Monday, May 8, 2017

Tunapanga Kuwa Masikini Namna Hii



Katika hali ya kawaida, kila binadamu anaishi kwa kupanga vitu vya kufanya. Katika zoezi zima la MPANGO, kuna makundi mawili ya watu. Kundi la kwanza ni watu waliopanga kutokuwa na mpango wowote wa maisha yao na kundi la pili ni
watu waliopanga kuwa na mpango wa maisha yao.

Kundi la watu waliopanga kutokuwa na mpango, maisha yao yanategemea zaidi imani na matumaini. Kwa kawaida watu hawa wanaamini mambo yote yanapangwa na Mungu, na kwahiyo, wao ni kufanya yale tu yanayowajia vichwani mwao kila waamkapo asubuhi.

Imekuwa ni kitu cha kawaida kusikia wengi wa kundi hili wakinena “Hata ufanyeje, Mungu kama hajapanga unajisumbua bure! huwezi kufanikiwa”. Kauli za namna hii ni za kukata tamaa ya maisha na pia yule anayeambiwa anakatishwa tamaa pia—anza kukaa mbali na wenye kutoa kauli hizi ni hatari kwa mafanikio yako.

Tabia hii ya kutokupanga aina ya matokeo unayoyataka ndiyo inayopelekea watu kuishi maisha ya kufuata upepo kama siyo mkumbo. Pia ni tabia hii inayowafanya watu kuwa na mipango ya muda mfupi na kupenda matokeo ya haraka.

Mfano: Baada ya sikukuu za pasaka nilikwenda Karagwe-Kagera. Nilichojionea ni kitu kikubwa sana. Watu wamelima sana msimu huu, karibu kila kipande cha ardhi kimelimwa na inaonekana watu watavuna maharage, mahindi, viazi mviringo n.k. Mahitaji ya mbegu za muhogo na viazi vitamu nayo yameongezeka, kwasababu kaya nyingi zinaamini mazao haya ni kinga madhubuti ya njaa.

Kwa mfano huo wa Karagwe ni kwamba wengi wao hawakuwa na mpango wa kuongeza uzalishaji, walikuwa walishasahau kupanda muhogo kama zao linalostahimili ukame, badala yake wamekuwa wanalima tu kama utamaduni.

Mipango ambayo kaya nyingi zimepanga na kutekeleza mwaka huu, naonekana haikuwepo kabla, kutokana na ukweli kwamba mipango imechochewa zaidi na majanga ya tetemeko la ardhi na ukame uliojitokeza.

Katika ziara yangu hiyo, sikuona wengi wakijishughulisha na kupanda migomba upya au kuiwekea mazingira rafiki ambayo yariharibiwa na ukame. Wengi wamewekeza nguvu zao zote kwenye mazao ya muda mfupi, na mara hii wamesahau migomba na kahawa ambayo ni ya kudumu na utoa chakula na kipato cha mara kwa mara kuliko mzao ya msimu.

Hali ya uzalishaji wa kilimo wilayani Karagwe, inawakilisha maisha ya watu wengi duniani, ambao wamepanga kutokuwa na mpango rasimi wa Maisha. Watu wasiokuwa na mpango, siku zote upanga tu kwaajili ya kukabiliana na yaliyokwishatokea tayari.

Lazima tutambue kuwa kitendo cha sisi kushindwa kuwa na mpango wa muda mrefu katika maandishi, kwa namna moja au nyingine ni kupanga kuwa maskini bila kujua”.

Kwanini tunasema ni lazima kuwa na mpango? Kwasababu kuna vitu vikubwa viwili ambavyo vina nguvu sana katika maisha yako; navyo ni MUDA na MABADILIKO. Muda una nguvu kwasababu, utake usitake lazima muda uende na mabadiliko ni hivyo hivyo, lazima yaje utake usitake .

Njia pekee ya kuweza kuwa na mamlaka juu ya muda na mabadiliko ni wewe kuwa na mpango. Binadamu wote tumepewa uwezo wa kuweza kupanga nini cha kufanya hata kama hakijatokea.

Tofauti na wanyama wengine, wao uweza kuishi kwa kufuata matukio au hali ya wakati huo. Wanyama hawana kabisa mpango unaoweza kuwaongoza kwenda kwenye mwelekeo wa maisha wanayoyataka. Ikitokea malisho yameisha wao uhamia sehemu nyingine na hiyo sehemu nyingine wakikuta wanyama wanaowawinda watarudi huko ambako walihama mwanzoni.

Ajabu na kweli ni kwamba watu wengi wanaishi kwa kufuata mabadiliko yanayojitokeza kwenye mazingira yao. Kikubwa hapa ni wewe kubadilika na siyo kubadilishwa na mabadiliko. Ukisubili kubadilishwa na mabadiliko maana yake mabadiliko yatakubadilisha jinsi yanavyotaka.

Yawezekana wewe unajiona uko sawa na mambo yako yanaenda vizuri, lakini ujue kuwa ukiwa na maisha ambayo huna mpango ulio katika maadishi, hapo ujue kuwa lazima ufuate kile ambacho mabadiliko yatakuletea na siyo wewe unavyotaka mabadiliko yawe. Ndiyo maana tunaambiwa kwamba ufunguo pekee wa mtu kuweza kudhibiti MUDA na MABADILIKO ni kuandika “mpango”.

Mpango maana yake ni kwamba wewe mwenyewe unapanga aina ya mafanikio unayoyataka kabla ya kuanza kuyatafuta. Mafanikio yoyote makubwa lazima upange kuyapata. Kwahiyo, tuseme kuwa mafanikio yako yapo tayari, kinachosubiliwa sasa hivi ni mpango kazi wako. Kama umepanga kutokuwa na mpango—tambua kuwa “Usipopanga kupata mafanikio, basi ujue unapanga kimya kimya kuwa masikini”.

Mpango ndio unakupa mwelekeo mzuri wa unakotakiwa kwenda. Kama wewe ndiye unayeshika upinde na mshale basi “Mpango” ndio unasaidia kuelekeza wapi mshale uende—wewe unachagua upande gani mshale upige. Athari za kutokuwa na mpango ambao unatuongoza juu ya nini cha kufanya ni pale tunapojikuta tunadhibitiwa na maisha badala ya sisi kuyadhibiti maisha.

Mpango unakupa nguvu na uwezo wa kuuamrisha muda ukufanyie nini. Ikiwa umepanga kutokuwa na mpango, basi ujue muda ndio utakupangia nini cha kufanya. Inafika kipindi fulani muda wenyewe unakulazimisha kufanya vitu ambavyo hupendi kuvifanya. Ulikuwa na nafasi ya kuamrisha muda, lakini hukuitumia, sasa ni zamu ya muda wenyewe kukuamrisha cha kufanya.

Ukiwa huna mpango unakuwa ni mtu wa kuishi kwa matumaini. Lakini kumbuka kuwa watu wengi wanaoishi kwa matumaini mara nyingi ni maskini. Kwahiyo, unahitaji mpango ambao ndio utakujengea imani ya kufanikiwa.

“Imani ni bora zaidi kuliko matumaini” jitahidi kuwa na imani juu ya mpango wako, huku ukizidi kuutekeleza kwa nguvu zako zote—hakika mafanikio uliyolenga kupata lazima yatokee tu!

Habari njema ni kwamba Mungu yupo anasubili mpango wako ili aubariki. Mafanikio yako makubwa yapo, lakini utayapata tu endapo utaandika leo mpango wako. Ukishindwa kupanga unapanga kuwa maskini—habari ndio hiyo!.

Kuendelea kupata maarifa mengi bonyeza MAARIFA SHOP kwaajili ya kujifunza zaidi.


No comments: