Sunday, May 31, 2015

Bila Picha Mpya Hakuna Jipya



·        Watu wengi wanafikiri kwa kutumia vitu vilivyopo tu!
·        Picha ya maisha mazuri haipo kwenye akili ya walio wengi!

Maendeleo yaliyopo kwa sasa yametokana na mawazo pamoja na picha mbalimbali zilizojengeka ndani ya ubongo wa binadamu. Vitu vyote tunaviona ambavyo vimetengenezwa na binadamu, vilitokana na mawazo na taswira/picha zilizoumbwa ndani ya ubongo wa mtu. Baada ya kuumba picha au taswira ya kile kinachohitajika kufanyika ndipo binadamu huweza kutumia nyenzo mbalimbali pamoja na malighafi nyinginezo kutengeneza vitu halisi, huku akiongozwa na ile taswira iliyoko kwenye akili ndani ya ubongo wake.

Nyumba ni mfano mmojawapo wa vitu halisi ambavyo huanza kama wazo. Leo hii tuna nyumba za kila aina, kwasababu mara nyingi tuna wasanifu majengo ambao kila mara uanza nyumba kwa kufikiria jinsi itakavyokuwa hata kama haijajengwa na baadae uchora ramani yake ambayo wajenzi uitumia katika kusimamisha jengo. Kwahiyo, aina mbalimbali za majumba tunazoziona leo zilitokana na fikra na ujenzi wa taswira ndani ya ubongo wa watu hao ambao ni wasanifu majengo (architect). Nyumba ikishakamilika ndipo watu wengine hupata fursa ya kujua kilichokuwa akilini mwa huyo mtu na pindi watoto wanapozaliwa na kukua ujenga mawazo na taswira ya kurithi kutokana na vitu vilivyopo tayari. Kwahiyo, mtoto akikua na kufikia wakati wa kujenga nyumba yake, moja kwa moja anapata picha ya nyumba kwenye ubongo wake ambayo ni ya kurithi kutoka kwenye nyumba zilizojengwa tayari. Kwa namna moja au nyingine ile picha iliyobuniwa kwenye ubongo wa mtu wa kwanza anakuwa ameinakiri kutoka nyumba halisi na kuijenga mara ya pili.

Katika nchi nyingi ikiwemo Tanzania, ambazo hazijapiga hatua kubwa kimaendeleo; vitu vingi vinavyofanyika vimetokana na taswira ya vitu halisi ambavyo tayari vipo na vinaonekana. Imejengeka tabia ya watu walio wengi kuhoji hasa pale mtu Fulani anapojaribu kuibua jambo jipya, mara nyingi linakataliwa eti! Kwa kisingizio cha kwamba “halijawahi kufanyika popote”. Kwahiyo, watu wanajisikia amani zaidi wanapoona wanafanya kitu ambacho tayari kinafanyika kwingine. Hali ya namna hii ndiyo inaendelea kutufanya tuendelee kuwa wategemezi na ombaoma mbele ya jamii ya kimataifa. Utamaduni huu wa kuendelea kutumia uzoefu na kuzama kwenye vitu vilivyoko mbele yetu muda wote (hali halisi), ndio unaotusababishia kuendelea kupata changamoto, matatizo na uzoefu ule ule miaka nenda rudi!. Mara nyingi uzoefu na elimu juu ya jambo fulani, ni vitu ambavyo vimejengeka kutokana na mambo yaliyopita au vitu vya zamani, kiasi kwamba, wewe unachofanya ni kuvikariri na kuvitoa upya, hali ambayo kiukweli kunakuwa hakuna jipya lolote la kutokea.

Misuli ya kuwaza ndani ya ubongo wetu, ndiyo hubadilisha mawazo na fikra zetu kuwa vitu kamili. Picha na fikra juu ya kitu tukitakacho, ndivyo vitu muhimu vinavyohitajika katika kujenga maisha mazuri ya baadae. Ni kwakutumia picha iliyoumbika ndani ya ubongo wetu, ndipo tunaweza kuona jinsi tunavyotaka maisha yetu ya baadae yawe. Tukishakuwa tumeyaona maisha mazuri ndani ya ubongo wetu, ndipo tunaweza kupata hari na shauku kubwa ya kuyatafuta hayo maisha ya ndoto yetu. Kwahiyo, ni wakati muhafaka sasa kwa kila mtanzania kujenga tabia ya ubunifu na kuendelea kujikita katika kufikiri mambo mapya na vitu vingine nje ya hivi vilivyopo. Kila mtu aanze kwa kutengeneza picha ndani ya ubongo wake juu ya maisha mazuri anayoyatamani na baadae kuweka mikakati ikifuatiwa na utekelezaji. Iwapo tutaweza kupata picha ya maisha tuyatakayo na jinsi tunavyopenda yawe, basi nguvu kubwa itakuwa imewekwa kwenye mwendo na mabadiliko makubwa  yakiambatana na maisha mazuri yatatokea bila pingamizi lolote. Kumbuka kuwa asilimia 80% ya mafanikio yako yataletwa na wewe mwenyewe na asilimia 20%  ndiyo inategemea watu wengine.

Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO

Kazi ni kwako! Timiza wajibu wako!

No comments: