“Siku Rahisi Kuishi bila Ujanja Zimeisha” ~ Cypridion Mushongi
Hapa kwetu Tanzania neno “Ujanja” mara nyingi linatafsiriwa Zaidi kuwa ni ulaghai, uhuni au udanganyifu. Ni kawaida sana kusikia mtu akimsema mwenzake kuwa “yule bwana ni mjanja mjanja” usimuamini!
Watu wengi hawapendi kuitwa wajanja; eti kwasababu itaonekana kwamba wao siyo waaminifu machoni mwa umma.
Kwa taarifa yako “Ujanja” ni..uwezo wa akili katika kutambua, kubaini au kuelewa mambo kwa haraka. Hapa, akili ninamaanisha uwezo wa kupata na kutumia maarifa na ujuzi katika mchakato mzima wa kuendesha maisha yako.
Kwa maneno mengine “mjanja” ni mtu mwerevu wa mambo na kwa mantiki hiyo “ujanja” ni kitu kinachoweza kukuzwa au kuendelezwa na muhusika.
Ujanja ni kuchunguza au kujua mambo: Ujio wa teknoljia ya habari na mawasiliano umeleta kundi la “wajanja” (wanaojua) na wasijua.
Wajanja ni wale wenye uelewa wa mambo na wenye kupata taarifa sahihi na “wasiojua” ni wale ambao hawajui ukweli wa mambo yanayoendelea na hawana taarifa juu ya nini kinaendelea duniani.
Ubunifu katika teknolojia ya habari na mawasiliano imewezesha “wajanja” kuchunguza mambo na kuchukua hatua kwa njia ya ufahamu zaidi kuliko siku za nyuma ambapo hisia za kawaida pamoja na Imani/kuamini ziliongoza kila hatua tuliyochukua, ikiwemo matendo yetu.
Leo, njia sahihi ya maisha ni kuwa “mjanja” ambapo unatakiwa "kuamini lakini thibitisha". Hii inamaanisha tunapaswa kuwaamini wale tunaofanyakazi nao lakini lazima kuthibitisha, kwamba maamuzi na matendo yao yanaendana na yale maslahi au manufaa tunayotarajia kutoka pande zote mbili.
Kwasababu ya upatikanaji wa taarifa, hata taaluma zinazoogopwa kama vile ya afya na tiba bado wagonjwa hasa kundi la “wajanja” wanafanya uchambuzi muhimu juu ya afya zao.
Madaktari wa matibabu leo, wanajua kwamba wagonjwa wanapokuja kliniki kwaajili ya kucheki afya zao, tayari wanakuwa wamejitambua kwa kusoma taarifa mbalimbali.
Taarifa hizi zinazopatikana kwa wingi kwenye tovuti za taasisi zinazotambulika na vitabu vya matibabu vya kujisaidia vilivyochapishwa na vyama vya matibabu vinavyotambulika.
Kwasababu ya taarifa hizi, baadhi ya wagonjwa wanaokuja kwenye zahanati na hospitali, tayari wamesoma makala nyingi na wana maoni juu ya shida zao za kiafya na matibabu yanayowezekana.
Hapa namaanisha kwamba kuna maarifa mengi na taarifa nyingi za kujisaidia katika zama hizi zinazotuwezesha kupata ufahamu mzuri na kupunguza hatari zaidi kuliko ilivyokuwa miaka mingi iliyopita.
Ujanja ni kudadisi: Mtu mdadisi daima huuliza maswali na kutafuta majibu sahihi. Majibu humsaidia kuona ulimwengu mpya wenye fursa ambao kwa kawaida hauonekani.
Kuuliza maswali kunakufanya kuelewa na kutambua mawazo mapya. Unapokuwa mdadisi wa kutaka kujua jambo ambalo akili yako inatazamia na kutarajia mawazo mapya kuhusiana na jambo hilo basi wazo likija utalitambua.
Bila udadisi fursa zikitokea bado utazikosa kwasababu akili yako haijajiandaa kuzitambua.
Hebu fikiria ni mawazo mangapi yamepotea kwa kukosa udadisi?
Kwahiyo, usiwe mtu wa kuchukulia mambo jinsi yanavyoonekana usoni; inakupasa kufikiri kwa undani na jaribu kuchunguza kila kitu kinachokuzunguka.
Njia pekee ya kupata undani wa mambo ni kuuliza maswali ya ufahamu. Unatakiwa kuuliza maswali kama haya: “ni nini?, kwanini?, lini?, nani?, wapi na vipi?”.
Kwa mfano kuhusu changamoto ya ukosefu wa ajira nchini, kama ningekuwa “mjanja” ningedadisi kwa kuuliza maswali kama haya; Je, ajira ni nini hasa? Je, kuna uhusiano gani kati ya serikali na ajira? Tofauti ya kazi na ajira ni ipi? Je, wanaonipa ajira wao wanatoa wapi? na nani aliwapa hizo ajira? Je, katika uhalisia ni nani mwenye jukumu la kunipa ajira?
Kwakuwa “Ujanja” ni kitu kinachoweka kukuzwa na kuendelezwa, itoshe kusema kwamba anza mwaka huu mpya wa 2023, safari yako ya kukuza na kuongeza kiwango cha udadisi.
Fungua akili yako ili iweze kupokea maarifa na ujuzi mpya.
Jitahidi kuwa mjanja katika maeneo ya kujenga mahusiano, mikakati, kazi, kutengeneza pesa, kutengeneza marafiki, uwekezaji, biashara, siasa, sera za uchumi n.k.
Tumia mtandao wa MAARIFASHOP kukuza ujanja maana wajanja bado ni wachache!
Kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno; NITUMIE MAKALA kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza hapa: MAFUNZO.
No comments:
Post a Comment