Saturday, May 1, 2021

KAZI Inaleta AJIRA na AJIRA Inamaliza KAZI ni Kweli?

"KAZI uzaa ajira lakini AJIRA haiwezi kuzaa kazi" ~ CYPRIDION MUSHONGI


    Mpaka sasa ajira bado ni tatizo kubwa kwa watu wengi hasa vijana nchini Tanzania na kwingineko duniani. Kukosekana kwa ajira kwa sehemu kubwa kunachangiwa na wadau wengi wa maendeleo kushindwa kubaini chimbuko halisi la ajira. Hali hii inafanya mikakati mingi ya kuongeza ajira kutofanikiwa. Wapo wngine wanaodhani suruhisho la ajira ni... kujenga viwanda vingi, wengine wanadhani ni kilimo, wengine utalii; wengine wanadhani ni kwenye TEHAMA. Matokeo yake suala la ajira limekuwa ni la kujaribujaribu bila mafanikio ya kuridhisha.

    Kitu cha kushangaza ni kwamba leo hii bado jamii inakabiliwa na matatizo na changamoto mbalimbali za kimaisha. Katika uhalisia wa mambo binadamu anavyojibidisha kutatua matatizo aliyonayo ndivyo ajira zinapatikana. Hapa namaanisha kwamba katika michakato ya kutatua matatizo na changamoto, binadamu anapata cha kufanya.
    
Swali langu ni; je, Nani mwenye jukumu la kuleta cha kufanya? Katika kujibu swali hili, wengi wamepata jibu la kwamba kuna mtu fulani tofauti na wao ambaye ndiye mwenye kuleta cha kufanya yaani “AJIRA”. Huyo mtu mwenye kuleta cha kufanya kimsingi ndiye mwenye “KAZI”.
   
    Habari njema ni kwamba mtu yeyote mwenye akili timamu anao uwezo wake wa asili wa kuweza kuleta cha kufanya. Kwasasa, mifumo mingi ya kiutawala ni kama haiwajui watu wanaoleta cha kufanya kwenye jamii. Ndiyo maana leo hii, tunajikuta tunaishi kwenye Dunia ambayo inathamini na kujali sana AJIRA kuliko KAZI.

    Ukichunguza kwa makini taasisi, idara, sheria, kanuni na taratibu nyingi utaona kuwa takribani asilimia 90% zimewekwa ili kushughulikia suala la AJIRA na siyo KAZI. Matokeo yake, kazi zinakuwa ni chache sana kiasi cha kutengeneza bomu la wanaotafuta ajira, ambalo linaweza kulipuka kama halitateguliwa. Ukweli ni kwamba ajira siku zote inapatikana ndani ya kazi na siyo kinyume chake.


    KAZI ilianza pale tu binadamu alipojitambua. Ikumbukwe kuwa binadamu alianza kazi ya uwindaji, uchimbaji mizizi na kuokota matunda porini. Tukiangalia mfano huu wa “kazi ya uwindaji”, utaona kwamba mwindaji alitakiwa kukamilisha shughuli fulani kabla na baada ya kuwinda. Shughuli za kabla ya kuwinda ilikuwa ni kutengeneza zana kama vile mkuki, upinde, visu, mitego n.k. na baada ya kuwinda ilibidi kufanya shughuli kama kuchuna ngozi, kukatakata nyama, kubanika, kusomba na kupeleka nyumbani. Hapa utaona kuwa shughuli zote hizi ilikuwa ni vigumu kufanywa na mtu mmoja, hivyobasi ilibidi mtu huyo kuwaomba majirani au ndugu kuja kumsaidia shughuli fulani fulani. Hawa watu walioitwa kusaidia, ilibidi nao kuwapa kiasi fulani cha nyama – na hii ndiyo tunaweza kusema kwa siku hizi ni PESA.

    Mfano mwingine ni “kazi ya kilimo cha mahindi”. Kwenye kazi hii kuna shughuli mbalimbali kama vile kuandaa shamba, kulima, kupanda, kupalilia, kuweka mbolea, kuzuia wadudu na magonjwa, kuvuna, kufungasha, kuhifadhi, kuuza n.k. Hizi zote ni shughuli ndani ya mchakato wa kulima mahindi. 

    Ili kufanya shughuli hizo kunahitajika ujuzi tofauti kutoka kwa watu tofauti. Kama mwenye kazi utatakiwa kuwaajiri watu wenye ujuzi tofauti tofauti kwa makubaliano ya kulipwa pindi watakapokamilisha shughuli hizo. Hapa wao watasema wamepata “AJIRA”.

    Mifano yote miwili inadhihirisha kuwa kazi ndiyo machimbo halisi ya ajira zote duniani. Maana yake, ndani ya “KAZI” ndipo kuna shughuli za kufanya. Katika dunia ya sasa, shughuli zilizopo kwenye kazi ndizo uzaa kitu kinachoitwa “AJIRA”.


    Watu wengi wakipata ajira wanabweteka kwa kudhani wamepata kazi. Ni bora kubweteka ukiwa umepata kazi kuliko kubweteka ukiwa na ajira. Kwani, kazi ndiyo uzaa ajira lakini, ajira haiwezi kuzaa kazi. Mara zote, kazi inakuwa ni mchakato unaolenga kupata matokeo yenye thamani fulani kwa watu.

    Kiuchumi tunasema lengo la kazi ni kuzalisha bidhaa au huduma. Kitu ajira mara nyingi kinatokea pale tu mwenye kazi anapotaka kuzalisha bidhaa/huduma nyingi kwaajiri ya watu wengine. Uwepo wa shughuli za kufanya ndio unamlazimu mwenye kazi atafute watu wa kufanya shughuli maalumu, ili kufikia lengo la mwenye kazi. Watu hawa watakaohitajika kusaidia kufanya baadhi ya shughuli zilizopo ndani ya kazi, ndio hao tunasema wamepata “AJIRA.”

    Unapopata ajira unapewa mwongozo na maelekezo maalum ya jinsi ya kufanya shughuli ulizopewa. Anayekupa mwongozo na maelekezo ni mwenye kazi kwasababu yeye ndiye anayejua undani wa zile shughuli na malengo yake.

    Lazima kwa aliyepata ajira kufuata maelekezo aliyopewa. Wakati mwingine unaweza usiruhusiwe kufanya namna wewe unavyojua, inakubidi ufuate ulichoambiwa na ukikifanya vizuri ndiyo unastahili kulipwa mwisho wa mwezi.

    Ikionekana baadhi ya shughuli hazijakamilika basi ujue kuwa unawezakuondolewa na akaletwa mwingine. Mwenye kazi ndiye anayeainisha shughuli za kufanya kwenye kazi yake ili iwe rahisi kubadilishabadilisha watu kama vipuli.

    Unapoajiriwa kufanya shughuli mojawapo ndani ya kazi, unatakiwa kufahamu kwamba kukamilika kwa shughuli yako pekee hakuwezi kuleta matokeo yaliyokusudiwa na mwenye kazi.

    Hii ni kutokana na ukweli kwamba, ili kazi ikamilike inategemea kufanyika kwa shughuli zaidi ya moja ikiwemo hiyo unayofanya wewe na shughuli nyingine zinafanywa na watu wengine.

    Kwahiyo, “Ajira” ni kufanya shughuli maalum ambazo zipo ndani ya kazi lakini, ambazo kila moja ikisimama peke yake haiwezi kuleta matokeo yaliyokusudiwa na mwenye kazi. Kwa kawaida, unaweza kuchomolewa kwenye hiyo nafasi na akaletwa mtu mwingine akafanya kile ulichokuwa unafanya na kazi ikakamilika.

    Mifano ya “kazi ya uwindaji na Kilimo cha mahindi” inatufundisha kwamba “huwezi kufukuzwa kazi lakini unaweza kufukuzwa ajira”. Kwahiyo, kama tunataka kutatua tatizo la ajira lazima tujikite katika mazingira ambayo watu wanaweza kutengeneza kazi ambazo kwa vyoyote vile lazima zitazalisha ajira.

    Katika zama hizi, “KAZI” ndiyo mgodi halisi ambapo unaweza kuchimba ajira nyingi na hivyo kuweza kuondoa tatizo sugu la ajira. Lazima tukubaliane kwamba chimbuko la ajira endelevu ni uwepo wa kazi ambazo mara nyingi zinabuniwa, zinaibuliwa na kutekelezwa na watu binafsi.

    Kazi zitatengenezwa kwa wingi iwapo tutapata mifumo ya utawala, uchumi na biashara itakayoweza kulinda mali ya mtu binafsi yaani “mwenye kazi”. Kutengeneza kazi kunahitaji mazingira ambayo watu watatumia vipaji vyao kutengeneza kazi na masoko. Uwepo wa bidhaa an huduma tofauti, uzalishaji kwa tija ndiyo vitapanua masoko. Mwisho wa siku tutapata fursa nying za ajira.

    Watu binafsi wajue kwamba bado wanaouwezo wa kutengeneza kazi. Na ni muhimu kutambua kwamba hakuna anayeweza kukunyanganya uwezo wa kutengeneza kazi. Kinachotakiwa ni kwamba kama tayari uko kwenye ajira basi jitahidi kutumia nafasi hiyo kupata maarifa ya kubuni na kutengeneza kazi. Uzuri wa kazi ni kwamba haina kustaafu japo ajira lazima usitaafu lakini pia ina uwezo wa kuzaa kazi nyingine.

    Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno NITUMIE MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO.

NAKUTAKIA MEI MOSI NJEMA!

No comments: