
Kwakuwa utazalisha
bidhaa na huduma zenye kuwa na manufaa makubwa kwa watu wengine, basi na wao
watakupatia zawadi ambayo ni pesa, ili kujipatia kila kilicho bora kutoka
kwako. Tukiweza kufanikisha azima hii, basi tutatajirika kutokana na ukweli
kwamba watu wengi kwasasa wanataka bidhaa na huduma ambazo ni suruhisho ya
changamoto zao.
Wateja ni wengi ambao
wako tayari kununua kila kitu kitakachozalishwa ilimradi kina thamani kwao ~
kwahiyo soko ni kubwa. Nchi yetu inapokaribia kuingia uchumi wa kati, mahitaji
ya bidhaa na huduma zitokanazo na nguvu ya akiri/fikra zitazidi kuongezeka.
Bidhaa zenyewe ni kama vile muziki, sanaa, vitabu, program za mafunzo ya ujasiriamali/biashara/afya/kilimo/majengo
pamoja na machapisho juu miongozo mbalimbali ya uwekezaji katika mambo ya
utalii, uwindaji, gasi, mafuta, madini, kilimo n.k.
Uchumi wa watanzania
ukizidi kuongezeka na idadi ya wasomi ambao ndio wahitaji wakubwa itazidi kuongezeka
huko tuendako ~ Kwahiyo ewe mtanzania mwenzangu, anza kuchukua hatua leo, wakati
ni sasa.
Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO.
No comments:
Post a Comment