Wednesday, May 26, 2021

Kazi ya Kuzalisha Mali ni ya Nani?

 

“Kuajiriwa na kujiajiri yote ni AJIRA siyo KAZI” ~ CYPRIDION MUSHONGI

Kazi mojawapo ambayo tumekuja duniani kuifanya ni kuzalisha mali. Hii ni kazi muhimu sana ambayo inatakiwa kufanywa na kila mtu aliyefikia umri wa kujitegemea. Jambo la ajabu ni kwamba kazi hii wengi wanaikwepa, hasa wale tuliokaa darasani miaka mingi. Sababu za kukwepa jukumu hili ziko nyingi; moja ni.. kwamba wengi tunaamini kupata ajira ni kazi kama ilivyo kazi ya kuzalisha mali. Ajira ni kitu chenye ukomo na huwezi kuirithisha kwa mtu mwingine kama mwanafamilia.

Pia, tunadhani kuna watu maalum wanaotakiwa Kuzalisha mali na siyo sisi. Vyovyote utakavyofikiria ni sahihi kwako binafsi japo hilo halitabadili ukweli.

Kiuchumi tunasema lengo la kazi ni kuzalisha thamani, ambayo mara nyingi huwa katika sura na umbo la bidhaa au huduma.

SOMA; LEO NI SIKU YA WAFANYAKAZI AU WENYE KAZI

Kazi ya kuzalisha mali ni mchakato unaolenga matokeo fulani kama inavyokusudiwa na mwenye kazi. Mtu anapoamua kuzalisha bidhaa au huduma kwaajili ya watu wengi zaidi, ni wazi kwamba anaibua shughuli nyingi za kufanya.

Uwepo wa shughuli hizo, ndio kunampa fursa mwenyekazi kuwa na hitaji la watu wengine wa kusaidia shughuli mbalimbali zilizopo. Watu hawa wanaotafutwa kufanya shughuli kwa maelekezo ya mwenye kazi ndio tunasema wamepata “Ajira”.

Wapo wanaodhani kupata ajira ni sawa na kuzalisha mali; ukweli ni kwamba kama muda mwingi uko kwenye ajira, ujue wewe bado hujaanza rasimi “kuzalisha mali”.

Mababu zetu huko nyuma walitambua kuwa unapofikisha umri wa kuoa au kuolewa kazi yako ni moja tu! Ya “Kuzalisha mali”. Wao hawakuwa na utamaduni wa kumlalamikia mtu kwasababu suala la kuzalisha mali lilikuwa linajulikana kuwa ni la kila mmoja.

Kupitia mchakato wa kuzalisha mali watu waliweza kubuni kazi mbalimbali kulingana na kipaji kila mmoja alichojaliwa kuwa nacho. Kuna walioamua kubobea kwenye kazi ya kufua vyuma ili kutengeneza silaha za jadi, zana za kilimo na uwindaji n.k; wengine walijishughulisha na kilimo, uwindaji, utengenezaji wa kazi za sanaa, uganga wa jadi n.k. hatimaye kila mmoja aliweza kubobea katika eneo la kipaji chake. Kwa kufanya hivyo waliweza kujenga utoshelevu wa uchumi katika jamii yao.

Hivi sasa watu wengi wana uelewa finyu sana kuhusu chanzo hasa cha ajira hizi zinazotafutwa kama dhahabu. Uelewa huu finyu pengine unatokana na athari za mfumo wa elimu rasimi tunayopata kutoka shuleni na vyuo mbalimbali.

Hivi sasa, hakuna anayekumbuka sawa sawa kwamba kazi ya uzalishaji mali ndiyo msingi wa maendeleo ya jamii yoyote ile na ndiyo machimbo endelevu ya ajira. Kwasababu hiyo basi, wengi wanaona kuwa kupata elimu rasimi ndio mbadala wa kazi ya “kuzalisha mali”, hii siyo sawa!

SOMA; KAZI inaleta AJIRA na AJIRA inamaliza KAZI ni kweli?

Nimesikia mara nyingi watu wa Bukoba wakisema kwa lugha ya yao kwamba “tinakushoma nkashuba kulima” kwa tafsiri isiyo rasimi wanamaanisha kwamba “siwezi kusoma halafu nikalima”.

Maana yake wanaamini kwamba lengo la elimu rasimi ni kwaajili ya ajira hasa ofisini na siyo kuzalisha mali. Ninaamini kuwa mtazamo huu juu ya elimu rasimi siyo tu kwa watu wa Bukoba bali ni nchi nzima. Pamoja na mambo mengine, mtizamo wa namna hii ndiyo unapelekea kuwepo kwa tatizo sugu la ukosefu wa ajira.

Mkoa wa Kagera ni miongoni mwa mikoa michache yenye hazina ya wasomi wengi, lakini takwimu za hivi karibuni zinaonyesha uko kwenye orodha ya mikoa maskini sana.

Lakini uwepo wa wasomi wengi inaonekana hauna uhusiano na ukuaji wa uchumi kwasababu wasomi wengi licha ya kwamba wanaishi nje ya mkoa wao hawafanyi kazi ya kuzalisha mali na kama wanafanya basi kazi zao ni zile zinazotoa ajira chache sana kwa watu wengine.

Kauli maarufu huku Kagera ni “mrithishe mtoto wako elimu”, kwamba baada ya hapo atapata ajira – hii ni ahadi hewa. Ahadi hii inaanza kutolewa kwa mtoto akiwa bado mdogo hadi anapokuwa mtu mzima. Ahadi hii ya ajira ilikwisha zama ndani ya akili, kiasi kwamba msomi kama msomi hafikirii tena kutumia kisomo chake katika kufanya kazi ya kuzalisha mali.

Watu wanapokosa ajira, utasikia wakisema “mimi nakwenda shule ili niweze kujiajiri. Hii inaonyesha kuwa sauti ya ajira ndiyo bado inatawala nafsi zetu. Kwanini hatusikii watu wakisema “nina kwenda shule ili nifanye kazi ya kuzalisha mali vizuri?”.

Mtu aliyejiajiri anafanana sana na yule aliyeajiriwa kwasababu yote ni AJIRA siyo KAZI ya kuzalisha mali. Wewe unachotakiwa kujua ni jambo moja tu! “Kuzalisha mali” siyo kuajiriwa wala kujiajiri. 

Katika mchakato wa kuzalisha mali tunapata vitu viwili muhimu kwa maisha ya binadamu ambavyo ni “Ajira” na “Utajiri”. Kwahiyo, ili tuweze kupiga hatua kimaendeleo lazima kuwekeza zaidi kwenye kuzalisha mali na siyo kutafutia watu ajira.

Wewe uliye tayari kufanyakazi ya kuzalisha mali, “nenda mapema darasani na uwahi kutoka kwasababu kazi ya kuzalisha mali inakusubili”.

Unapoanza kazi ya kuzalisha mali usifanye peke yako; inabidi utafute watu wengine wa kukusaidia kufanya shughuli mbalimbali zilizo ndani ya mchakato mzima wa Kuzalisha mali.

Tukipata watu wengi kama wewe ambao watakuwa na kazi za kuzalisha mali kwenye jamii yetu ndipo tutapata uwezo na uhakika wa kuzalisha ajira kwa wingi.

Kumbuka kuwa suala la kuzalisha mali ni la mtu binafsi na hakuna anayejali wewe kuwa na mali.

Huu ni wakati wetu wote hasa tuliokaa sana darasani kuwa na ilani binafsi ya kuzalisha mali. Kwasababu suala la kuzalisha na hatimaye kuwa na mali binafsi halimo kwenye ilani za wanasiasa. Ukichunguza ilani za wanasiasa utaona kuwa kinachozungumziwa sana ni ajira siyo wewe kuwa na mali.

Sasa hali hii ndiyo itupe picha ya kwamba suala la kuzalisha au kutafuta mali halizungumzwi sana japokuwa ndilo suala muhimu katika kuleta suruhu ya matatizo ya ajira. Kama halizungumzwi sana maana yake halifanyiwi kazi ipasavyo, kwahiyo wewe binafsi ndiyo unatakiwa kulizungumza na kulifanyia kazi.

Tukitafakari, tukalijua hili na kulifanyia kazi vizuri nina uhakika hata wazungu tutaweza kuwapatia ajira, kwani hata wao ni kama sisi, linapofika kwenye suala la AJIRA na KAZI ya kuzalisha mali.

Wewe unayesoma Makala hii, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno NITUMIE MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO.

No comments: