Monday, May 4, 2015

Shule ya “Maisha Yako” Inataka Malengo na Mipangilio Yako Iwe ni kwa Maandishi


Kumbukumbu ni kitu muhimu sana katika kujenga misingi imara ya mafanikio yoyote yale. Watu tuna kumbukmbu nyingi na za kila  aina ndani ya vichwa vetu. Kutokana na hazina hii ya kumbukumbu, watu wengi uzitegemea sana katika kufanya maamuzi ya shughuli mbalimbali za kila siku. Lakini, utafiti umebaini kuwa, huwezi kupata mafanikio makubwa ambayo ni endelevu, kama huna ndoto ya aina ya maisha unayoyataka. Kwa walio wengi yawezekana wana ndoto kubwa, lakini ndoto hizo hazitimii kwasababu mbalimbali, na sababu mojawapo ambayo ni muhimu ni kuendekeza utamaduni na tabia ya kutekeleza mipango kutokea kichwani.

Kumbuka kuwa, kila siku ubongo wetu unapokea na kutunza kumbukumbu nyingi sana, kiasi kwamba, inakuwa vigumu kwako wewe kuweza kukumbuka mambo muhimu ambayo unahitaji kuyatimiza. Matokeo yake, unajikuta kila siku unashughulika na vitu vipya tu! Au kulingana na mambo yanavyojitokeza. Mara nyingi shughuli zako zilizo nyingi zinakuwa hazina mwendelezo wa pamoja. Hii ni hatari sana kwa mafanikio na pia, ni vizuri ukafahamu kuwa, kuendelea kukumbatia tabia hii ya kutegemea kumbukumbu ambazo ziko kichwani, itakuwa ni vigumu sana kufikia maisha ya ndoto yako.

Tunapoongelea kumbukumbu hatuamanishi zile za mapato na matumizi tu! bali ni kumbukumbu zile ambazo zimejikita kwenye mambo ya fursa, malengo ya muda mrefu na mfupi, aina ya maisha unayotaka kuishi miaka (mtano, kumi, ishirini au zaidi) ijayo, mambo yanayotakiwa kubadilishwa ili wewe uweze kusonga mbele, mambo unayohitaji kujifunza n.k. Ni wazi kwamba kumbukumbu za aina hii, nyingi tayari unazo kichwani, lakini hazijaweza kukusaidia pengie kwasababu, nyingine ukumbuki kama unazo kwenye kichwa chako.

Kwahiyo, mwanzo wa kuweza kupanga na kutimiza malengo makubwa katika maisha ni kuwa na kumbukumbu za mawazo mazuri lakini yaliyoandikwa kwenye karatasi, kwani huu ndiyo msingi mkubwa na mzizi mkuu wa mafanikio. Watu wengi waliofanikiwa wanasema kumbukumbu ambazo  “zimeandikwa kwenye karatasi” ndizo za uhakika na ambazo unaweza kuzitegemea  kukuongoza kwenye safari yako ya kuelekea maisha unayoyataka. Ili kuweza kupata na kutunza kumbukumbu, huitaji kuwa na kitu kingine zaidi ya “nidhamu” ya kufanya vitu rahisi na ambavyo ni vya kawaida kila siku.

Wajasiriamali waliofanikiwa wanakwambia kwamba, kama ukipata au kusikia wazo zuri kuhusu jambo fulani lenye mashiko kwenye ndoto zako, shika kalamu na daftari na uliandike maramoja. Alafu wakati wa jioni au usiku kukiwa kumetulia, jaribu kulipitia daftari lako. Fikiria wazo ambalo lilibadilisha maisha yako, wazo lililonusuru ndoa yako, wazo lililo kutoa kwenye wakati mgumu, wazo lililokusaidia ukafanikiwa. Kazi hii endelea kuifanya mara zote bila kuacha. Kwahiyo, uwe ni mkusanyaji wa mawazo mazuri, mkusanyaji wa uzoefu kwaajili ya biashara na mahusiano yako na kwa maisha yako ya mbeleni (future).

Tunahitaji kuanzia sasa tujenge utamaduni na tabia ya kuandika kila wazo zuri tunalolipata kila siku; iwe kulifikri wenyewe, kusikiaau kuona kwa marafiki au watu wengine, iwe ni kulisoma kutoka vitabuni n.k. Ili uweze kulifanikisha hili, ni vyema ukakumbuka kuwa tabia ya kuweka na kutunza kumbukumbu za mawazo mazuri katika maadishi haitakuja ghafla kwako, isipokuwa itakuja kama utaianza kuifanya taratibu lakini ukaifanya kila siku kwa kipindi kirefu, ili uweze kuizoea. Kumbuka tulipokuwa shuleni, walimu walitufundisha kuwa na daftari kwaajili ya kuandika notisi na kabla ya kuandika tulihimizwa kuanza tarehe. Na hapo mambo yote tuliyokuwa tukifundishwa tulikuwa tukiyaandika na ndiyo maana wakati wa mitihani ulipokaribia, ilikuwa ni rahisi sana kujikumbusha kwa kupitia notisi zilizoko kwenye daftari na hatimaye kuweza kufahuru mitihani.

Tunapokuwa tumemaliza shule na kuanza maisha ya kujitegemea na kujiongoza wenyewe, tunahitaji kuwa “wanafunzi wa maisha yetu” na hapa ndipo tunatakiwa kuwa na daftari maalumu la kuandika na kuweka kumbukumbu za mawazo na mipangilio mingine ya jinsi tulivyojipanga kufanikisha ndoto zetu. Uzuri wa kuwa na daftari hili, ni kwamba, ni rahisi sana kurithisha watoto wako pamoja na vizazi vingine.


Ukweli ni kwamba, inaleta changamoto sana kuwa “mwanafunzi” wa maisha yako, maisha ya mbeleni, mwisho wako (unakotaka kufika). Kumbuka utakapo amua kuwa mwanafunzi katika shule iitwayo “maisha yako” ni tofauti na shule zingine ulizowahi kusoma. Hapa katika shule ya “maisha yako”, wewe mwanafunzi ndiye kila kitu, hakuna wa kukuamsha, wala wa kukuogoza bali wewe tu ndiye unajiongoza, unajihimiza na unajiwekea presha mwenyewe. Ni kutokana na yote haya ndiyo maana daftari la kumbukumbu za mipangilio ya maisha ya ndoto yako ni muhimu sasa kuliko siku zote. Ni muhimu tuamke, na tuweke msingi imara kwaajiri ya kufikia mafanikio makubwa.

Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO

No comments: