Sunday, July 19, 2015

Mafanikio Yako Yamejificha Ndani ya Thamani

Mafanikio Yako Yamejificha Ndani ya Thamani

    • Kadiri utakavyozidi kutengeneza thamani nyingi kwaajiri ya watu wengine, ndivyo utakavyozidi kupata pesa nyingi.

    • Kwa mtu ambaye ni mjasiriamali mahili, kitu thamani ni bora kuliko pesa!
    Siku watu wengi wakigundua kuwa thamani ndiyo pesa yenyewe wataanza kuthamini sana “thamani” kuliko “pesa”; na ndipo kila mmoja atawekeza juhudi na maarifa katika kusaka thamani kwaajiri ya jamii, kuliko hivi sasa ambapo watu wengi wanakesha wakitafuta pesa. Iwapo, watu watajihusisha zaidi na kusaka thamani badala ya pesa, ni wazi kwamba dunia itajaa bidhaa na huduma bora zenye kukidhi mahitaji yote ya binadamu (maisha bora), na dunia itakuwa ni mahali pazuri pa kuishi. 

    Je uliwahi kujiuliza hiki kitu kinachoitwa thamani ni nini hasa? Au na wewe unaendelea kukutana nalo kwenye maandishi au mazungumzo basi! Maana ni kawaida kusikia watu wengi wakiongea juu ya suala zima la kuongeza thamani. Unapowauliza watu juu ya maana yake, jibu la haraka haraka unaambiwa kwa kingereza, yaani “Value” ukiuliza tena maana ya “value” anaambiwa ni “thamani” mwisho inakuwa kama ule mchezo wa kuku na yai ni kipi kilitangulia!.

    Mara nyingi, neno “thamani” linapewa tafsiri na maana ya juu juu, kiasi cha kuwafanya watu kushindwa kupata picha halisi juu ya umuhimu, ukubwa na upekee wa “thamani” katika maisha. Kutokana na tafsiri ya juu juu sana, thamani kama kitu halisi, imekuwa haithaminiwi kama ilivyo pesa.  Sababu mojawapo za kutothamini thamani ni kutokana na ukweli kwamba, thamani ni kitu ambacho hakionekani kwa macho na hakishikiki mkononi, hali ambayo huwafanya watu wengi kushindwa kutambua kuwa, pesa zote halali walizonazo zinatokana na thamani. Kwa maneno mengine “thamani ndiyo kila kitu” ambacho binadamu utumia kumaliza kero na changamoto mbalimbali za kimaisha”. 

    Thamani ni kile kiwango cha umuhimu uliomo ndani ya bidhaa au huduma. Pia thamani ni ubora ambao huifanya bidhaa/huduma fulani kupendeka au kuhitajika. Kwa maneno mengine, thamani ni ule uhitaji, umuhimu, faida, urahisi ambao mara nyingi huwekwa kwenye bidhaa au huduma fulani fulani. Thamani ndani ya bidhaa au huduma ndiyo hasa huwafanya watu kutoa pesa yao waliyoitolea jasho kwa hiari, kwa lengo la kujipatia thamani ili kukidhi mahitaji. Kwahiyo, thamani ni matokeo ya kile akipatacho mtu baada ya kuwa ametumia bidhaa au huduma yako.


    Kwa mtu ambaye ni mjasiriamali mahili, kitu thamani ni bora kuliko pesa, kwasababu kiasi cha pesa ambacho mtu ukipata, lazima kilinganishwe na thamani iliyoko ndani ya bidhaa au huduma. Watu wengi waliofanikiwa wanaangalia zaidi thamani ya vitu walivyotengeneza, tofauti na kwetu hapa ambapo wengi wanaangalia pesa tu!. Mwazoni kabla ya kutengeneza bidhaa, thamani yake inakuwa bado iko kichwani mwa mjasiriamali. Kinachotakiwa ni wewe kuitoa ndani yako na kuiweka katika hali ile ambayo unaweza kuwapa au kuwasaidia watu wengine ili watimize matakwa na haja zao. 

    Kadiri utakavyozidi kutengeneza thamani kubwa kwaajiri ya watu wengine, ndivyo utakavyozidi kupata pesa nyingi. Na ukiona unapata pesa kidogo usianze kutafuta mchawi, bali jiulize maswali ya kwamba wewe umetoa thamani ya kiwango gani kwa watu wengine? Kwahiyo, wewe jikite katika kutoa thamani ya kiwango kikubwa kwa watu wengine. Thamani unayotengeneza na kuwapa watu wengine inawasaidia kukidhi mahitaji yao mbalimbali. Kwa mjasiriamali yeyote, ni muhimu kutambua kuwa kila unapofirkiria kutengeneza thamani yoyote ile, hakikisha hisiwe ni kwaajiri yako peke yako, bali iwe ni kwaajiri ya watu wengine. Endapo utatengeneza thamani inayokulenga wewe peke yako, basi ujue kuwa, hakuna atakayekuletea pesa yake, kwasababu thamani uliyonayo haimfai chochote mtu mwingine. 

    Watu wengi wanaendelea kuishi maisha duni, kwasababu wanatumia muda wao mwingi kutengeneza thamani kwaajiri yao peke yao, na wala si kwa watu wengine. Kumbuka kuwa watu mpaka watume pesa kwako ni lazima kuwe na thamani fulani kwako. Ukweli ni kwamba, pesa aliyonayo mtu, mara nyingi ameitolea jasho kuipata, lakini mtu huyo yuko tayari kuiachia kwa hiari, iwapo kitu anachokitaka kutoka kwako kina thamani kubwa kuliko kiasi cha pesa unachomtaka atoe. Kwahiyo, tukitaka kutengeneza pesa kwa urahisi, ni lazima tujikite katika kutengeneza thamani kwa wengine. Na endapo utakuwa umechangia thamani yoyote kwa maisha ya watu wengine, na thamani hiyo ikawa na faida kubwa kwao, basi wewe tunastahili malipo. 

    Binadamu siku zote huwa anatafuta thamani kwaajiri ya kukidhi mahitaji yake ya kimaisha. Kwahiyo, kwa yeyote yule atakayeweza kutengeneza thamani, ni wazi kwamba kila mara pesa itakuwa inamfuata alipo. Watu mara zote wananunua thamani kupitia bidhaa au huduma mbalimbali. Wewe kama mjasiriamali, ni muhimu ukatambua kuwa, watu wanaponunua bidhaa, kinachonunuliwa siyo bidhaa kama bidhaa bali ni thamani yake. Thamani ya kitu, ndiyo huwasukuma watu wengine kutuma pesa zao kwako wewe uliye na thamani fulani. Wajasiriamali tunatakiwa kutambua kuanzia mwanzo wa utengenezaji bidhaa kuwa, thamani iliyoko ndani ya bidhaa ndiyo wateja wanatafuta. Kwa mfano; unapoona mteja amekuja kwenye salooni yako usifikiri amekuja kusuka, kuseti au kunyoa nywele bali anacholenga ni kupendeza na kupendeza ndiyo thamani halisi ya kusuka au kunyoa nywele. 

    Katika zama hizi tulizomo na huko mbele tuendako, maisha mazuri pamoja na ukuaji wa uchumi vitategemea sana uwezo na ujasiri wa watu katika kuhamisha thamani zote zilizoko ndani yao na kuziweka ndani ya bidhaa na huduma mbalimbali. Katika uwekaji wa thamani kwenye bidhaa, tulenge zaidi zile thamani ambazo zinatatua kero sugu kwenye jamii. Endapo thamani zilizotengenezwa zitatoa suluhisho la changamoto kwa watu waliowengi, moja kwa moja watu watakuwa tayari kutoa pesa yao kwa hiari kwenda kwa yule aliyetengeneza thamani.  Jambo la msingi hapa ni watu kuendelea kuelekeza nguvu na maarifa yao, katika kutengeneza na kuzalisha thamani nyingi kadiri inavyowezekana, kwani kwa kufanya hivyo, uchumi wa kaya na taifa kwa ujumla utakuwa sana na Tanzania itaendelea kuwa mahali pazuri pa kuishi.

    Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO

    Sunday, July 12, 2015

    Kama Huko Hivi si Mjasiriamali



    • Mjasiriamali Ujikita Katika Kuzalisha Bidhaa/Huduma kwa Lengo la Kugusa Maisha ya Watu Wengine
    • Uongozi ni Ujuzi Muhimu Sana Unaotakiwa kwa Mtu Anayetaka Kuwa Mjasiriamali

    Nafahamu kuwa kuna watu wengi wanatamani kuwa wajasiriamali na wengine hasa waliojiajiri wanadhani na kuamini kuwa, wao ni wajasiriamali. Kuna dalili zinazoonyesha kuwa jambo hili la ujasiriamali linachukuliwa kimzaa mzaa sana. Imekuwa kitu cha kawaida sana hapa Tanzania, kusikia watu wengi wakijiita wajasiriamali, hasa wale wanaofanyakazi za kujiajiri wenyewe. Lakini je? kitendo cha wewe kujiajiri tu peke yake, kinatosha kukufanya huwe mjasiriamali?. Sasa huyu anayeitwa mjasiriamali ni mtu wa namna gani?  Mjasiriamali ni ujuzi na siyo mtu. Kazi unayofanya, timu ya watu uliyonayo, maisha unayoishi, ukubwa wa kazi yako, maamuzi unayofanya kila siku n.k. vyote hivi vina nafasi kubwa ya kukufanya wewe kuwa mjasiriamali au vinginevyo!.

    Mjasiriamali ni mtu anaona fursa, anaweka timu ya watu pamoja na kujenga biashara ambayo uzalisha faida kutoka kwenye fursa husika”. Ni wazi kwamba wapo watu wengi ambao wameweza kuona fursa na kuamua kuzichangamkia kwa malengo ya kupata faida wao peke yao. Lakini, kama ukiona fursa na ukaona una uwezo wa kuifanyia kazi wewe peke yako, basi ujue wewe ni mfanyabiashara mdogo sana ambaye umejiajiri au umeajiliwa na biashara badala ya wewe kumiliki biashara”

    Kuna tofauti sana kati mtu aliyejiajiri na mjasiriamali. Mtu aliyejiajiri, ni mtu ambaye anaweza kuzalisha 
    bidhaa au kutoa huduma yeye mwenyewe peke yake. Kwa mfano msanii anaweza kuchora picha yeye mwenyewe, daktari anaweza kukutibu jino mwenyewe, au mtu anafuga mifugo yeye mwenyewe. Mjasiriamali, hawezi kufanya vyote vinavyotakiwa kufanyika katika kuendesha biashara peke yake. Mjasiriamali ni lazima awe tayari kupata na kuunganisha vipaji vya watu wenye uwezo na ujuzi tofauti tofauti, ambapo huwaunganisha ili wafanye kazi pamoja kwaajili ya kukamilisha uzalishaji wa bidhaa au huduma fulani. Kwa maana nyigine, mjasiriamali ujenga timu ambayo ujikita katika kuzalisha bidhaa/huduma, kazi ambayo mtu mmoja mmoja hawezi kuifanya yeye peke yake.

    Mjasiriamali ni mtu ambaye anapoamua kufanya biashara mara nyingi anakuwa analenga kutatua changamoto au kero fulani kwenye jamii. Kwa maana nyingine “mjasiriamali ujikita katika kuzalisha bidhaa au huduma mbalimbali kwa lengo la kugusa maisha ya watu wengine  na siyo yeye peke yake”. Sababu kubwa ambayo huwafanya watu wengi kuendelea kuwa wadogo au kuwa na biashara ndogo ni kwasababu biashara wanazoziendesha ni kwaajiri ya kutatua matatizo yao peke yao. Ndiyo maana unakuta mtu anafanya biashara fulani miaka 20, lakini biashara haibadiliki, hiko vilevile na haijawahi kupanuka kwa miaka yote. Watu wa namna hii ndio wengi wamejiajiri na ndio hawa wanaodhani na kuamini kuwa na wao ni wajasiriamali.

    Mjasiriamali ni mtu anayebeba majukumu ambayo yanahitaji timu ya watu. Mjasiriamali ambaye utegemea timu ya watu  kufikia malengo, huwa halipwi mpaka hapo timu yake ikishafanya kile kinachotakiwa kufanyika wa kama timu. Waajiriwa wengi, na wale waliojiajiri wanalipwa kulingana na kile ambacho wanaweza kufanya kama wao binafsi. Tofauti na waajiriwa/waliojiajiri, mjasiriamali amejijengea tabia ya kufanya kazi bila kulipwa, kutegemeana na unachofanya wakati mwingine unaweza kulazimika kukaa muda mrefu zaidi ya mwaka ndio unakuja kulipwa kama umefanikisha kile ulicho kilenga. 

    Malipo ya mjasiriamali ni baada ya kukamilisha kazi na timu, wakati malipo ya waajiriwa wengi ni kabla ya kuanza kazi. Kama alivyo mkandarasi wa majengo, huwa anatumia watu kujenga nyumba; mfano: mafundi bomba, umeme, seremara na wataalam wengine kama wasanifu majengo, wahasibu n.k. na mjasiriamali utafuta watu tofauti tofauti kama vile, mafundi mchundo (technicians), wasomi, na wataalam wengine katika kumsaidia kujenga biashara”. Kwahiyo, ni muhimu tukatambua ndani ya fikra zetu kuwa,  mjasiriamali ni mtu ambaye ni kiongozi, japo wakati mwingine yawezekana wasifanye kazi na timu zao moja kwa moja. “Kadiri utakavyoongoza timu ya watu ambao ni wazuri wenye uelewa, haulazimiki kufanya kazi kama sehemu yao, ndiyo vizuri na ndiyo utafikia kiwango cha kuitwa mjasiriamali mkubwa.

    Kuna watu wanamiliki makampuni mengi, lakini huwa hawafanyi kazi katika makampuni hayo. Ndiyo maana wanaweza kutegeneza pesa zaidi na kufanya vitu vingi bila kuwa wamefanya kazi. Ni kutokana na hali hii, tunakumbushwa kuwa, “Uongozi ni ujuzi muhimu sana unaotakiwa kwa mtu anayetaka kuwa mjasiriamali”.” Uongozi siyo zawadi ni ujuzi na wala hauzaliwi nao bali ni kitu ambacho ukiamua unajifunza. Ukitafakari kwa kina unagundua kuwa sisi wote tuna chembe chembe za ujuzi wa uongozi. Tatizo lililopo kwa watu waliowengi ni kwamba, watu wengi utumia maisha yao yote kukuza ujuzi katika taaluma nyingine tofauti na uongozi, ndiyo, maana kuna watu wengi ni waajiriwa na wengine wamejiajiri. Ni watu wachache sana, ambao wanatumia muda wa maisha yao kukuza ujuzi wao wa uongozi, kwasababu, uongozi  ndio ujuzi ambao unatakiwa kwa wajasiriamali (wamiliki wa biashara). Kwahiyo, ni vizuri watu tukaamua kuwa wajasiriamali na kujikita katika kusaka kila aina ya ujuzi utakaotuwezesha kuongoza timu zetu, hili hatimaye tuweze kumiliki biashara kubwa na mwisho kufikia maisha ya ndoto yetu.

    Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO

    Sunday, July 5, 2015

    Unashangaa Nini? Pesa Yako ni Sanamu



    • Ukitumia macho ya ubongo  unaona "Wallet" zetu hazijabeba pesa, bali vitu tofauti
    • Ikiwa biashara yako wewe ni kufuga na kuuza kuku, “basi elfu kumi yako ni kuku”
    Ilikuwa siku ya jumanne ya tarehe 30/06/2015, kwenye kipindi cha tuongee asubuhi kinachorushwa na ITV kila siku mara baada ya kusoma magazeti asubuhi. Zamu hii, alikuwa akihojiwa kiongozi mmoja wa dini, ambaye alikuwa akijaribu kuelezea jinsi walivyojipanga katika kuandaa na kukamilisha siku ya mkesha wa kuombea uchaguzi mkuu wa Tanzania mwaka huu, na akasisitiza kuwa maombi yatafanyika mkesha wa 8/8/2015. Katika mazungumzo yake akagusia jambo moja muhimu kuwa kwa sasa watu wengi wanatanguliza pesa mbele hata kabla ya kufanya kazi na wengine wanadai walipwe pesa, ndipo wapige kura za ndiyo kwa wagombea, hasa katika kipindi hiki tunapoelekea uchaguzi mkuu. Kiongozi huyu, alitumia fursa hiyo kuwahasa watanzania kujiepusha na tabia ya kupenda kutanguliza pesa mbele. Katika kuweka msisitizo wa kuonyesha ni kwa jinsi gani pesa siyo kitu halisi; alirejea maandiko kutoka katika vitabu vitakatifu yanayosema kuwa “Pesa ni Sanamu”. Kitendo cha watu wengi kushindwa kutambua usanamu uliopo juu ya pesa, ndicho chanzo cha kuwepo kwa changamoto nyingi zinazotukabili leo hii kama watu binafsi na taifa kwa ujumla.

    Dhana hii ya “pesa ni sanamu” ni muhimu tukaijua na kuielewa vizuri,  ili hatimaye mimi na wewe tupate kujinusuru kwa kutoka kwenye kundi kubwa la watu wanaotafuta pesa kama “sanamu”. Yawezekana leo hii hatupati pesa ya kutosha na unaangaika sana, kwasababu fikra na mitazamo yako ni ile ile ya kudhania kuwa pesa ni kitu halisi kumbe ni “sanamu”. Tafsiri ya neno “pesa ni sanamu” inamaanisha kwamba, pesa siyo kitu halisi bali ni mfano au kivuli cha bidhaa na huduma mbalimbali, ambazo hazionekani kwa macho yetu ya kawaida. Kwa maana nyingine, pesa ni kitu ambacho husimama badala ya bidhaa na huduma mbalimbali hasa wakati wa zoezi zima la ubadilishanaji vitu kati ya muuzaji na mnunuzi.

    Usanamu wa pesa unatokana na ukweli kwamba, pesa uliyonayo mfukoni imetokana na wewe kuwapa watu wengine bidhaa au huduma ulizokuwa nazo; na wao kwa hiari yao wakaamua kukupa vithibitisho ambavyo ni kama stakabadhi zinazothibitisha uwepo wa makabidhiano ya bidhaa/huduma kati yako na watu wengine. Kwahiyo, unapoangalia pesa uliyonayo mfukoni ujue una mfano tu wa vitu vilivyofanya pesa kiasi fulani ije kwako. Kwenye wallet zetu hatuna pesa bali tuna vitu tofauti tofauti. Mfano: utakuta mtu mwingine kwenye wallet yake ameweka huduma ya mapambo, usafiri, ufundi, elimu, kuchangia mawazo kwenye vikao n.k. Wengine wallet zao utakuta bidhaa kama vile chakula, nguo, dawa, jiko, taa, simu, mafuta n.k. Ukiamua kutumia macho ya ubongo wako utakubaliana na mimi kuwa, pesa tulizonazo kwenye wallet zetu hazifanani.

    Wote tunaweza kuwa na noti ya shilingi elfu kumi za kitanzania, ambazo kwa macho ya kawaida zinafanana, lakini kwa macho ya ubongo, wallet zetu hazijabeba pesa bali zimebeba vitu tofauti mtofauti kabisa. Kwahiyo, ikiwa wewe biashara yako ni kufuga na kuuza kuku basi elfu kumi yako ni kuku; kama wewe ni mwandishi basi elfu kumi yako ni habari, gazeti au kitabu na ikiwa wewe ni mshereheshaji basi elfu kumi yako ni ushereheshaji, ualimu, uchoraji n.k. Mifano hii michache inatuonyesha kuwa, pesa zote tulizonazo hazifanani kabisa, isipokuwa bidhaa na huduma tunazozalisha ndizo hubadilika na kuwa kitu kimoja ambacho ni sanamu yaani “pesa” inayoonekana kwa macho yetu ya kawaida. 

    Kwa wale wote wanaoamini kuwa pesa siyo sanamu, maana yake ni kwamba vitu vyote vinavyotengeneza pesa waliyonayo, hawawezi kuviona kwasababu macho yao ya ubongo yamepofuka na hivyo wamebakia kutumia macho ya kawaida peke yake. Ukiangalia pesa kwa macho ya kawaida (kwa mujibu wa kinachonekana), kiukweli wewe utaishia tu kuona noti za elfu 10, 5, 2, 1 n.k. ikiwa kuona kwako kutaishia hapo, basi na wewe ni mmojawapo wa watu hawaoni pesa bali wanaona “sanamu”. Mtu anayeona sanamu kila wakati, hawezi kujua mahali kitu halisi kilipo na wala hatajua hiyo pesa ilikotoka. Ndiyo maana inapotokea mtu akapata pesa na baadae kuishiwa, ni vigumu kuzipata tena kwa haraka kwasababu, anakuwa tayari ameishasahau zilikotoka. Na kwa yule anayetambua kuwa pesa aliyonayo kwenye wallet ilitokana na mkusanyiko wa bidhaa na huduma mbalimbali; ni rahisi sana kwake yeye kuzipata pesa kwa muda mfupi, kwasababu chanzo chake kinajulikana na kimekuwa kikitunzwa na kuimarishwa mara kwa mara.  

    Kwenye jamii yetu kwasasa, bado watu wengi wanaishi kwenye ulimwengu wa vitu vinavyoonekana kwa macho ya kawaida. Tunahitaji kujifunza kutumia macho yetu  ya ubongo katika kuona vitu vinavyoonekana na visivyooekana na hapo ndipo tutaweza kuiona pesa halisi badala ya sanamu tunayoiona sasa. Ni wakati muhafaka sasa kwa watu wote wanaotaka mafanikio makubwa kugeukia kile kinachofanya pesa ije kwenye wallet zao; kwani hicho ndicho kitu halisi. Ni muhimu, juhudi na maarifa yetu yote yakaelekezwa kwenye kuzalisha thamani kupitia vitu na huduma mbalimbali ili kukidhi mahitaji ya watu wengine na jamii kwa ujumla. Na tuyafanye yote haya, huku tukiamini kufanikiwa na hakika tutafanikiwa.

    Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO