uzoefu umeonyesha kuwa, pamoja na kulipa gharama zitokanazo na makosa fulani fulani bado makosa hayo hayo ni fursa nzuri sana ya kujifunza na kuweza kuwa bora zaidi. Hapa chini kuna mfano halisi wa jinsi nilivyoweza kujifunza kitu kikubwa baada ya kufanya makosa:
Siku ya Jumapili ya tarehe 12/11/2017, nilisafiri kutoka Nyakanazi (Biharamulo) kwenda Kasulu (Kigoma). Mara likatokea basi kutoka Kahama, nikaamua kwenda kuuliza kama inawezekana kusafiri na basi hilo. Kondakta aliponiona kama mtu mwenye nia ya kusafiri, akaniwahi kwa kuniuliza ninakokwenda. Kusikia hivyo bila hata ya kutafakari nikamwambia nakwenda Kasulu, naye akasema nauli hadi Kasulu ni shilingi 15,000/-.
Baada ya kulipa nauli niliingia kwenye gari na safari ikaanza mara moja. Kwa mshangao mkubwa, tulipofika stendi kuu ya mabasi mjini Kibondo, tukaambiwa mwisho wa gari ni hapo stendi na wakasema abiria wote tuliolipia nauli ya moja kwa moja hadi Kasulu, tuingie kwenye gari (TOYOTA ICE), ambalo lilikuwa limepaki pembeni tayari kwenda Kasulu. Hapa ndo kusema kuwa “tulifaulishwa”. Baada ya kupanda ICE hiyo, ndipo nikagundua kuwa wale tuliofaurishwa, tulikuwa ni wachache (watu wanne tu). Changamoto ikawa ni kwamba, lazima tusubili abiria wengine waje kujaza gari ndipo liweze kuanza safari ya kuelekea Kasulu. Kwa jinsi ilivyokuwa siku ya jumapili, niliona kwa haraka haraka niliona hiyo ICE itachelewa sana kuondoka (labda saa kumi jioni badala ya kuondoka saa sita na nusu mchana). Baada ya kukaa stendi kwa muda wa saa nzima bila kuona abiria anayekuja kupanda ICE hiyo, ndipo nilianza kulaumu na kulaani, nikajiuliza maswali mengi yasiyokuwa na majibu; “kwanini hawa vijana wamenifanyia yote haya”? Hawajanitendea haki”, “wamenidanganya” …... nikawa na kila aina ya malalamiko yote unayoyajua.
Baada ya muda akiri yangu ilifunguka nikagundua nimefanya MAKOSA makubwa wakati wa kulipa nauli. Nilitakiwa kulipa nauli hadi Kibondo, nauli inayobaki ningepanda gari ambalo ningeona linafaa kupanda. Kimsingi, mimi ndiye nilikuwa mjinga, kwasababu sikujua taratibu na kanuni zisizo rasimi kwenye sekta ya usafirishaji wa abiria. Nilitakiwa kuuliza mwisho wa basi ni wapi—sikufanya hivyo, badala yake, niliishia kujibu kile nilichoulizwa na kondakta. (kondakta: unasafiri kwenda wapi? Mimi: Kasulu; kondakta: nauli ni 15,000/-; lipa nauli tiketi hii hapa; Mimi: Nikalipa….).
Baada ya kukiri makosa yangu kwenye usafiri niliamua kuwajibika kwa kulipa tena nauli ya shilingi 8,000/- na nikapanda BASI JINGINE lililokuwa likitokea Mwanza ambalo lilisimama stendi (Kibondo) kushusha abiria. Safari hii sikufanya kosa nilikuwa wa kwanza kumuuliza kondakta kama basi lake linafika Kasulu.
Ukifuatilia kisa hiki kizima utaona ni kama vile nililipa shilingi 8,000/- zaidi. Lakini, ukweli ni kwamba pesa hiyo haikulipwa kama nauli bali kama gharama au hada (karo) ya mwanafunzi ambaye alitakiwa kulipia masomo na kupata majibu ya kile ambacho nilikuwa sijui kwenye masuala yote yanayohusu usafiri hasa wa magari ya kuungaunga (kupokezana vijiti).
Baada ya akiri yangu kuichukulia shilingi 8,000/- kama “hada/karo” ya kufuta ujinga, hali ile ya kulalamikia upotevu wa pesa haikuwepo tena. Niliona ilikuwa ni haki hizo pesa zaidi nizilipe, kwasababu, kuanzia siku hiyo nilikuwa tayari nimejifunza jinsi ya kuwa makini wakati wa safari hasa unapotumia magari ya kuungaunga.
Jifunze Kubadili Makosa Kuwa Masomo
Ukiyachukulia makosa kama masomo, uwezo wako wa kutatua au kurekebisha makosa yako unaongezeka. Mfano mzuri ni kama nilivyoeleza hapo juu, endapo siku hiyo nisingeamua kulichukulia KOSA langu kama somo, pengine ningechelewa sana kwenda nilikokuwa naenda. Kwasababu ningeona ni kupoteza pesa kwa kulipa nauli mara mbili.
Sisi kama viongozi wa maisha yetu, ni muhimu sana kuyachukulia makosa kama fursa ya kujifunza kitu kipya juu ya hicho unachofanya, iwe ni kwenye maisha au biashara. Katika kitabu cha “Before You Quit Your Job” (bofya KITABU kupata nakala)—Bwana Robert Kiyosaki anasema; makosa ni kama alama za barabarani zinazoamrisha kusimama. Kwamba makosa ni kama yanakwambia “wewe, sasa ni muda wa kusimama…. tulia kidogo…. kuna kitu hujui …. Ni wakati wa kuacha na kufikiri kwanza. Bwana “Kiyosaki” pia anaendelea kusema kwamba “makosa ni ishara inayokuonyesha kwamba sasa ni muda wa kujifunza kitu kipya ambacho ulikuwa hukijui hapo mwanzo”
Kwahiyo, kila wakati unapofanya makosa, simama, chukua hatua ya kujifunza kitu kipya. Kama kuna kitu hakiendi vizuri kwa jinsi ulivyotegemea au kimekwenda kinyume na matarajio yako, jipe muda wa kufikiri kwa kina. Ukishagundua somo lililokuwa limejificha ndani ya mfuko wa makosa, lazima utakuwa mwenye shukrani kwa makosa hayo.
Waajiriwa na Wajasiriamali Wana Falsafa Gani Juu ya Makosa?
Waajiriwa na wajasiriamali ni watu wanaoishi dunia mbili tofauti na falsafa yao juu ya neno “makosa” ni tofauti sana. Kwa waajiriwa kufanya makosa ina maana kwamba kuna kitu hujui kabisa na wewe ni mjinga. Ndiyo maana mwajiriwa yeyote akifanya makosa, mara nyingi anajifanya hajafanya makosa yoyote; anakataa na anasema makosa yamefanywa na watu wengine siyo yeye. Mwajiriwa atafanya kulaumu wengine juu ya makosa yake—Jambo hili lipo sana kwenye maofisi mengi ya umma na ya watu binafsi.
Ni waajiriwa wachache sana wanaochukulia makosa kama fursa ya kujifunza na kuongeza uwezo wao wa kufikiri. Kila mara waajiriwa tunakuwa makini hadi kupitiliza, huku tukijitahidi kukwepa kufanya makosa, kwasababu tunaamini makosa nikitu kibaya sana.
Kwa maneno mengine ni kwamba watu wengi wanaoishi kwa kukwepa kufanya makosa mara nyingi ni watu wa kulaumu na kulalamikia wengine. Watu wa namna hii ni wagumu sana kukubali kwamba wamefanya makosa, matokeo yake huwa ni vigumu sana kwao kupata muhafaka wa makosa yaliyotendeka jambo ambalo husababisha makosa yale yale kujirudia mara kwa mara.
Wajasiriamali wao wanaamini makosa ni kitu kinatokea nje ya ufahamu wako ulionao kwa wakati huo. Pia, wanaamini makosa ni kitu ambacho kinaweza kumtokea mtu yeyote bila kujali kisomo, umri na uzoefu wa mtu. Kutokana na Imani hii ya wajasiriamali juu ya kitu “makosa”, wemejifunza kitu kimoja cha muhimu katika biashara au maisha, nacho ni “kuyakiri makosa”.
Kitendo cha kukiri makosa ndicho uwapa uwezo wa kusimama na kuanza tena pale inapotokea wakaanguka. Unapokubali kuwa makosa yametendeka na wewe pengine umehusika, ndipo akiri yako inafanyakazi katika viwango vya juu zaidi na hivyo kupata suruhisho la kudumu juu ya matatizo na changamoto zinazokukabili.
Sasa ni wakati wa kufikiri juu ya maisha mazuri unayoyataka. Ni wakati wa chukua hatua (anza kufanya kwa vitendo), huku ukitambua kuwa makosa yatakuwa ni sehemu ya mchakato wa kufanya hicho unachofanya. Kila yatakapojitokeza makosa badala ya kutafuta mchawi, wewe yafungue makosa hayo, ili hatimaye uweze kunufaika na (masomo, ukweli na fursa)—yawezekana vyote hivi viko ndani ya mfuko wa makosa. Unatakiwa kuacha kulalamika, fungua mfuko wa makosa sasa na endelea kusonga mbele.
No comments:
Post a Comment