Monday, July 31, 2017

Muuzaji na Mnunuzi Nani ni Mfanyabiashara?


Katika maisha yetu ya kila siku hapa duniani, kuna watu wanaofikiri na kuamini “sisi siyo wafanyabiashara wao ni wafanyabiashara”. Wengi wanaamini kuna kundi fulani la wafanyabiashara. Kutokana na mtazamo huu juu ya biashara, wengi wanajiaminisha kuwa wanaweza kuishi maisha mazuri bila kuwa wafanyabiashara. 

Watu wengi wanadahani mfanyabiashara ni
yule mtu anayekuja kwako kununua bidhaa au huduma (mnunuzi). Imekuwa siyo kawaida hasa hapa Tanzania kukuta mzalishaji au muuzaji anayejiona na kujichukulia kama mfanyabiashara. 

Wazalishaji wengi wa vitu mbalimbali wanadhani kazi ya kufanya biashara siyo yao, kwasababu wanaamini kwamba biashara ni shughuli maalumu inayofanywa na watu maalumu. 

Hali hii ya mzalishaji kutokujitambua kuwa na yeye ni mfanyabiashara, pengine inatokana na kutumia muda mwingi na nguvu nyingi wakati wa mchakato mzima wa kuzalisha bidhaa. Kwa kawaida, mtu akishazalisha bidhaa yake anajiona kuwa amemaliza kazi. Matokeo yake anajitoa kwenye fikra ya kwamba bado yeye ni mfanyabiashara. 

Mzalishaji anapokuwa amejitoa ufahamu wa kujitambua kama mfanyabiashara, moja kwa moja inamjengea picha kichwani kuwa mfanyabiashara pekee ni yule atakayekuja kununua bidhaa au huduma yake. Ndiyo maana wazalishaji wengi wa bidhaa wamejenga tabia ya kujiona bora zaidi na kudhani kuwa mnunuzi ndiye mwenye shida na bidhaa au huduma yake. 

Kila wakati mzalishaji anapomfikiria mnunuzi anamuona kama mtu ambaye anafanya kazi kidogo na pengine anadhani mnunuzi huyo hastahili kulipwa hicho analipwa. Pia mzalishaji anapomuona tu mnunuzi, kwa haraka haraka anapata hisia ya kwamba mnunuzi huyo anakwenda kumuuzia mtu mwingine na atajipatia pesa haraka sana kwa kazi ndogo. Hisia za namna hii juu mnunuzi, ndizo humfanya mzalishaji kushindwa kujiona na kujitabua kuwa na yeye ni mfanyabiashara kama alivyo mnunuzi.

Katika ulimwengu wa biashara na masoko ni vizuri tukafahamu kuwa, uzalishaji wa bidhaa yoyote ni mchakato ambao ni sawa na mnyororo unaoungwa kutokana na kufanyika kwa shughuli mbalimbali. Mnyororo unaanzia uzalishaji hadi kwa mtumiaji/mlaji wa mwisho. Katika mnyororo wa bidhaa, kunakuwa na kubadilika badilika kwa umiliki wa bidhaa husika. 

Kwa mfano: Mtu anayeuza mbegu za mahindi kwenye mnyororo anakuwa ni mmiliki namba moja; namba mbili ni mkulima (mzalishaji); namba tatu ni mnunuzi wa nafaka; namba nne ni muuzaji wa unga; namba tano ni mnunuzi wa unga (mwenye duka/kiosk) na wa mwisho ni mlaji wa ugali au mtumiaji wa unga.

Kwahiyo, mkulima kama mzalishaji na muuzaji, umiliki wake wa mahindi (nafaka) unakoma mara moja pale anapomaliza kupokea pesa kutoka kwa mnunuzi wa nafaka. Baada ya hapo mwenye mali anakuwa ni mnunuzi wa nafaka, naye huyu akiuza kwa mwenye mashine ya kusaga unga, hapo hapo umiliki wake unakoma akishapokea pesa. Anayesaga unga naye akiuza kwa mwenye duka, umiliki wake wa unga unaishia hapo, mwenye duka akiuza kwa mlaji wa mwisho umiliki wake unaishia hapo na mwisho yule anayekula ugali ndiye anafunga mnyororo wa bidhaa ya mahidi tangu mahindi yalipotoka kwa muuza pembejeo yakiwa kama mbegu na sasa ugali.

Mfano huu wa mnyororo wa zao la mahindi unatufundisha somo muhimu sana kwamba “biashara ni kununua na kuuza". Haijalishi imekuchukua muda gani kupata bidhaa, suala ni kwamba mwisho wake utauza tu kwa mtu mwingine. Huwe ni mkulima, mnunuzi wa nafaka, muuzaji wa reja reja, msindikaji (mwenye kinu cha kusaga), lazima utanunua na kuuza utake usitake.

Kwanini ni Lazima Tuuze?
Kinachotufanya tuuze bidhaa zetu ni kutokana na ukweli kwamba, kila mmoja kwenye mnyororo wa thamani anakuwa na ukomo wa uwezo wake wa kuongeza thamani ya bidhaa husika.  

Mfano: mkulima hana uwezo wa kuzalisha mbegu bora, lakini anao uwezo mkubwa wa kuzalisha mahindi yanayofaa kwa chakula (nafaka), hapa anaongeza thamani kwa kuzalisha nafaka kwa wingi kukidhi mahitaji ya chakula.

Mnunuzi wa nafaka yeye anaongeza thamani kwa kusaga unga na kufungasha vizuri, tayari kwa walaji kupata chakula (ugali). Mwenye duka/kioski yeye anaongeza thamani kwenye bidhaa ya unga kwa kusogeza unga karibu na walaji, pia anaongeza thamani kwa kuhakikisha unga unapatikana kwa muda wote unapohitajika. Mifano yote hii, inatuonyesha kuwa, katika maisha yetu ya kila siku, kila mtu ni mfanyabiashara

Kwahiyo, kama kila mtu ni mfanyabiashara, maana yake ni kwamba kila mmoja anatakiwa kuzalisha bidhaa kwa mtazamo wa kuuza. Ukizalisha kwa mtazamo wa kuuza ni bora zaidi, kwasababu unapata ari, nguvu na shauku kubwa ya kufanya kile unachofanya. Pili, ukizalisha kwa mtazamo wa kuuza ni rahisi kuzalisha bidhaa yenye ubora wa hali ya juu, kwani wakati wa mchakato wa uzalishaji, utazingatia sana mahitaji ya wale wateja wako watarajiwa.

Ukitambua kuwa wewe ni mfanyabiashara, hapo hapo utagudua kuwa wewe siyo bora kuliko wanunuzi badala yake utagundua kuwa wote muuzaji na mnunuzi ni sawa mbele ya biashara, kwasababu wote mnayo masilahi katika kile mnachotaka kubadilishana. Mnunuzi anataka kumiliki bidhaa ya muuzaji na muuzaji anataka alipwe pesa ili aachie umiliki kwa mnunuzi.
Wazalishaji, lazima wajue kuwa nao ni wafanyabiashara, lazima wajue kuwa wanahitaji pesa kwaajili ya kupata mahitaji mengine, kwasababu, maisha siyo bidhaa hiyo moja uliyonayo. Wazalishaji lazima watambue kuwa, ili tupate kuishi maisha mazuri tunahitaji bidhaa na huduma zaidi ya moja. 

Ili kupata bidhaa na huduma zaidi ya moja, tunahitaji kuuza bidhaa yetu moja, ili kupata pesa ya kununua bidhaa na huduma zaidi ya moja. Mwisho ninasema “hakuna aliye juu kati ya muuzaji na mnunuzi japo kuwa pesa nyingi itapatikana endapo utajifunza kuwa mfanyabiashara”—ni muhimu ufanye hivyo sasa!

Kwa mafunzo zaidi juu ya biashara na uwekezaji weka e-mail yako kwa kubonyeza maneno haya: MAARIFA SHOP.

No comments: