“Haikugharimu chochote kujiunga na wengi, inakugharimu kila kitu kusimama peke yako” ~ CYPRIDION MUSHONGI
Katika hali ya kibinadamu watu wote tunataka maisha mazuri. Maisha mazuri ni hali fulani ya kuishi, ambapo mtu binafsi anakidhi mahitaji yake na kuridhika na hiyo hali. Lakini, ukweli ni kwamba hali ya Maisha tunayoishi kwa kiasi kikubwa ni.. duni na wengi haturidhiki na hali hii. Tunaishi maisha ambayo hatuna fursa ya kuchagua.
Ni Maisha ambayo huwezi kula chakula unachokitaka kila wakati; huwezi kusafiri kwenda popote unapotaka; huwezi kuishi kwenye nyumba unayoitaka; huwezi kufanya kazi unayoipenda; huwezi kuchagua mtu wa kufanyanaye kazi, huwezi kupumzika siku yoyote unayotaka wewe n.k. Kwa ufupi tunaishi maisha ambayo siyo huru.
Maisha yetu yamekuwa ni yale ya utegemezi wa hali ya juu; tunaambiwa cha kufanya; tunapewa maelekezo ya jinsi ya kutenda yale tutendayo; tunategemea tuambiwe ni elimu gani inatufaa; tunategemea tuambiwe umuhimu wa kulinda afya zetu n.k. Matokeo yake tumejikuta tuko katika hali ambayo hutuna nafasi tena ya kuchagua tunachotaka katika Maisha yetu.
Leo hii familia nyingi hazina uhuru wa kipato; maisha yao yanayodhibitiwa na watu wengine, na hivyo kuishi kwa kunyanyasika. Imefikia hatua lazima tuseme imetosha, kwasababu hatuwezi kuendelea kuishi maisha ya namna hii.
Maisha enzi za mababu zetu yalikuwa mazuri kutokana na ukweli kwamba babu zetu walikuwa ni watu ambao waliwajibika kikamilifu kwa kila jambo ambalo lilijitokeza katika Maisha yao. Babu zetu walikuwa na roho ya “kujitegemea” na “ujasiri”. Uwezo wa kubeba majukumu yao yote na hatimaye kujitegemea ndiyo imeleta maendeleo tunayoyaona sasa katika dunia iliyo huru.
Wazee wetu, hawakuwa na roho ya utegemezi na hawakusubili mtu mwingine yeyote kuwambia kitu cha kufanya, kama ilivyo siku hizi. Walitambua majukumu yao na zaidi walifanyakazi waliyoipenda bila kupangiwa na mtu kitu cha kufanya. Walikuwa ni watu ambao walibeba majukumu yao yote kwa kila kitu kilichotokea maishani mwao.
Ilikuwa ni hiyo roho ya ujasiri na kujituma kwao, ndiyo ilichochea maendeleo ya binadamu ambayo tunayaona sasa. Najiuliza maswali mengi; leo hii iko wapi roho ya kujitegemea kama ilivyokuwa enzi za mababu zetu?; iko wapi tena “roho ya kujituma na kufanya mambo yote unayoyataka bila kuambiwa na mtu mwingine?”. Iko wapi leo _"roho ya kujiongoza na kujiambia nini cha kufanya?".
Nauliza ilipo roho ya kujitegemea kwasababu, kila mmoja wetu amezaliwa nayo. Wote tuna zawadi hiyo, isipokuwa kuna watu wachache ambao wanaitumia na kuna wengine wengi wameamua kutoitumia.
Kuna kanuni ya ulimwengu inasema hivi; _"kitu ambacho ukitumii kinapotea"_. Kwa mfano; Imani ambayo haitumiki inapungua, usipotumia ujuzi ulionao unaupoteza, usipotumia uhuru ulionao unaupoteza. Maana yake ni kwamba, kutokutumia roho kujitegemea ambayo tumejaaliwa kuwa nayo ndani ya mwili, kumesababisha watu wengi kupoteza hiyo zawadi.
Kupotea au kufifia kwa roho ya kujitegemea ndio imekuwa chimbuko la kuwa na jamii ya watu tegemezi. Wanaozalisha ni wachache kuliko wanaokula kiasi kwamba wazalishaji wachache na serikali wanalemewa mzigo mkubwa na hivyo kushindwa kuwahudumia wategemezi.
Miaka kabla 1960, watu chini ya asilimia tano tulifanyia kazi watu wengine au serikali. Watu zaidi ya asilimia 95 tulikuwa ni watu tuliobuni kazi na kufanya kazi zetu wenyewe. Hii ina maana kwamba tulikuwa ni watu tuliojitegemea. Sasa ni miaka takribani 80 baadae imekuwa ni kinyume chake kwamba sasa hivi wategemezi wanazidi kuwa wengi kuliko wanaojitegemea.
Hii ndio kusema kwamba tumebadilika kutoka jamii ya watu waliojitegemea na kuwa jamii ya wategemezi. Taratibu taratibu tumebadilika kutoka kuwa watu waliobeba majukumu yao yote. Walikabiliana na kila kitu kilichotokea maishani na kuwa watu ambao tumekuwa wepesi na wazuri sana wa kulaumu watu wengine kwa kila tatizo linalotukuta.
Ule ujasiri, nguvu na ari walivyokuwanayo babu zetu vyote vimefifia. Mababu zetu hawakufikiria wala kuuliza juu ya nani atajali maisha yao, walichokuwa wanauliza ni fursa ya kuwa huru na uwezo wa kujali maisha yao na familia zao.
Kupata mafanikio hasa uhuru wa kipato unahitaji sana kufufua roho ya kujitegemea. Katika kujaribu kufufua roho ya kujitegemea anza kwa kuhoji uhalali wa wewe kuishi hayo Maisha uliyonayo. Pili pata picha halisi ya Maisha unayoyataka, weka mkakati na anza kidogo kidogo kufanyakazi hadi kufikia Maisha ya ndoto. Katika kufikiria Maisha ya ndoto yako jitahidi kuwa na mtazamo wa muda mrefu. Hakikisha wakati wote unakuwa na mtazamo chanya.
Nitaendelea kukuletea makala zenye thamani zitakazokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno NITUMIE MAKALA kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO.
No comments:
Post a Comment