Monday, November 6, 2017

Kwanini Tunahitaji Umakini Kwenye Biashara?



 
Biashara au uwekezaji wowote unahitaji msingi imara, ili kuweza kukua na kuleta faida kwa mmiliki. Ukiwa na msingi imara kiwango cha hatari ya kushindwa kinapungua kwa kiasi kikubwa.

Chukulia mfano wa ujenzi wa nyumba; ukiwa unajenga nyumba unahitaji msingi imara, ili kuepuka nyumba yako kuanguka baadae. Ili kuufanya msingi wa nyumba yako kuwa imara, lazima unahitaji..
kufahamu ni vitu gani vimetengeneza msingi ulionao. Lengo hapa nikutaka kuongeza kile ambacho kitaufanya msingi wako kuwa imara zaidi.

Ikiwa umejenga nyumba yako kwa fito na miti, lazima msingi wako utakuwa dhaifu na mwisho wa yote, nyumba yako itaanguka. Ukijaribu kulinganisha mfano huu wa nyumba, unaona kuwa mambo huwa hivi hivi linapokuja suala la uwekezaji au biashara. Katika kujipanga kuwa mwekezaji au mfanyabiashara mkubwa, unatakiwa kuanza na mambo muhimu, sawa na kujenga msingi imara, kwa lengo la kupunguza hatari ya kupata hasara.

Ukitathimini kwa kina, utaona kuwa watu wengi tunashindwa kwenye uwekezaji, kwasababu mtazamo wetu juu ya uwekezaji ni tofauti kabisa. Watu wengi wanafikiri kuwekeza ni jambo tu la kutenga na kuweka pesa kwenye mradi fulani kwa matarajio ya kupata faida kutoka kwenye mradi husika. Kinyume chake ni kwamba, kile watu wanachodhani ni uwekezaji, kumbe ni kamali au bahati na sibu. Ndiyo maana watu wengi wamefirisika licha ya kwamba waliwahi kuonekana wawekezaji wakubwa.
Kwa mfano; kuna baadhi ya wafanyabiashara walinunua mahindi kwa bei kubwa wakati yameadimika na wakaendelea kuyatunza licha ya kwamba bei iliendelea kupanda, kiasi kwamba kama wangeamua kuuza baada ya mwezi mmoja wangeweza kupata faida. Lakini wao kwa kipindi chote cha kupanda bei walikataa kuuza. Sasa imefika wakati mahindi yameanza kushuka bei kutokana na kuingia kwa mahindi mapya sokoni na sasa hawana namna inabidi wauze kwa hasara na wengine kwa faida ndogo sana.

Kwa upande mwingine, wawekezaji wazoefu walifahamu misingi muhimu ya biashara hii ya mazao, walikataa kununua mahindi ya kutunza kwa bei kubwa, wengine waliuza mahindi waliyokuwa nayo kwenye stoo zao na kujipatia faida nzuri.

Tofauti iliyopo kati ya kundi lililopata faida na lile lililopata hasara ni kwamba ni suala tu la “umakini” na “maarifa”

Linapokuja suala la biashara na uwekezaji kinacho mtofautisha mbabaishaji (mcheza kamali) na mwekezaji/mfanyabiashara makini ni ule uwezo wa kufahamu mambo muhimu ya msingi katika biashara. Kufahamu na kufuata misingi hii, kunasaidia sana katika kuondoa hatari ya kupata hasara katika uwekezaji wowote utakaoufanya.

Hatahivyo, kuna kiwango fulani cha hatari ambacho uambatana na kila biashara unayoiona, lakini kwa kujikita katika mikakati madhubuti ya uwekezaji na kupanga kuzuia njia za kusababisha hasara, hatari ya kupoteza inaweza ikapungua kwa kiwango kikubwa. Kimsingi, hatari kubwa unayokabiliana nayo ni kushindwa kwako kujihusisha moja kwa moja na uboreshaji wa elimu yako ya fedha.

Lazima ujielimishe na kuendelea kujifunza kila siku. Kwahiyo, kama wewe ni mgeni katika uwekezaji na biashara anza taratibu kufuata misingi hii minne, ambayo waliofanikiwa huwa wanaifuata:

Biashara lazima iweke pesa mfukoni mwako: Kitu cha kwanza lazima kuangalia uwezo wake wa kutiririsha pesa; pili ni uwezo wake wa kuongezeka thamani. Mwekezaji aliyefanikiwa, ni yule anayejikita katika kujenga kiingiza pesa chake au (asseti yake). Kwahiyo, uwekezaji wowote ambao hauweki pesa kwenye wallet yako ni mzigo/deni na siyo kitegauchumi.

Biashara moja lazima ijitegemee/isimame peke yake: Biashara haiwezi kudumu kwa kutegemea pesa kutoka kwenye biashara nyingine—Maana yake ni kwamba, huwezi kutumia utajiri wa biashara moja kutunza biashara ambayo iko kwenye madeni na hali ngumu. Kila biashara, lazima itengeneze faida yake yenyewe na uwekezaji ni hivyo hivyo.

Udhibiti uwepo kila inapowezekana: Katika biashara, ni lazima kudhibiti mapato, matumizi, na madeni. Kila wakati lazima kutafuta namna ya kuboresha uwekezaji na kuongeza thamani yake au mapato kutoka kwenye biashara husika. Hapa ndipo umuhimu wa kujifunza kila siku unapokuja. 


Lazima kuwe na mpango mkakati wa kuuza: hii ni ngumu kwa wengi: Kila wakati fahamu ni wakati gani utauza kabla ya kununua. Maamuzi haya lazima yazingatie vigezo kama: bei, upatikanaji, mahitaji mapya ya wateja, matukio ya kitaifa na kijamii n.k

Yote hayo yakifanyika vizuri yanasaidia sana kujenga msingi imara wa biashara yako au uwekezaji wako. Na biashara iliyojengwa katika msingi imara ndiyo ina uwezo wa kujiendesha bila kunyonya biashara zako nyingine.

Ujenzi wa biashara, lazima uendane na wewe kujiendeleza kwa kujifunza kila siku mambo mapya yahusuyo biashara unayofanya. Endelea kujifunza na kupata maarifa kila siku kwa kutembelea mtandao wako wa MAARIFA SHOP. Pata makala mpya kila zinapochapishwa kwa kuweka barua pepe yako baada ya kubonyeza neno hili hapa; MAKALA.

No comments: