Saturday, November 14, 2015

Kupata Mapato Makubwa Kunahitaji Jambo Moja Muhimu

“Hakuna aliyewahi kulipwa pesa nzuri kwa kugundua matatizo, isipokuwa wale wanaotatua matatizo ya watu wengine wengi”
Pesa huwa inatiririka zaidi kuelekea kwa mtu yeyote aliye na suruhisho la matatizo au changamoto mbalimbali zilizoko kwenye jamii.

Kwa kawaida ni kwamba, thamani ya suruhisho lako ni......
sawa na ukubwa wa tatizo au changamoto uliyotatua. Na hii ndiyo kusema kwamba, kiasi cha pesa utakachopata ni sawa na ukubwa wa changamoto ulizozipatia suruhisho au ufumbuzi.

Kwa maana nyingine, watu wanakulipa pesa wewe, kutokana na matatizo unayotatua.

Kwa Mfano: ukitoa suruhisho la changamoto ndogo utapata pesa kidogo; ukitoa suruhisho ya changamoto ya wastani utapata pesa ya wastani; ukitoa suruhisho ya changamoto kubwa utapata pesa nyingi na ukitatua changamoto inayogusa nchi nzima utapata pesa nyingi kutoka kwa watu wa nchi nzima.

Ndiyo maana watu ambao wako kwenye kiwango cha uwekezaji hapa Tanzania na duniani kote wanaheshimika sana kwa serikali na jamii kwa ujumla. Serikali nyingi duniani, upendelea kuwapa wawekezaji misamaa na unafuu wa kodi kama njia ya kuwavutia na kuwapa motisha.

Lengo likiwa ni kuwajengea mazingira wezeshi yanayowasaidia kuendelea kutoa suruhisho za kukabiliana na matatizo au changamoto mbalimbali, kama vile ajira kwa vijana.

Kwasababu hiyo, kutokana na mchango wa wawekezaji hawa, jamii yetu imejikuta ikitoa pesa ili kulipia suruhisho mbalimbali zilizotolewa na zinazoendelea kutolewa na wawekezaji ambao ni “wafumbuzi wa changamoto”.

Kama wewe uko kwenye kundi la watu wanaotoa suruhisho kwa matatizo madogo basi huwezi kuelewa haraka dhana hii ya matajiri kupewa unafuu wa kodi. 

Serikali inapoamua kuondoa unafuu wa kodi, basi inafanya hivyo kwa umakini mkubwa na pale inapogundua kuwa imekaribia kuwaumiza watoa ufumbuzi wa matatizo makubwa nchini, basi mara moja lazima waanze kutoa misamaa ya kodi katika sekta fulani fulani zinazozalisha bidhaa na huduma zinazogusa watu wengi.

Kama wewe bado uko kwenye fikra za kijamaa, ambapo unaendelea kuiona serikali kama baba wa kukupa misaada hata kwenye mambo yako ya starehe, hili la matajiri wakubwa kusamehewa kodi huwezi kulielewa sasa hivi, LABDA utalielewa huko mbele ya safari, pale utakapoanza kujishughulisha na ujasiriamali kwaajiri ya uwekezaji.

Katika hali halisi ya maisha ya binadamu, hakuna aliyewahi kulipwa pesa nzuri kwa kugundua au kubaini



matatizo, isipokuwa wale tu wanaotatua matatizo yao na ya watu wengine.

Kwa maana nyingine ni kwamba, uwezo wako wa kugundua matatizo haukamiliki kama wewe hautatafuta suruhisho la matatizo hayo uliyoyagundua.

Watu wengi katika dunia ya leo ni wazuri sana katika kuona, kutambua, kuibua na kulalamika juu ya matatizo LAKINI bado wameendelea kubaki maskini, kwasababu kazi wanayoifanya ya kuongelea matatizo kamwe haivuti pesa kuja kwao, bali pesa itakuja kwao iwapo wataamua kuwa wafumbuzi wa matatizo na watoaji wa suruhisho ya matatizo yanayosumbua watu wengi.

Usizungumze, usitafiti kuhusu umaskini au kujisumbua sana nao. Usijali ni nini chanzo cha umaskini, huna chochote cha kufanya kuhusu chanzo chake, kile unachohitaji wewe ni kupata tiba ya ya umaskini.

Umaskini unaweza kuondolewa siyo kwa kuongeza idadi ya watu wenye uwezo wa watu ambao watawafikiria masikini, bali ni kwa kuongeza idadi ya watu masikini, ambao watakuwa na kusudi na imani ya kuwa matajiri.

Kwahiyo, jitahidi kufikiri kwa kina juu ya matatizo yaliyoko kwenye jamii yako ili hatimaye uweze kugundua na kutafuta suruhisho la matatizo hayo. Basi kwakufanya hivyo, utapata pesa kiasi kinacholingana na ukubwa wa suruhisho ulilotatua.

Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO


No comments: