Monday, June 19, 2017

Tambua Viingiza-pesa Sahihi Kupata Uhuru wa Fedha





Habari njema ni kwamba kila mmoja wetu anayetafuta mafanikio ya kiuchumi amepewa uhuru na wigo mpana sana wa kuchagua njia na mbinu zitakazo mpeleka mpaka kufikia UHURU WA KIPATO (fedha). Unapoanza safari yako ya kutafuta “uhuru wa kipato” ni wazi kwamba ni muhimu sana kwako kuweza....

kufahamu aina ya “Viingiza-Pesa” ambavyo vitakupatia pesa bila kikomo. Kwa maana nyingine ni kwamba huwezi kuwekeza kwenye kila kitu na ukafanikiwa—siyo rahisi.

Suala la kuwekeza kwenye “Kiingiza-Pesa" chochote hochote ni suala ambalo kimsingi ni la binafsi zaidi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kuna vitu vingi au maeneo mengi ya kiuwekezaji. Suala la kutafuta aina ya “Viingiza-pesa (au vile vitegauchumi ambavyo vinaingiza pesa mfukoni) ni suala ambalo wengi wetu tunao uwanja mpana wa kuweza kuchagua. Kila kundi la “viingiza-pesa lina faida na hasara na kila kiingiza-pesa kinahitaji kiasi tofauti cha muda, jitihada, nguvu na elimu.

Makundi manne ya viingiza-pesa ni yapi?
Kwa ufahamu tu ni kwamba kila uwekezaji tunaoufanya kwa njia moja au nyingine unaangukia kwenye makundi manne makubwa. Watu wengine wanawekeza katika makundi yote manne au wengine wanawekeza kwenye mojawapo tu! Kwa kawaida kuna njia mbalimabali za uwekezaji na za kujenga utajiri. Na mara tu ukiongeza elimu yako juu ya pesa, utakuwa katika nafasi nzuri sana ya kuelewa juu ya viingiza pesa vipi bora kwako. Lakini, ili kukusaidia wewe kuanza, hapa chini kuna baadhi ya makundi manne ya “viingiza-pesa” ambayo ni maarufu na yanajulikana.

Namba moja: Kundi la uwekezaji katika karatasi Kundi hili linaitwa la makaratasi kwasababu, uwekezaji unakamilika kwa wewe kujaza makaratasi na kulipa pesa kiasi unachoona kinafaa. Mfano; ukinunua hisa kwenye kampuni kama VODACOM, unapewa kitu kama cheti au mkataba unaokuthibitisha wewe kwamba ni mwanahisa wa kampuni husika. Pia, ukishakuwa umenunua hisa shughuli ya kufanya wewe imeishia hapo isipokuwa unabaki kufuatilia maendeleo ya kampuni basi. Kwenye hisa wewe haufanyi kazi tena badala yake kampuni ndiyo inaendelea kufanya kazi kwa niaba ya wanahisa na hivyo kuwajibika kwao katika kuwatengenezea faida mwisho wa siku.

Tunaposema uwekezaji wa karatasi, tunamaanisha vitu kama hisa, hatifungani (bond), vipande kama vya mfuko wa UTT, pesa yako ya akiba kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii (NSSF, PSPF, PPF n.k). Viingiza-pesa vingine katika kundi la karatasi ni pamoja na mifuko ya dhamana ya uwekezaji na biashara ya kubadilishana pesa. Uwekezaji katika kundi hili unalipa kwa namna mbili. Moja ni faida kutokana na ongezeko la bei uliyonunulia na kwa upande mwingine ni malipo kupitia gawio litokanalo na faida iliyotengenezwa na kampuni husika. 

Waliofanikiwa katika uwekezaji huu ni wale wanaowekeza mfurulizo kwa muda mrefu na hivyo kufaidika na gawio kubwa ambalo linatolewa na kampuni bila kikomo, ilimradi kampuni husika inaendelea kutengeneza faida. Uzuri wa malipo ya gawio ni kwamba yanakuja pasipo wewe kufanya kazi tena, hata ukiwa umelala, umesafiri, au unaumwa pesa inaingia tu!

Ndiyo maana watu wengi upenda kuwekeza kwenye viingiza-pesa kama HISA, au kwenye soko la hisa. Hivi ndivyo viingiza-pesa rahisi kuweza kuingia na kutoka. Kuna wakati mtu mmoja anawezakuwa amewekeza kwenye hisa, hatifungani, vipande vya UTT, bima n.k. na mtu huyo akifikiri kwamba amewekeza kwenye mikondo tofauti ya kuingiza pesa, LAKINI kimsingi siyo kweli, kwasababu vyote hivyo nilivyotaja hapo juu vitu ambavyo viko kundi moja tu ambalo ni la “uwekezaji katika karatasi”. Kwahiyo, kama ni uwekezaji kwaajili ya kupunguza hatari inayoweza kutokea mbeleni utakuwa hujafanya kitu, kwani bado uwekezaji wako utakuwa kwenye eneo moja na hatari za mtikisiko wa uchumi zikitokea zitakuathiri kwa kiasi kikubwa.

Namba mbili: Uwekezaji katika kundi la Bidhaa
Tunaposema uwekezaji kwenye bidhaa nazo ziko kwenye makundi madogo madogo kama vile madini (dhahabu, shaba fedha, n.k); vyakula (nafaka, kahawa, na sukari), mali-ghafi (mafuta, gesi, pamba n.k). Uwekezaji katika kundi hili, mara nyingi ni kwa faida itokanayo na kupanda na kushuka kwa bei, kwani unaweza kununua kwaajili ya kuuza baadae bei ikipanda. Kama wewe bado ni mgeni katika aina hii ya uwekezaji, anza kidogo kidogo na kuza na kujenga elimu yako ya pesa.

Namba tatu: Uwekezaji katika kundi la Biashara
Ili ni eneo la viingiza-pesa ambalo watu wengi wanazidi kulifahamu na kulichamngamkia, hasa kutokana uwepo wa matangazo ya kwenye runinga. Unaweza kuwekeza kwenye biashara zako mwenyewe au kwa mwingine au kampuni binafsi. Jambo la maana linaloongelewa hapa ni wewe kuweza kurudisha pesa yako uliyowekeza, wawekezaji wenzako na wale wote waliokukopesha pesa. Unachotakiwa kufanya ni kufanya utafiti, kuchambua kwa kina mradi husika, washirika, jinsi ya ufadhiri wa mradi wako, timu ya watu watakaofanya menejimenti kabla ya kuamua kuwekeza kwenye biashara husika.

Namba nne: Biashara ya Majumba
Biashara katika majumba inalipa kwa namna mbili hasa—kupitia kodi ya pango na ongezeko la thamani (kununua na kuuza). Kwa biashara ya majumba, unapata uwezo wa kutumia pesa ya watu wengine kununua viingiza-pesa vingine. Unaweza ukawa na nyumba ukaitumia kukopa pesa benki na ukanunua nyumba nyingine na bado ile uliyoiweka rehani ukapata mteja mwenye kuinunua kwa pesa zaidi ya ile unayodaiwa na benki. Mteja akipatikana analipa ile tofauti alafu inayobaki kama deni la benki anaendelea kuirejesha taratibu mpaka litakapoisha.

Unadhani ni kiingiza-pesa kipi kitakupa UHURU WA KIPATO?
Linapofika suala hili la kuchagua kiingiza-pesa kwaajili ya uhuru wa fedha, ni uamuzi binafsi ambao unategemea zaidi lengo lako mahususi la maisha. Na wakati mwingine inaweza kuwa inavutia sana mwanzoni, lakini wewe jitahidi kuanza kidogo. Kikubwa ni wewe kuweka malengo yanayotekelezeka na kupimika, fanya utafiti wa kina huku ukijitahidi kuongeza elimu yako ya fedha, lakini mwisho ni kuchukua hatua.

Watu wengi (nikiwemo mimi) wameanza kubadili maisha yao kwa kuwekeza kwenye viingiza-pesa, na wewe ninaamini unaweza kufanya hivyo.

Ni hatua gani moja utachukua leo kwenye safari yako kuelekea UHURU WA KIPATO?
Ili kupata elimu na taarifa nzuri wakati huu unapoanza safari yako ya kwenda kwenye UHURU WA KIPATO, ni wakati muhafaka sasa ukajiunga— bonyeza hapa INGIA ili kuwa miongoni mwa wafuatiliaji wa mtandao wa MAARIFASHOP.

No comments: