Nadharia
ya kutafuta kazi eti! Inayoendana na mapenzi yako Ndiyo chanzo cha watu wengi
kuchagua kazi na kuishia kukosa kazi. Wataalam wa masuala ya kazi na
Ujasiriamali wanasema kuwa, Katika ulimwengu wa kazi kuna makundi makuu mawili yote
yakitofautiana kulingana na mtizamo juu ya “kazi” . Kundi la kwanza lina
mtizamo wa kujiuliza swali la “dunia
inaweza kumpatia mtu kitu gani kinachoweza kumridhisha au kumfurahisha”? (Passion
Mindset) na kundi la pili lina mtizamo wa kujiuliza swali la “Mtu anaweza kuipatia dunia kitu gani kitakacho
wafurahisha au kuwapendeza watu”? (Craftsman Mindset).
Katika
Utafiti uliofayika duniani imekuwa ni vigumu sana watu wa kundi la kwanza
kuweza kufanya kazi kwa bidii na kuishi kwa furaha. Kukosekana kwa furaha
kazini, siyo tu kumetokana na maslahi duni bali ni kutokana na ukweli kwamba,
ni vigumu kampuni husika kuweza kumridhisha kila mtu kwa jinsi apendavyo bila
kuingilia maslahi ya kampuni hiyo, kwa hiyo kinachotokea ni ni huyo mtu kuanza
kupambana na mwajiri kwa kudai mambo ambayo yanaweza kumfurahisha au kumridhisha
kama yeye binafsi. Na iwapo mambo hayo hayapati basi migogoro na mwajiri inaanza
mara moja, matokeo yake mtu anaanza kuishi kwa misuguano mingi na mwisho wa
yote anaishi bila furaha kila anaposhindwa kupata maslahi aliyotarajia kipindi
kile alipo wazia dunia itampatia nini.
Kutokana
na mtizamo wa “dunia itakupatia nini” mtu huendelea kujaribu huku na kule akiwa
ujatulia kabisa, huku ukitafuta chochote cha kupata kutoka kwenye dunia. Mara
nyingi, maisha ya namna hii, huwa ni ya kubahatisha au kujaribu jaribu. Katika
kubahatisha, mtu anafika mahala dunia inampatia fursa ya kazi (ajira) kutoka
kwa watu wengine waliotengeneza kazi, hapo ndiyo hujenga matumaini na matarajio
makubwa ya kukidhi furaha yake na tamaa zake nyingine kutoka kwenye ajira
aliyopewa. Baada ya kipindi kifupi, mtu huyu ghafla unashangaa hapati kile
kilichokuwa kinamfurahisha kwenye kazi ya ajra aliyopewa miaka miwili iliyopita.
Hali
ya kutopata kile alichotarajia mwanzo, humfanya huyo mtu kutafuta suluhisho la
haraka, ambalo huwa ni ni kutafuta sehemu nyingine yenye kumpatia furaha na
maslahi mazuri zaidi na hapo anafurahia kwa muda na baadae tena kero mpya
zinaibuka upya. Kwahiyo, inakuwa ni mzunguko ambao unakuwa maisha yenye furaha kipindi
kifupi na kipindi kirefu cha kero nyingi; hali ambayo husababisha kiwango
kidogo sana cha ufanisi, ikiwa ni pamoja na uzalishaji chini ya kiwango
inachotegemewa. Watu wengi katika kundi hili la kwanza, hawapendi kazi
wanazozifanya, isipokuwa wanaendelea kufanya kazi kwasababu wanalipwa pesa.
Kutokana
na kuhamahama kwa watu ambao tayari wana kazi (ajira) kutoka mwajiri mmoja
kwenda mwingine, ndiyo sababu ya kuongezeka kwa kundi la watu wanaotafuta
ajira. Kwani kunakuwa na kundi la vijana ambao ni wapya (walio hitimu karibuni)
na kundi la zamani wote wakishindana kupata nafasi chache zilizoko kwenye soko
la ajira. Kundi la watu wa zamani, ambao kimsingi ni wazoefu, wanatumia kigezo
cha uzoefu ujuzi kazini kuwashinda wapya hasa katika nafasi zinazosemekana zina
marupurupu makubwa.
Kwa
upande wa kundi la pili lenye mtizamo wa “Mtu
anaweza kuipatia dunia kitu gani kitakacho wafurahisha au kuwapendeza watu?;
Mtizamo huu unafanana sana na mtizamo watu wa sanaa na maonyesho kwa ujumla.
Kundi hili kwa kuongozwa na mtizamo huu, kila mara lina jaribu kuumiza vichwa
vyao kufikiri na kutafakari ni kitu au vitu gani waifanyie au waipatie dunia!.
Kwakuwa kundi hili linashughulika tu na kufikiria cha kufanya, linajikuta swala
zima la kazi siyo tatizo kwasababu ni watu wa kundi hili wanaoibua na kutengeneza
kazi. Kundi hili linapokuwa limeibua na kutengeneza kazi ndipo linajikuta likikabiliwa
na majukumu mengi yaliyopo mbele yake katika kufanikisha kazi hizo. Hili
kukabiliana na majukumu hayo, kundi hili hulazimika kutafuta watu waliobobea katika
fani mbalimbali, ili waweze kusaidia katika kutimiza na kufanikisha malengo ya
kazi husika. Mfano chukulia ‘Wasanii wa muziki na firamu za kitanzania’
ukitafiti watu hawa utagundua kuwa wanaipenda sana kazi yao, na kutokana hali
hiyo kupenda kazi yao, wemeweza kuwekeza nguvu na maarifa yao yote na matokeo
yake, wameweza kutegua kitendawili cha ajira , jambo ambalo linaonekana
kuwaelemea sana wasomi wengi hasa wanaotoka vyuoni.
Katika
nchi zote duniani, wanaomiliki uchumi wa nchi huska ni wale tu walio na utashi
na uwezo wa kutengeneza kazi, na hii ni kutokana na ukweli kwamba faida yote inayotokana
na kazi husika mara nyingi inachukuliwa na yule tu! aliyetengeneza kazi,
waliobaki bila kujali idadi yao kwenye kazi husika, wanaendelea kuhesabika kama
sehemu ya gharama za uendeshaji. Kwa hapa Tanzania, wasomi wengi tunayo nafasi
nzuri zaidi ya kuweza kutengeneza kazi kuliko wale ambao hawakusoma, kwasababu,
wasomi ni rahisi kupata ujuzi na habari za mambo mbalimbali yaliyoko duniani na
kuzitumia katika maamuzi ya kutengeneza kazi mbalimbali ambazo zingeweza kuvuta
maendeleo ya haraka hapa nchini. Cha ajabu kabisa, hapa Tanzania, wale ambao
hawakubahatika kuedelea na shule, ndio wengi wao waliamua kutengeneza kazi na
wemejiendeleza Kiasi cha kubobea katika kazi hizo hizo walizozitengeneza.
Kwasasa, watu hawa ndio wanaendesha uchumi wa nchi huku wakitoa pia ajira kwa
wasomi ambao wangeweza kutengeneza kazi nyingine nyingi zaidi.
Watu
wengi katika kundi hili linaloongozwa na mtizamo wa “nitaipatia nini dunia”? wanapenda sana kazi zao ambazo
wamezitengeneza wenyewe. Na kwasababu hiyo; wanazifanya kwa moyo, umakini,
kujituma na kwa juhudi na maarifa. Mambo yote haya, ni nadra sana kuyakuta
kwenye kundi la kwanza ambalo ni la wenye mtizamo wa “dunia itanipatia nini”?. Kundi hili la pili, ndio wanaotoa ajira
kwa wale wanaoitwa “wasomi” na hii nikutokana na ukweli kwamba, wale ambao
hawakusoma walijikuta wakilazimika kutengeneza kazi ili waweze kuishi. Mfano ni
wakulima, wasindikaji; wavuvi, wafugaji; wasanii, wafanyabiashara, mafudi n.k.
bila watu hawa mambo hayaendi na serikali inategemea sana kundi hili kupata
pesa za kugharimikia huduma za jamii.
Mwisho
nipende kusema kuwa, kazi zinazo subili kutengenezwa zipo nyingi sana hapa
Tanzania, lakini ajira ambazo zinatafutwa na watu wengi ndizo chache sana. Kwa
maana nyingine, ajira haziwezi kuwa nyingi kama kazi zinazotengenezwa ni chache
sana. Ewe mtanzania jiunge na mtandao wa watengeneza kazi, ili uweze kufanikiwa
na kuishi maisha yenye furaha. Kuanzia leo, acha kulalamikia watu wengine kwa
mambo ambayo ni majukumu yako na jitenge kabisa na watafuta ajira. Bila kujali
umesomea nini, anza leo kufikiria ni kitu gani unaweza kuwapatia watu
wakafurahi kwa kukidhi mahitaji yao, na iwapo utafanya hivyo, basi utakuwa
umepata suluhisho la kudumu na hivyo kuweza kutegua kitendawili cha “kazi”
maisha yako yote.
Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO.
~TWENDE
KAZI PAMOJA~
No comments:
Post a Comment