Monday, July 24, 2017

Hatari ya Kushindwa Kupanga ni Kama Hii



Nikiwa mmojawapo wa washiriki wa kikao cha kamati ya mradi wa kilimo siku ya tarehe 13/07/2017, mwenyekiti wa kamati alifungua kikao na kukumbusha wajumbe kuwa mojawapo ya majukumu ya kamati ni pamoja na kupanga namna bora ya uendeshaji wa shughuli za mradi. 

Katika kusisitiza hilo alisema “kushindwa kupanga ni kupanga kushindwa”. Maneno haya yalinigusa sana na yalinifanya kutafakari zaidi juu ya maana ya maneno haya katika maisha yetu ya kila siku.

Katika maisha kuna vitu ambavyo vipo na havitegemei uwepo wako. Vitu ambavyo havitegemei uwepo wako ni
vingi; mfano ni ulimwengu ambao unajumuisha ardhi, nyota, jua, mwezi, viumbe, Hali ya hewa na hewa yenyewe, mvua, ukame, mabadiliko ya tabia ya nchi, muda n.k. Vyote hivi ni vitu ambavyo tumezaliwa tukavikuta. Mahusiano na mwingiliano wa vitu vyote hivi ndani ya ulimwengu huu, ndivyo kwa kiasi kikubwa vinatengeneza mazingira yanayokuzunguka kila siku. Mazingira haya yanaweza kuwa aidha ni hatarishi au wezeshi kwako.

Kwa maneno mengine ni kwamba, uwepo wa vitu ambavyo havitutegemei unatulazimisha kujipanga sawa sawa kama kweli tunataka kuishi maisha mazuri. Ukweli ni kwamba, binadamu yeyote kwa kiasi kikubwa anategemea sana vitu ambavyo havimtegemei. 

Kwakuwa sisi binadamu ndio tunategemea vitu vya ulimwengu kuishi vizuri, mara nyingi tunakuwa katika hali fulani ya kinyang’anyana rasilimali. Katika mazingira ya namna hii ni kuwa na ndoto ya maisha mazuri unayoyataka na mpango madhubuti wa namna gani utapata maisha hayo. Mpango unakuwezesha wewe kuweza kuchuma vizuri chochote unachokihitaji katika ulimwengu huu.

Sisi kama binadamu wawajibikaji tunahitaji kujipanga, ili kuona ni namna gani tutafaidika na hali hii ya asili. Maisha bora yatategemea zaidi na namna tunavyojipanga wenyewe kwa lengo la kujiandaa lakini pia kwa lengo la kufaidika na fursa zinazotokana na mazingira. Watu wengi hawana muda wa kupanga na hivyo kujikuta wanapokea kila hali inayojitokeza. Unapokuwa mtu wa kupambana na vitu ambavyo vimekwishatokea, ujue utahitaji nguvu nyingi kupita kiasi ili kuweza kukabiliana na changamoto zilizopo.

Usipopanga kuna mambo ambayo lazima yaendelee. Kwa mfano; lazima watoto waendelee kukua, lazima waendelee kuhitaji shule, matibabu, chakula bora, serikali lazima iendelee kukudai kodi kwa namna moja au nyingine. Kanisani bado nao wanaendelea kukutaka utoe matoleo na sadaka pia. Misiba inaendelea kutokea, kuugua kunaendelea bila kuwepo au kutokuwepo kwa mpango wako.

Kama yote niliyoyataja hapo juu yanaendelea kutokea bila kujali kuwepo au kutokuwepo kwa mpango wako, maana yake wewe kila wakati utajikuta unaishi katika hali ya kutoa pesa ili kukidhi shinikizo la mahitaji ya lazima. Kwa maneno mengine ni kwamba, wewe unakuwa ni mtu unayeishi kwa kusukumwa na matukio yenye kuchukua pesa kwako tu basi. Mwisho wake unajikuta huna muda wala fikra yoyote inayohusu jambo muhimu lenye kukuletea maendeleo makubwa. Huwezi tena kufanya shughuli zenye kukuletea pesa za kustawisha na kurutubisha maisha yako, kwasababu kila ukitafuta pesa tayari inakuwa na kitu cha kuichukua mara tu inapoingia mfukoni mwako.

Usipopanga unaruhusu hali duni ijitokeze kwako kwa kiwango kikubwa sana. Kwahiyo, usipopanga maana yake umepanga umaskini ujitokeze kwako, LAKINI ukipanga maana yake umepanga umaskini usitokee kwako—kwamba umaskini ushindwe na ulegee!

Kwahiyo, lazima tuamue kupanga kama kweli hatutaki na tunauchukia umaskini. Utaratibu wa kujiwekea mpango katika maandishi ni mzuri sana, kwasababu mpango ndiyo unakupa dira na ramani. Ramani ndiyo inakuwezesha wewe kupita njia sahihi kwenda huko unakotamani kwenda. Mpango unakufanya ujue ugumu na urahisi wa kazi iliyoko mbele yako, pia ni rahisi kwako wewe kujua mwisho wa safari yako.


Unapokuwa na picha kamili juu ya kile unachotakiwa kufanya ili kupata maisha bora na uhuru wa kipato, kila wakati unakuwa na hamasa na sababu thabiti ya wewe kufanya kazi muda wote. Ukishindwa kupanga unajikuta ni mtu ambaye upo upo tu huna hata hamasa yoyote ya kufanya kazi. Muda mwingi unakuwa ni mtu ambaye anapenda sana kusema “nitafanya kesho” au “mambo yangu yakitulia nitafanya hivi” au “nikipata muda nitafanya hiki na kile”. Kila wakati unakuwa ni mtu wa kuongea tu na kujiahidi juu ya mambo mazuri ambayo yanaishia kwenye kauli basi. Matokeo yake unakuja kugundua kuwa miaka inazidi kwenda na ukipima miaka kumi unagundua hali yako ya kiuchumi imerudi nyuma zaidi kuliko ilivyokuwa hapo awali (kabla ya miaka kumi). Kila wakati likumbuke hili “Usipopanga umepanga umaskini uje kwako na ukipanga umepanga umaskini usikanyage kwako”.

Kwa mafunzo Zaidi juu ya mpango wa kufaidi rasilimali za ulimwengu weka e-mail yako kwa kubonyeza maneno haya: MAARIFA SHOP.

No comments: