Saturday, November 7, 2015

Maisha ya Ajira Yamtesayo Mjasiriamali ni Haya Hapa



 

Ni ukweli usiopingika kuwa maisha tunayoishi sasa, kwa sehemu kubwa yameegemea zaidi mfumo wa ajira na waajiriwa. Sababu mojawapo ya kuzama katika mfumo wa ajira ni....
kwamba, baada ya ukoloni na baadae ukoloni mamboleo kujikita katika bara la Africa, moja kwa moja tulianza kuathirika na mapinduzi ya viwanda uko barani Ulaya.

Zama za mapinduzi ya viwanda ndizo zilisimika mfumo wa ajira na kundi kubwa la waajiriwa tunaowashuhudia leo hii. Kundi hili la waajiriwa limekuwepo kwa muda mrefu sasa na limejijengea misingi imara na taratibu za kuendesha shughuli zake. Mfumo wa ajira umekomaa kiasi cha kuyafanya makundi mengine (wakulima na wajasiriamali), kuendesha mambo yao kwa kufuata mfumo huu wa ajira na waajiriwa.

Kwa hapa Tanzania, mfumo wa ajira umeathiri sana kundi jipya la wajasiriamali, ambalo linazidi kupanuka kadili siku zinavyozidi kwenda mbele. Hatahivyo, pamoja na kupanuka kwa kundi hili, bado watu waliowengi ndani ya kundi hili, hawajaonekana kufanya vizuri kimaisha, licha ya kwamba wao wenyewe wanazo funguo za mafanikio yao.

Zipo sababu nyingi zinazofanya wajasiriamali wengi kutokufanya vizuri, lakini kubwa zaidi ni kuendelea kufungwa na kukumbatia tabia na mifumo yote inayoongoza “ajira na waajiriwa” kwa ujumla. Kwa maana nyingine, wajasiriamali wengi wazoefu na wapya wanaendelea kufanya kazi zao kwa kufuata na kutumia mifumo, kanuni, taratibu na tabia za waajiriwa au “watu wanaopangiwa chakufanya” kila wakati.

Kitendo cha wajasiriamali kuendelea kuishi kwa kufuata mfumo mzima wa maisha ya waajiriwa, kimedhoofisha sana jitihada mbalimbali za kufanikiwa kimaisha. Wajasiriamali wengi wameshindwa kubadilika kwanza kifikra na kitabia, ili kuishi maisha halisi ya mjasiriamali. Watu wanaendesha biashara na miradi mingine ya kiuchumi huku wakiwa bado ndani ya mfumo wa ajira na waajiriwa..!!

Mfumo wa maisha ya waajiriwa ni sawa na mnyororo mkubwa ambao tusipotumia nguvu za fikra kuufungua, basi itabidi tusahau kuyaona maisha ya ndoto zetu. Ili kuanza mchakato wa kufungua mnyororo huu, inabidi tutafute funguo nyingi na tujipe muda kufungua sehemu moja baada ya nyingine. Sehemu za kuanza kufungua ziko nyingi, lakini ebu tuanze kwa kuangalia maeneo 8 yatakayo kusaidia kulegeza au kufungua mnyororo wa mfumo mbovu wa maisha ya waajiriwa:

1. Waajiriwa wana siku maalum za kupumzika: Waajiriwa wengi wana mikataba ya ajira (rasimi na isiyo rasimi). Mikataba imetaja kuwa siku za mapumziko, hutakuja kazini na badala yake utaendelea na shughuli zako binafsi. Siku hizo ni kama vile siku za jumamosi na jumapili; sikukuu za kitaifa (mf. nyerere na karume day); sikukuu za kidini n.k. Kwa mtazamo wa waajiriwa, hizi siku zote zinaitwa siku ambazo “siyo siku za kazi”.
Wajasiriamali na sisi tumelichukua hili kama lilivyo na tunaamini kwa dhati kwamba siku za mwisho wa wiki na sikukuu siyo siku za kazi. Mjasiriamali halisi hana siku (weekend) maalum ya kupumzika, anapumzika anapokuwa amekamilisha malengo aliyojipangia. Kwa mfano: Anaweza kupanga kazi ambazo zitamchukua wiki mbili au mwezi kuzikamilisha, na baada ya hapo akajipangia siku au masaa ya kupumzika.

2. Waajiriwa wana masaa maalum ya kufanya kazi: Waajiriwa wengi wanaanza kazi saa moja hadi saa mbili asubuhi na kutoka kazini saa tisa arasiri hadi kumi na moja jioni. Wajasiriamali nao, wanafanya biashara zao kwa kufuata masaa ya jua sawa na waajiriwa.

Kimsingi hakuna sababu ya wajasiriamali kufuata ratiba ya masaa ya kazi kama wafanyavyo waajiriwa, tunatakiwa kuwa huru kwa kuipanga siku yetu (masaa 24) vingine, ili ikidhi matakwa yetu kama wajasiriamali. Unaweza kuamua kuamka na kuanza kazi saa tisa usiku hadi saa nne asubuhi na kupumzika kama masaa matatu hivi na baadae kuendelea na ratiba zingine, hufungwi na wala hukatazwi na mtu yeyote.

Tutakapofikia kuipanga upya siku yetu na ikawa tofauti na mtindo uliozoeleka na unatumiwa na watu wengi, ni wazi kwamba tutaweza kuokoa masaa mengi tunayopoteza kwa siku. Ukiweza kuokoa masaa 4 kila siku, maana yake kwa wiki utakuwa umeokoa masaa 28 ambayo ni sawa na siku moja na robo. Kwa mwezi mmoja unaokoa siku 5 na kwa mwaka unaokoa siku 60 sawa na miezi miwili.

Tofauti na wengine, wewe kama mjasiriamali, utakuwa unaingiza pesa kwa muda wa miezi ya 14 ndani ya ziada kutoka kwenye miezi miwili unayofanya kazi za kuingiza kipato.

3. Waajiriwa wanapenda kufanya kitu kimoja tu: Waajiriwa wengi wanapenda kufanya kazi ya aina moja maisha yao yote, na hii ni kutokana na mfumo wa elimu ambao unakulazimisha kubobea katika fani moja, yaani “specialist”. Waajiriwa wengine wanakuwa ni wataalam waliobobea katika fani mbalimbali, na pindi wanapoajiriwa, wanatakiwa kutumia taaluma zao kuchangia katika kufanikisha ndoto au malengo ya mtu mwingine ambaye ni mwajiri au tajiri wao.

Wajasiriamali wengi wanafanya biashara ya aina moja na kwa kwango kile kile miaka nenda rudi. Unakuta mtu anafanya biashara ya kuuza mchele, lakini unashangaa mtu huyo kwa muda wa zaidi ya miaka 10 bado anauza gunia tatu kwa mwezi miaka yote.

Sababu ya mjasiriamali huyu kuendelea kubaki vile vile miaka yote, ni kwamba amegeuza biashara ya mchele kuwa “ajira” na si mradi wa kumtoa kimaisha. Kwa maana nyingine, tunaweza kusema mtu huyu anafanya biashara ya kuuza mchele lakini anaishi maisha kama mwajiriwa, kutokana na kweli kwamba yeye ni “mwajiriwa wa biashara” ya mchele.

4. Waajiriwa wanapenda kupongezwa: Kama wewe ni mwajiriwa, bila shaka umezoea kupata mrejesho juu ya utendaji wako wa kazi unazopangiwa mara kwa mara kuzifanya. Waajiriwa wengi tumezoea kuambiwa na waajiri wetu, jinsi tulivyo wachapa kazi, hata kama tunajua kuwa si wachapa kazi hodari. 


Imekuwa ni kawaida ya waajiri wengi, kuwapongeza wafanyakazi wao; kwasababu, pongezi zinatia sana hamasa na hivyo kuwafanya waajiriwa wengi kuongeza bidii ya kazi na kujituma kujituma zaidi.

Kama waajiriwa, kupongezwa na watu wengine pale tunapofanya kazi zetu vizuri ni jambo jema, kwasababu tunapopongezwa na waajiri wetu, ni kiashiria cha kwamba, waajiri wetu wanafurahishwa na kile tunachoendelea kukifanya.

Pia, tunapopongezwa na wakubwa zetu inatufanya tuendelea kujiona kuwa wenye uhalali na stahiki ya kuwepo mahali petu pa kazi. Kutokana na hali hii, watu wengi tumezoea sana na tunapenda kupongezwa na watu wengine kwa kila kitu tunachofanya maishani mwetu na hata kama kitu hicho ni kwa manufaa yetu binafsi. Kasumba hii, ipo zaidi kwa watu wengi walioajiriwa.

Wakati kwenye ajira kuna utaratibu wa kupongezwa na wale waliotuajiri, kwenye ujasiriamali hali ni tofauti kabisa. Ukiwa mjasiriamali, hutasikia kitu chochote cha “kupongezwa” na watu wengine, labda ujipongeze mwenyewe.

Pongezi zako zinakuja katika mfumo wa pesa utakazotengeneza kutokana na kazi ulizokamilisha kufanya. Na inachukua muda kabla ya wewe kuanza kupata pongezi “pesa” hizo. Kwahiyo, pongezi za kweli kwa mjasiriamali ni zile tu zinazotoka ndani yako wewe unayetenda kazi fulani.



Ukiona umefikia kiwango cha kuipongeza kazi uliyoifanya wewe mwenyewe, basi ujue umeshinda hatua moja ya kujiondolea mnyororo unaokufunga usiweze kufikia maisha bora ya ndoto yako.

Kukosekana kwa jambo la “kupongezwa” na watu wengine hasa unapokuwa mjasiriamali ndilo limesababisha watu wengi na hasa wasomi kuona kuwa ujasiriamali ni mgumu au kuonekana ni kitu chenye changamoto nyingi sana.

Matokeo yake, wale waliowahi kuingia kwenye ujasiriamali, wamejikuta wakikabiliana na hali ngumu ya maisha, kiasi cha watu wengine kuamua tena kusaka ajira, hata kama zinawalipa kiasi kidogo kuliko kiasi walichoanza kupata kutoka kwenye biashara zao binafsi.

5. Waajiriwa wanapenda kutumia uzoefu tu! Waajiriwa wanafanya kazi kwakutumia uzoefu wa mambo yaliyowahi kutokea huko nyuma. Kwenye mfumo wa ajira, vijana wanapata wakati mgumu kupenyeza mambo mapya, kutokana na kutothaminiwa michango yao eti kwasababu siyo wazoefu.

Mfumo wa ajira, unatumia sana suala la uzoefu katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya kazi. Kadili tunavyozidi kukumbatia mfumo wa kutumia uzoefu kwa kila jambo ndivyo tunavyozidi kupalilia ugonjwa hatari wa “mazoea”.

Mwajiriwa anaweza kuendelea kutumia mfumo wa uzoefu peke yake na bado mambo yakaenda, lakini si kwa mjasiriamali. Kwa mjasiriamali halisi, licha ya kutumia uzoefu, unatakiwa kwa kiasi kikubwa kuwa na uwezo wa kubuni mambo mapya na ni lazima uwe na uwezo wa kuona picha nzuri ya maisha siku za mbeleni. Na kikubwa zaidi, lazima uanze kuchukua hatua mbalimbali za kukufikisha kwenye maisha hayo mazuri unayoyaona au kuyatarajia siku za mbeleni (future).

6. Waajiriwa hawapendi kufikiri nje ya mfumo uliopo: Tangu unapoajiriwa unakuta tayari kuna mfumo utakaokuongoza kwenye utendaji wako wa kazi, kwahiyo, ili uweze kukamilisha kazi zako vizuri ni wewe kufuata maelekezo na si vinginevyo. Ukifikiria njia mbadala siajabu ukaambiwa umekiuka utaratibu.

Kwahiyo, wengi wa waajiriwa tunakabiliwa na “hofu ya kuvunja utaratibu” wa kazi na hivyo kushindwa kuwa wabunifu katika maisha, hali ambayo utusababishia umaskini. Katika ujasiriamali unatakiwa kila siku kufikiri na kubuni mambo mapya, pia unatakiwa kujifunza kila siku, ili kujijengea uwezo wa kukabiliana na changamoto ambazo huibuka kila wakati.

7. Waajiriwa wengi wanafanya kazi ambazo hawazipendi: Watu wengi katika maisha ya ajira wanafanya kazi ambazo hawazipendi hata kidogo kutokana na ukweli kwamba, wengi wanatumikia ili wapate pesa ya kujikimu. Kazi nyingi zinazofanywa na waajiriwa wengi, nyingi hazitokani na ndoto zao binafsi bali zinafanyika ili kufanikisha malengo ya mtu mwingine.

Mara nyingi, nimekuwa nikikutana na wajasiriamali wengi ambao hawapendi kazi wanazozifanya utadhani kuna mtu amewalazimisha. Kama wewe ni mjasiliamali wa ukweli unatakiwa na ni lazima upende kazi hiyo unayoifanya nje ya hapo inabidi uiache ukatafute kazi utakayopenda kuifanya. Wajasiriamali wengi wameshindwa kufanikiwa kwasababu ya kutoipenda kazi wanazofanya.

8. Waajiriwa wanajenga urafiki na watu wenye taaluma kama zao tu: Waajiriwa wengi wanatumia sana kigezo cha taaluma kuchagua na kupanga marafiki. Unakuta mtu kama ni mwalimu rafiki zake wengi ni walimu, daktari rafiki zake ni madaktari, muhasibu rafiki zake ni wahasibu n.k. Kiasi kwamba inakuwa vigumu sana kukuta mtu mweye taaluma fulani kujenga urafiki na watu wengine nje ya taaluma aliyoisomea.

Hali hii ni kutokana na ukweli kwamba watu wenye taaluma moja mara nyingi wanakabiliwa na changamoto zinazofanana hasa zile zitokanazo na waajiri wao. Kwahiyo lengo lao la kujenga urafiki pamoja ni kuimarisha mshikamano, ili kudai maslahi yao kwa mwajiri.

Wajasiriamali nao wameiga na kujenga kasumba kama ya waajiriwa, kiasi kwamba unakuta mfanyabiashara wa sokoni marafiki zake ni hao wa sokoni tena wenye bidhaa kama yake tu. 

Tabia hii kwa wajasiriamali inatukumaliza kimya kimya na hatuwezi kusonga mbele hata kidogo. Ukiwa mjasiriamali ni muhimu ukaanza kujenga urafiki au tandao na wateja wako bila kujali taaluma au kazi wanazofanya.

Tunaposema kujenga urafiki siyo kumchekea tu mteja pindi anapokuja kununua bidhaa bali tunatakiwa kwenda zaidi ya hapo. Mfano; kama mtu ni mteja wako mzuri tunakutegemea akifiwa mtumie walau salamu za pole; akiwa na sherehe mpe mchango, akiwa mgonjwa mtembelee hospitali n.k. 

Ukiweza kufanya hivyo hakika ujasiriamali utakuwa umeupatia sawa sawa. Kwa maana nyingine, wewe kama masiriamali unatakiwa kujenga mahusiano na watu wa aina mbalimbali ilimradi mnasaidiana kwa usawa mnaoridhika nao.

Wakati sasa umefika kwako wewe mtanzania hasa kijana ambaye umeamua kujikita kwenye ujasiriamali kubadilika na kuanza kuishi maisha halisi ya kijasiriamali na kuachana na mfumo yote ya waajiriwa ambayo haiendani na biashara yako unayoifanya.

Ewe mjasiriamali, unatakiwa kuanzia leo uache kufanya biashara kwa kukiendekeza mfumo wa maisha ya waajiriwa badala yake JIFUNZE kwanza undani wa mfumo wa maisha ya wajasiriamali na baadae maisha yako yafuate mfumo huo.

Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO

No comments: