Tuesday, May 12, 2015

Usibane Matumizi ya Kipato Tumia Kipato Kupanua Njia za Kuingiza Kipato




Yawezekana unaendelea kuishi maisha duni, kwasababu unaishi kwa “kubana matumizi”; na hii ni kutokana na ukweli kwamba, tangu tukiwa wadogo tumefundishwa na wazazi, ndugu jamaa na marafiki kuwa ili uweze kuwa salama ni “Ishi Chini ya Uwezo Wako”. Watu wengi wenye mtazamo huu, mara nyingi wanaotumia njia ya kubana matumizi kuwa ndiyo suluhisho na njia pekee ya kukabiliana na ugumu wa  wa maisha. Ukweli ni kwamba, kubana matumizi ni utaratibu mzuri lakini inategemea una malengo gani ya kufanya hivyo. Kutokana na kutotambua ubaya wa tabia ya kubana matumizi, wengi wamelichukulia kuwa ni utaratibu wa kudumu badala ya kuwa wa muda tu!. 

Watu wameendelea kubana matumizi tangu wanajitabua mpaka wanazeeka. Unapokuwa mtu wa “kubana matumizi” muda wote, kinachojitokeza ni kwamba unajenga hofu kubwa ndani yako juu ya kuishiwa pesa kidogo uliyonayo. Akiri yako yote inaelekezwa kulinda pesa yako isitoke au wengine wanasema eti! Itoke kwa mpangilio – lakini mwisho wa yote hali inabakia palepale “kuishiwa na kutaabika”. Kwa mtu ambaye amejiwekea utaratibu wa kudumu wa kubana matumizi, akiri yake inadumaa sana kiasi cha kukubali kuishi maisha duni na ufukara. Mtu wa namna hii kila anapotafuta na kupata, badala ya kuwaza ni kwa namna gani atapata kingi zaidi, yeye mara moja unawazia kuishiwa, ndiyo maana anaanza kuweka nguvu nyingi kubana hicho kidogo kilichopatikana. Mwisho anatumia kwa kujinyima sana na hatimaye kinaisha ndipo huyo mtu uhanza tena kutafuta. Kwahiyo, unajikuta umenasa katika mzunguko wa kuishiwa na maisha yanakuwa ni ya kubangaiza miaka yote. 

Kuishi chini ya uwezo wako ni kitu cha kawaida na mara nyingi ushauri utolewa sana na wataalam na wasomi wa masuala ya biashara na uchumi kuwa njia pekee ya kuendana na hali ni kufanya vitu vilivyo chini ya au vinanavyolingana na uwezo wako. Lakini badala ya kulikubali hili bila kulitafakali ngoja tujiulize ni kwanini wanasema hivi? Au kwanini imani hii ya kubana matumizi inatokea? chimbuko la kubana matumizi ni kuazia wakati ule wa zama za kale ambapo binadamu aliishi kwa kukusanya matunda na kuwinda wanyama. Wakati huo, watu hawakuwa na fikra za uzalishaji, kwasababu walizoea kula vitu ambavyo vilijiotea na kukua vyenyewe bila kutegemea akiri na nguvu ya binadamu. 

Kazi ya binadamu wakati huo ilikuwa ni kutafuta na pale vilipopatikana vilikusanywa kiasi cha kutosha. Baada ya kuvikusanya, binadamu huyo wa kale alijitahidi sana kuvitunza ili vikae muda mrefu bila kuisha. Kwakuwa vitu hivi mara nyingi vilikuwa vinatoka mbali sana na makazi yao, ilibidi kujitahidi kubana ili kupunguza safari za kwenda huko; njiani walipambana na wanyama wakali, mafuriko, mvua n.k. kwahiyo kila walikuwa wakifkiria safari ilikuwa ni budi wabane kupunguza hadha za namna hiyo. Sasa wewe unayeishi katika zama hizi za leo, tayari una uwezo wa kuzalisha bidhaa na huduma mbalimbali, na hivyo kutotarajiwa kuishi kwa style kama ya enzi za kale. Uhamuzi ni wako kwa maana kwamba unaweza kuamua kuzalisha vingi na ukatumia kiasi unachoona kinafaa kukutoshereza mahitaj yako ya wakati huo. Badala ya kila wakati kufikiria kubana matumizi na mwisho kuishia kuishi katika maisha ya kupata mahitaji chini ya kiwango chako halisi. 

Kuishi chini ya uwezo wako ni sawa a kujiaminisha kuwa suluhisho la kumudu gharama za maisha ni kupunguza matumizi. Kuishi juu ya uwezo wako ni sawa na kujiaminisha kuwa pesa ipo nyingi. Hali zote mbili hazifai, bali suluhisho pekee ni kupanua na kuongeza vyanzo vya mapato. Kila mmoja anaweza kupunguza matumizi, na kila mmoja anaweza kutumaini na kuomba Mungu kuwa pesa itakuja, lakini inahitaji ubunifu, maarifa na uelewa, pamoja na ujasiri ili kukuza na kupanua mapato yako kupitia njia halali. Kimsingi siamini katika kuishi chini ya uwezo na wala kuishi juu ya uwezo, ninachoamini ni kuishi kwa kupanua na kuongeza njia za kuleta mapato. 

Siamini katika mtazamo wa “ishi chini ya uwezo wako”; kwa ujumla mtazamo huu ni wa kimaskini na siyo mzuri. Lakini pia, kibaya zaidi ni kwamba ushauri huu wa kuishi chini ya uwezo unasababisha kuua kabisa dhamira na fikra za ujasiriamali. Ushauri huu unakufanya usinyae kuwa mdogo. Hali hii inafanya mtu anakuwa na maisha duni kuliko alivyopaswa kuwa. Hali hii pia inakufanya kuingia katika kundi la watu wa kawaida au wenye mawazo ya wastani (mediocre). Na kama uliwahi kuambiwa na wewe mwenyewe kuwazia kwamba unatakiwa kuishi chini ya uwezo wako acha mara moja. Huu ni wakati wa kukua na kufanya mambo makubwa, ni wakati wa kuwekeza asilimia kubwa ya kipato chako kwenye vitu vinavyoingiza pesa kwako; ni wakati wa kuwa mbunifu na kupanua siyo tu njia za kuingiza kipato, bali pia jitanue kwa kuilisha akili yako ili uweze kufaidika na fursa zilizokuzunguka.

Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO

No comments: