Sunday, January 8, 2023

Mpenzi wa Kutiwa Moyo Kuna Ujumbe Wako wa Mwaka Mpya



"Roho ya kujitegemea ni kinga dhidi ya wakatisha tamaa" ~ Cypridion Mushongi



Wakati huu tunapoanza mwaka mpya wa 2023, tukumbuke kuwa dunia ya sasa ina watu wengi wanaotukatisha tamaa kuliko wanaotutia moyo. Yawezekana wewe ni..mmoja wa wale watu wasiopenda kusikia maneno haya. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, binadamu tulio wengi tunapenda sana kutiwa moyo kwa kila jambo tulifanyalo maishani.

Kitu cha ajabu ni kwamba watu wengine wanataka kutiwa moyo hata kwa kitu chenye maslahi yao binafsi.

Kupenda kutiwa moyo ni jambo zuri, lakini ukumbuke kuwa siyo lazima na siyo wajibu wa watu wengine kukutia moyo.

Watu wengi hawataona umuhimu wa kukutia moyo, na kinyume chake wengi watakukatisha tamaa. Sisi binadamu tumezaliwa na "roho ya kujitegemea", hivyo basi usiogope wakatisha tamaa, kwani tayari dawa yao unayo ndani yako.

Hii "roho ya kujitegemea" ndiyo inatuwezesha kufanya yale yote tufanyayo kwa ukamilifu, hata kama hakuna mtu wa kututia moyo.

Hapo zamani (miaka ya 1960 kurudi nyuma), mababu zetu walikuwa na roho ya kujitegemea, enzi hizo "babu zetu hawakusubili kuambiwa cha kufanya, hawakusubili mtu fulani afikiri, atende au aongee kwa niaba yao".

Wao waliangalia matatizo na changamoto walizokuwanazo na walianza kuzikabili mara moja.

Kwa kufanya hivyo walijikuta wakifanya mambo makubwa ya kuwaendeleza wao binafsi na jamii zao. Hata hapa tulipo, tumesimama walipoishia, kwani katika zama zetu hizi, hatujafanya kitu kikubwa kuzidi wao.

Hatahivyo, hivi sasa, "roho ya kujitegemea" imebaki kwa watu wachache sana. Kwa walio wengi nafasi ya "roho ya kujitegemea" imechukuliwa na "roho ya utegemezi".

Watu wenye roho ya utegemezi, wanadhani ni lazima watu wengine wawatie moyo au kuwapongeza kila wanapofanya kitu fulani. Hilo lisipotokea, ni wepesi sana wa kukata tamaa.

Ukweli ni kwamba, ukiwa na kiwango kikubwa cha "roho ya utegemezi", mara nyingi unakuwa ni mtu unayependa sana kupongezwa au kutiwa moyo kwa kile unachokifanya.

Roho ya utegemezi inasababisha kukosekana kwa ubunifu kwa kila kitu tunachofanya. Matokeo yake, miradi mingi ya kutuingizia kipato siyo endelevu na inafanana sana, jambo ambalo limezidi kusababisha umaskini na ukosefu wa ajira.

Pia, miradi mingi isiyo na ubunifu ndani yake hailipi, richa ya kwamba wateja wengi kwasasa wanakabiliwa na uhaba wa bidhaa na huduma zenye kukidhi mahitaji yao halisi.

Habari mbaya kwa mwaka mpya huu (2023) ni kwamba tutashuhudia kuongezeka kwa idadi ya watu wenye "roho ya utegemezi".

Kwahiyo, ni muhimu sana kwako wewe pamoja na kufanya mambo mengine mwaka huu, ni lazima tujikite kwanza kufanya kazi ya kurudisha ile roho ya asili (roho ya kujitegemea). Kazi hii iambatane na zoezi la kuiwasha upya roho ya kujitegemea.

Kuwasha upya roho yako ya asili roho ya kujitegemea ndiyo dawa ya kuaminika katika kukabiliana na wakatisha tamaa yaani (wasiokutia moyo). Wakatisha tamaa wanachangia sana kuzima moto wa roho ya kujitegemea.

Hivyo basi, kuwasha upya kwa roho yako ya kujitegemea ndiko kutakukwamua kutoka kwenye kundi kubwa la wakatisha tamaa au wenye "roho ya utegemezi".

Mwaka mpya huu wa 2023, hakikisha "roho ya kujitegemea" inawaka muda wote yaani masaa 24 siku saba za wiki (24/7). Pia, jaribu kuhakikisha mwaka huu huwe ni wa kuziba masikio, ili kupunguza kiwango cha mitetemo ya kukatisha tamaa.

Unayesoma makala hii, hapa MAARIFASHOP endelea kuutumia vizuri mtandao huu katika kujifunza mambo mbalimbali yatakayo kuwezesha kupata mafanikio unayoyataka. 

Kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno; NITUMIE MAKALA kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO.

No comments: