Monday, June 5, 2017

Unaongeza Idadi ya Marafiki Wanyonyaji kwa Njia Hii



Katika Maisha ya binadamu ni kitu cha kawaida na muhimu kuwa na marafiki. Kwa karne nyingi, watu wametumia njia mbalimbali katika kuchagua marafiki wakuwanao karibu kila inapobidi. Katika kuchagua marafiki, wengi wetu tumekuwa tukitumia vigezo mbalimbali. Mfano ni
vigezo vya ujirani, kusoma shule moja, kuwa na dini moja, kuzaliwa wote, ukoo, kabila, chama cha siasa, mnafanya kazi ofisi moja, kuwa na taaluma inayofanana n.k. 

Utumiaji wa vigezo hivi, ndio umesababisha wengi wetu kuwa na tabia ya kutafuta marafiki tu mnalingana kiuchumi au unaowazidi kiuchumi. Hadi sasa, watu wengi bado wanachagua marafiki kwa kutumia vigezo vile ambavyo vimekuwepo tangu zamani. Ikumbukwe kuwa kwa mazingira yale ya zamani, yawezekana vigezo hivyo vilikuwa na maana, na vilifaa sana wakati huo. Lakini, uzoefu umeonyesha kuwa kwasasa haviwezi kukupatia marafiki mtakaosaidiana kiuchumi. Kwa vigezo hivi vya zamani, ni wazi kwamba tutaendele kupata marafiki ambao kiuhalisia ni “wanyonyaji”.

Marafiki wengi tulionao ni kwaajili ya kusaidiana wakati wa shida na raha. Lengo la kuchagua marafiki kwaajili ya kusaidiana, limekuwa ni jambo jema sana, isipokuwa tatizo liko kwenye hicho mnachosaidiana na marafiki wako wa karibu. Wengi tumekuwa tukisaidiana pamoja, wakati wa misiba, sherehe, kuoneana huruma, kusaidiana wakati wa majanga mbalimbali n.k. 

Ukiangalia kwa undani juu ya mambo mengi tunayosaidiana, unagundua kuwa, mengi ni yale yanayochukua pesa yetu mfukoni kwa wote (mtoaji na mpokeaji). Kwa maana nyingine ni kwamba, mfumo wa urafiki tulionao ni ule unaotufanya wote tuishiwe pesa bila kujua—yaani sisi pamoja na marafiki zetu. 

Kinachotokea baada ya hapo, ni wote kuendelea kudhoofika kiuchumi taratibu na mwisho kuwa kundi kubwa la mafukara, ambao hawawezi tena kuwa na uwezo wa kusaidiana kama hapo mwanzo. Kwa maneno mengine ni kwamba, tunachoambulia kwenye mfumo wetu wa urafiki ni umoja wa watu wasiojiweza labda kuoneana huruma basi!

Uzoefu unaonyesha kuwa, ukishakuwa umezungukwa na kundi kubwa la marafiki wasiojiweza, moja kwa moja unakuwa na tabia ya kujenga UKUTA dhidi ya watu walio na hali nzuri ya kiuchumi. Kila unapofahamiana na mtu mpya, mara moja unaanza kuchunguza kiwango chake cha utajiri. Pindi unapogundua kuwa mtu huyo anakupita kiuchumi, mara moja unasitisha harakati zozote za kujenga mahusiano ya karibu naye. Sana sana, wengi wanachofanya ni kuungana na marafiki wenzao wasiojiweza, kufanya kila wawezalo kuwaangusha kiuchumi, wale wanaodhani wanawazidi—japo jitihada zao hizo, zimekuwa zikigonga mwamba.

Mfumo uliopo sasa, ni ule ambao unakuwa na marafiki wakati wa kutumia, lakini wakati wa kutafuta na kuzalisha pesa, kila mmoja anafuta peke yake. Hali hii ya kila mtu kutafuta peke yake, inafanya wengi kuona ugumu hasa linapofika suala la kutafuta pesa. Wengi wanaamini kuwa, kama Mungu hajapenda huwezi kupata. Habari njema ni kwamba Mungu alishakukabidhi funguo za kupata pesa, na pia anasubiri umwambie kazi unayofanya, ili akubariki. Utafutaji wa kila mtu kivyake, ni changamoto kubwa inayotukabili kwasasa na ninachelea kusema kwamba, ni vigumu kufanikiwa kwasababu, kazi ya kutafuta mafanikio ya kweli, inahitaji timu ya watu wenye kusaidiana katika kutimiza malengo ya kiuchumi.

Kwa muda mrefu sasa nimejifunza kupitia video za wanyama wawindao—hasa simba. Unakuta ikifika muda wa kuwinda, wanakwenda kushambulia pamoja na mara nyingi wamekuwa wakifanikiwa. Wakishamaliza kuwinda wanaketi na kula pamoja. Baada ya hapo, kila mmoja anaweza kupumzika au kutembea tembea peke yake. 

Kwa binadamu, hasa Tanzania, hali ya utafutaji kiuchumi ni tofauti na Wanyama kama simba. Kwetu sisi, suala la kutafuta pesa ni la binafsi. Yaani unakwenda kutafuta peke yako, lakini ukirudi nyumbani unakutana na watu wanaosubili hicho ulichopata na bila kujali yaliyokukuta wakati wa utafutaji. Mara nyingi wanataka uwagawie na ikibidi wewe ujinyime, ilimradi wao wapate— “huu ni unyonyaji uliopitiliza”.

Jiulize ni mara ngapi, kila ukirudi nyumbani umekuwa unakutana na kadi za michango ya sherehe kutoka kwa ndugu, jamaa na marafiki. Viongozi wa dini nao, hawaangahiki na wewe wakati wa kuinua uchumi wako, lakini kila ukirudi nyumbani unakuta nao wanasubili mgao wao. Wanachama wenzako (chama cha kusaidiana) nao wanasubili mchango wako, kwasababu kuna mwenzenu amepatwa na matatizo. 

Je? Kwa mtindo huu, unadhani kuna njia yoyote ya wewe kuinuka kiuchumi? Ukweli ni kwamba huwezi tena kuinuka; kwa lugha ya vijana, wanasema “huwezi kutoboa”. Maana yake ni kwamba, kiwango cha umaskini kitaongezeka kadiri umri wako utakavyoongezeka. Ndugu, kamwe usisingizie uzee kuwa ndio umekusababishia umaskini, bali ni yale mambo na maamuzi madogo madogo ambayo unayafanya kila siku, ndiyo yanaungana na kuleta hali mbaya ya kiuchumi uzeeni— "usisahau kuwa uzee ni dhahabu"!

Kwasasa, watu wengi tunakabiliwa na tatizo la kupata marafiki wa kiuchumi. Wengi hatuna mbinu wala elimu ya namna ya kujenga marafiki ambao kusudio kuu ni kuinuana na kusaidiana kiuchumi. Tunahitaji kuchagua marafiki wapya, ambao msingi mkuu utakuwa ni kwaajili ya kusaidiana kiuchumi na mambo mengine ya kimaisha yatafuatia. Siyo vibaya kuwa na marafiki, ila kwasasa tunahitaji kukuza orodha ya marafiki ambao tutawachagua kwa vigezo vinavyendana ukubwa na hali ya ndoto zetu za Maisha bora na uhuru wa kipato.

Marafiki uliokwisha kuwanao endelea nao, lakini wekeza na kuelekeza zaidi nguvu na rasilimali zako katika kutafuta na kujenga marafiki wapya bila kujali sehemu wanakotoka, undugu, dini, na misimamo mingine ambayo haina tija. Jambo la msingi ni kwamba hakikisha, marafiki hao wapya wawe ni watu ambao wako tayari kuungana na wewe katika kufanikisha malengo ya kiuchumi. 

Hakikisha marafiki wapya wawe ni wale wanaoendana na ndoto, maono na malengo yako ya muda wa kati na mrefu. Jitahidi kukuza orodha ya marafiki wa namna hii, kwani hawa ndio watakuwa kwenye timu yako ya kutafuta ushindi dhidi ya umaskini. Tofauti na hapo utabakia kukimbia mbio za sakafuni—ambazo mwisho wake huwa ni ukingoni mwa ukuta.

Ni matumaini yangu kuwa, kuna kitu cha msaada umekipata kwenye Makala hii na kwakuwa kazi ya kujifunza ni endelevu, basi endelea kuufanya mtandao wako wa 
MAARIFASHOP kuwa miongoni mwa kimbilio lako katika kusaka maarifa ya kukufikisha kwenye mafanikio unayostahili. Kujifunza zaidi bonyeza neno “NIUNGE, ili kuwa karibu zaidi na mtandao huu muhimu.

No comments: