Monday, July 10, 2017

Dawa ya Ujasiri wa Kukopa Pesa Benki Inapatikana Hapa



Kila ukigusia suala zima la watu kukopa pesa, wengi uonyesha wasiwasi wao mkubwa juu ya kitu mkopo. Kutokana na mtazamo uliopo juu ya mkopo, inaonekana kuwa mkopo ni kitu cha mwisho mtu kuweza kukifanya hasa hapa Tanzania. Ukweli ni kwamba jamii yetu imejaa woga juu ya mikopo hasa ile itolewayo na benki za biashara. Niseme kama wewe ni mjasiriamali wa kweli, uhitaji kuwa mwoga, bali
unatakiwa kutafuta kitu ambacho kitakopa pesa kwa niaba yako.

Kitu pekee kinachoweza kukopa kwa niaba yako ni “biashara”. Hapa, namaanisha kuwa biashara ni mradi au mfumo wowote unaoweza kufanya pesa ikatiririka kuja kwako. Biashara siyo lazima iwe ni ile tu ya kununua vitu na kuuza kwa bei ya juu. Biashara yaweza kuwa shamba la mazao, mifugo, usindikaji unga, kutengeneza matofari, kuuza pesa za kigeni n.k. ilimradi kuwe na mfumo wa kuzalisha bidhaa au huduma, ambazo hatimaye zitauzwa kwa watu wengine.

Katika mazingira ya uchumi wa soko, “biashara” ndiyo kitu kimojawapo kinachoweza kukusaidia kukopa pesa kwa niaba yako. Unachotakiwa kufanya ni kuhakikisha unaifanya biashara yako kuwa HAI, kwani kwakufanya hivyo unakuwa umeiwezesha biashara yako kuwa na uwezo wa kukopa.

Kwa bahati mbaya wengi wetu tunawaza kwanza kukopa sisi kama sisi alafu ndio tufanye biashara. Kwa maana nyingine ni kwamba wazo la kukopa linatangulia kabla ya biashara yenyewe. Katika hali ya uhalisia inatubidi tubadili mtazamo juu ya mkopo. Mtazamo wetu uwe ni kuzifanya biashara zetu ziweze kuchukua mikopo na kulipa zenyewe, siyo sisi kulipa mikopo tuliochukua kwaajiri ya biashara.

Lazima suala la kusimamia biashara litiliwe mkazo, ili kuhakikisha biashara zetu zinakuwa na uwezo mkubwa wa kumaliza matatizo yake yote bila kugusa pesa zetu binafsi. Tunahitaji kuitazama biashara yetu kama mtu binafsi (binadamu). Tuhakikishe biashara inakuwa ni kitu kinachojitegemea, kitu chenye uhai, kitu kinachokua. Imani yangu inanituma kuamini kwamba endapo tutafanya biashara zetu katika mtazamo wa namna hii, ni wazi kwamba hatutaweza kuogopa kukopa mkopo wowote ule. Kinachotufanya tuogope ni kila mara tunawaza kukopa sisi kama sisi na siyo biashara tunayotaka kufanya au tunayofanya tayari.

Ndiyo maana kila mara tunapofikiria kukopa picha inayotujia akirini ni pamoja na hali itakavyokuwa baada ya sisi kushindwa kurudisha mkopo. Hapa tunaona vitu vya hatari tupu, unaona nyumba yako au gari lako binafsi vikipigwa mnada, unaona vitu vyako vya muhimu vikiuzwa na wewe kubaki bila kitu cha maana. Ukishaona picha ya namna hii mara moja hamu na shauku ya kukopa inaisha kabisa kutokana na ukweli kwamba unajawa na woga wa kukopa, mwisho unaamua kuendelea na maisha yako yale uliyoyazoea. Lakini, kama hiyo haitoshi unageuka kuwa muhubili kwa watu wengine juu ya ubaya na hatari za mtu kukopa pesa. Katika hili unahakikisha kila mtu aliyekaribu na wewe, na yeyote atakayerogwa akakuomba ushauri unampa eti uzoefu wako katika mkopo, wakati wewe hujawahi kuchukukua mkopo popote.

Hiyo ndiyo aina ya jamii tunayoishi nayo, jamii ya watu waoga, ambao hawana uzoefu unaotokana na kutenda wala kuthubutu. Kama wewe umeamua hakikisha usizame sana kwenye madhara ya mkopo yaliyowapata watu wengine, kwa maana haujui nini kilitokea mpaka wakashindwa kurejesha mikopo yao. Wewe unachotakiwa kufanya ni kujikita katika kuimarisha biashara yako iendelee kuwa na nguvu kubwa ya kujitunza na kujiendesha. Pia, katika mawazo yako ondoa kabisa dhana ya kwamba wewe ndiye unalipa mkopo na badala yake weka dhana ya kwamba biashara yako, ndiyo inayolipa mkopo na siyo wewe.

Kwanini tunasema biashara ndiyo inayolipa mkopo?
Unapokuwa umekwenda benki na ukapewa mkopo, tambua kwamba hiyo pesa uliyopewa siyo ya kwako bali ni pesa za watu wengine waliojiwekea akiba benki. Hapa maana yake ni kwamba, biashara yako ndiyo inabeba dhamana ya kulipa mkopo kutokana na shughuli za kiuchumi zinazofanywa na hiyo biashara yako. Biashara yako ndiyo inabeba jukumu la kuzalisha bidhaa au huduma ambayo inauzwa kwa watu wengine kwa faida. Sehemu ya faida itokanayo na biashara ndiyo utumika kulipa mkopo, mpaka hapo wewe hujausika kwa namna yoyote ile kulipa mkopo.

Mara nyingi utasikia watu wanasema eti! Ukichukua mkopo unawafanyia benki yaani unapata faida kidogo. Napenda kukuhakikishia kwamba ukifahamu mbinu za kufanya biashara yako iwe hai na yenye afya kwa vyovyote vile faida itakuwa kubwa tu. Lakini, pia hata kama faida ni ndogo, unapaswa kukumbuka kuwa pesa iliyotumika kuleta hiyo faida unayoita kidogo haikuwa ya kwako, ilikuwa ni pesa ya watu wengine. Kwa maana nyingine tunaweza kusema pesa tunayopata kama faida kutoka kwenye mikopo ni pesa ya bure, kwahiyo usiumie sana pale unapoanza kurejesha pesa kwa wale waliokukopesha mtaji.

Mpendwa msomaji wa mtandao huu wa MAARIFA SHOP utakubaliana na mimi kuwa suala hapa siyo kukopa wewe kama wewe bali ni kuacha biashara yako ikope. Kuweza kuifanya biashara yako iwe na uwezo wa kukopa kwa niaba yako ni suala linalohitaji kujifunza. Njia mojawapo ni kujaza kichwani mwako taarifa zilizochambuliwa kwa kina na siyo kutumia taarifa za majukwaani, vijiweni, barabarani n.k. Kwa mafunzo ya kuboresha fikra zako endelea kuwa karibu na mimi kwa kutembelea mara kwa mara mtandao huu wa MAARIFA SHOP

No comments: