Sunday, May 17, 2015

Watu Hawajui Kitu Wanachohitaji Kama Hawajakiona Ongeza Kasi ya Ubunifu Soko Lipo

Mara zote tunapenda kuhitaji bidhaa ambazo tayari tumeziona zipo au tumezizoea. Utafiti umebaini kuwa mahitaji ya binadamu huwa hayana kikomo, kiasi kwamba kila mara anhitaji ama kitu kipya au kile alichokizoea. Ukweli ni kwamba, bado maisha yetu ni magumu kwasababu bado tunatumia nguvu nyingi kufanikisha mambo mbalimbali yanayohitajika katika maisha yetu kwa ujumla. Ugumu wa maisha unatokana na kiwango kidogo sana cha ubunifu na uzalishaji wa bidhaa. Hapa Tanzania, bado tunazidi kutegemea mbinu zile zile za zamani ambazo wazee wetu walizitumia wakati huo kupambana na maisha. Maana yake ni kwamba katika zama hizi hatujatoa jipya sana lenye kuendana na kasi ya mabadiliko yanayoendelea kutokea duniani kote.

Kwa sasa Tanzania, tuna mahitaji makubwa sana ya ubunifu na teknolojia katika nyanja mbalimbali za maisha. Yawezekana watu wengine wako tayari kulifanya hili lakini wanaogopa au wana hofu na mashaka juu ya kukosekana kwa soko la bidhaa mpya ambazo zitatokana na ubunifu au teknolojia mpya. Kamahiyo, kama hiyo ni mojawapo ya sababu, basi tunatakiwa kuondoa hofu na kuanza kufikiria “tutaipatia nini dunia”, yaani tuwe na mtazamo kama wa watu wa sanaa (craftsman mindset).  Watu katika fani ya sanaa ni mfano wa kuigwa, kwani wao huwa hawasubili watu wawambie nini wanataka, bali wao uchukua muda wao na kuwaza ni kitu gani kinaweza kuwafurahisha watu basi! na kweli kama ni mziki ukitoka, unaona kila mmoja anajaribu kusaka CD ili kununua.

Hapa Tanzania, katika kipindi cha miaka kumi iliyopita kuna vitu vimeibuliwa ambavyo havikuwepo huko nyuma. Lakini baada ya wabunifu mbalimbali kuvileta kwetu, tumejikuta tunavihitaji sana kiasi cha kwamba, kuna watu wengi ambao hawawezi kufanya mambo yao yakaenda sawasawa bila kutumia vitu hivyo. Mifano ni mingi sana, lakini tuangalie michache tu kama ya usafiri wa pikipiki, chakula cha ndizi na matumizi ya simu za mkononi

Usafiri wa pikipiki: Huduma ambayo haikuwepo huko nyuma hii ya usafiri wa pikipiki maarufu kama “BODA BODA”. Ebu jiulize kabla ya ujio wa usafiri huu, watu walikuwa wanatumia nini kusafiri? Najua utasema magari, lakini walio wengi, magari yalikuwa hayawezi kufika majumbani kwao. Kwa wale wanaofanya kazi hasa sehemu za starehe, wanalazimika kutoka kazini wakati wa usiku wa manane, usafiri huu wa pikipiki umekuwa mkombozi kwao. Kumbe kwa muda wote ambao hakukuwepo na usafiri wa pikipiki, watu waliendelea na maisha kama kawaida na kwa wakati huo hakuna  aliyewahi kufikiria juu ya mahitaji makubwa ya usafiri huu. Kwa maana nyingine ni kwamba, tangu zamani tulikuwa na mahitaji makubwa ya huduma hii, lakini hatukujua kabisa kama tulihitaji kitu hicho, mpaka kilivyoletwa na wabunifu wetu, ndio tukaanza kujisikia kuwa na mahitaji ya Usafiri wa pikipiki.

Chakula cha ndizi: Hapo zamani tulikuwa na makundi manne ya ndizi (kupika, mbivu, kuchoma/kukaanga na pombe). Aina ambazo zilikuwa kwenye kundi la ndizi za kuchoma na kukaanga, kwa hapa Bukoba zinafahamika kama “e’nkonjwa/gonja” na huko Karagwe ni “e’ngarambi”. Kutokana na matatizo mbalimbali, aina hii ya ndizi ilianza kupungua na hivyo kuadimika. Kutokana na kuadimika kwake, ndipo wajasiriamali hasa kutokea miji ya kanda ya ziwa,  walipoamua kujaribu kukaanga aina nyingine kutoka kundi la ndizi za kupika, lengo likiwa ni kuhakikisha wanawapatia wateja wao angalau ndizi wakati wanapo kula nyama choma. Baada ya watu kuonja aina nyingine ya ndizi hizi za kupika, walitokea kuzipenda pia na ndipo mahitaji ya ndizi za kupika yakaongezeka mara mbili yaani zikawa zinakaangwa na wakati huhuo zikawa zina pikwa. Hivyo, tunaona kwamba watu kwa sasa wanahitaji sana ndizi zilizokaangwa bila kujali ni aina ipi ya ndizi, japo wakipata ile ya aina ya “gonja” wanafurahi zaidi. Watoto waliozaliwa hivi karibuni na kukulia kanda ya ziwa hawatajua kuwa kulikuwa na aina fulani ya ndizi ambayo ni maalumu kwaajili ya kukaanga, bali watapokea kilichopo au kitakachokuja baadae na hicho ndicho watazidi kuhitaji.


Matumizi ya simu za mkononi: Tualiowengi hawakujua kama wanahitaji mawasiliano ili kuweza kufanya biashara na shughuli nyingine za kimaisha. Wale wagumu walianza kuwasema wenzao kwamba wanapoteza pesa kwa kupiga simu lakini kwakuwa simu tayari zilianza kuonekana kila mahali basi na wale waliofikiri kuwa hawazihitaji baadae waliona umuhimu wa simu. Baada ya watu wengi kumiliki simu za mkononi, sasa kuna aina mpya zijulikanazo kama “Smartphone” aina hizi za simu kwa Kagera zinajulikana kwa jina maarufu kama “tachi”. Tunaona kuwa kadiri siku zinavyokwenda watu wengi wanazidi kuona umuhimu wa simu za aina hii, kwasababu wale ambao hawajaamua kuwa nazo, wanaona wenzao wenye simu hizo wanavyofaidika na Huduma zipatikanazo kwenye simu za “Smartphone”. Mfano: wale wenye magari wanaweza kupiga picha spare na vipuli vya aina mbalimbali na kuvituma kwa wenye maduka ili kujua kama vinapatikana na ni bei gani, wengine wanaweza kupata taarifa kwa picha juu ya aina za nguo na mitindo mbalimbali n.k. Tokea huko nyuma hatukujua kama tulihitaji huduma za namna hii kwasababu tulikuwa hatujaziona, lakini baada ya kuona umuhimu wa matumizi ya simu, sasa tuna mahitaji makubwa sana.

Kwakuwa watu wanapenda kuona kitu kwanza alafu ndio wanahitaji, basi hali hii inatoa fursa ya kufanikiwa haraka kwa wale wote ambao wako tayari kufikiri, kubuni na kugundua vitu vipya, kwasababu, soko lipo la kutosha kwa wazalishaji wote. Kinachotakiwa ni kwamba kitu kipya ulicholeta kiwe na manufaa makubwa kwa watu waliowengi. Ni muhimu kwa wapenda mafanikio kukaa muda wote katika hali ya utafiti kwenye jamii. Kwakufanya hivyo, ndipo tutaweza kugundua mahitaji muhimu ambayo ni mapya. 


Ili kufanikisha hili, ni vyema tukajifunza jinsi ya kutumia macho ya ubongo kuona fursa badala ya kutumia macho ya kawaida kama tulivyozoea. Pia, tunahitaji kuwekeza muda mwingi kufikiri na kuchambua hali ya maisha yetu na tunatakiwa kuwa wadadisi kila mahali tunapokuwa, na hatimaye tuchukue hatua na kuanza kuzalisha bidhaa mpya na zenye manufaa makubwa kwa jamii. 

Wito kwa wajasiriamali; ni muhimu sana tuanze sasa kutumia muda mwingi tulionao kufikiri na kuongeza kasi ya ubunifu katika kila nyanja ya maisha. Likifanyika hili, tuna uhakika wa kupiga hatua kubwa sana kimaendeleo hasa ya kiuchumi na kijamii. Wito pia ni kwa wale wote waliokabidhiwa majukumu ya kuweka mazingira wezeshi kuendelea kulisimamia hili, kwani tunaanza kuona ongezeko la vijana ambao wako tayari kufikiri na kubuni vitu vipya ambavyo hatimaye vitarahisisha maisha na hivyo kuendelea kuifanya Tanzania kuwa mahali pazuri pa kuishi.

Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO

1 comment:

Unknown said...

This awesome Mr., its really educative