Tuesday, March 15, 2016

Ukiendelea Kutafuta Muda Utazidi Kuhailisha Mengi ya Muhimu!


“Muda ni bure lakini huwezi kuuza kwa bei yoyote, huwezi kuumiliki lakini unaweza kuutumia, Huwezi kuutunza lakini unaweza kuupoteza, ukishakuwa umeupoteza huwezi kuupata tena” ~ Harvey Mackay
 
Watu wengi tuko busy sana katika kutafuta muda eti! Wa kufanya mambo makubwa maishani. Lakini imeonekana kuwa pamoja na kutafuta muda, bado haupatikani kirahisi, kwani malalamiko ya watu kuhusu kukosa muda wa kutenda kazi mbalimbali ni mengi.

Nadhani na wewe umesikia mara nyingi watu wakilalamika kuwa wanashindwa kufanikisha jambo fulani kwasababu ya uhaba wa muda. Malalamiko haya yanatokana na.....
ukweli kwamba, watu kwenye fikra zao wanadhani muda haupo au uliopo ni kidogo sana.

Ndiyo maana watu wakiwa wanawahi kufanya jambo fulani wanadhani muda unakimbia kumbe wao ndio wanaokimbia. Muda haujawahi kukimbia hata siku moja kutokana na ukweli kwamba MUDA ni kitu cha kutengenezwa na wewe binafsi.

Siku zote shauku na hamasa ya kufanya shughuli fulani ndiyo ukufanya uwe mtu mwenye haraka na hivyo kuona kama vile kinachokimbia ni muda. Unapokuwa mtu wa kuona muda unakimbia basi ujue kuwa wewe ni kati ya wale wanaodhani muda ni tatizo.

Binafsi nimekuwa nikisikia kwa watu wakisema “Nataka kufanya kazi au kitu fulani LAKINI tatizo ni MUDA”. Eti! mtu anadiriki kusema kuwa muda ni tatizo. Muda hauwezi kuwa tatizo kama ukiamua au ukiwa na nia ya kufanya kitu fulani.

Kauli nyingi za “tatizo ni muda” zinaonyesha kuwa watu tuliowengi tunadhani na kuamini kuwa muda unajileta na kujipanga wenyewe. Pengine ndiyo maana hata wewe umejenga tabia ya kuhairisha mambo kila mara ukidhania kuwa ipo siku ambayo itatokea ukamilishe shughuli ambayo ilipaswa kufanyika siku za nyuma.

Ni vema tukafahamu kuwa dhana ya muda inaendana na maamuzi ya kuchukua hatua. Kila utakapoamua kufanya jambo fulani, ujue kuwa muda wa kufanya hivyo utapatikana mara moja na endapo utaamua kutofanya jambo hilo, basi ujue kuwa muda hautapatikana kamwe!.

Ukweli juu ya muda ni huu….“huwezi kukosa muda wa kufanya kitu unachokitaka”. Kwa maana nyingine ni kwamba, unapoona mtu anakwambia siwezi kufanya biashara au shughuli fulani kwasababu ya muda, basi ujue kuwa mtu huyo HATAKI KABISA kufanya kazi hiyo. Kinachotokea ni yeye kujificha kwenye kivuli cha “kukosa muda”.

Mara nyingi watu wengi tunapenda kutumia MUDA kama kisingizio cha kutofanya vitu ambavyo hatutaki/hatupendi kuvifanya, lakini wakati huo huo hatutaki kuwaudhi marafiki zetu ambao wanataka tushirikiane katika kufanikisha mambo fulani fulani. Tumekuwa siyo wakweli (wanafiki) wa nafsi zetu, kwani kila mara tunapofikiria kufanya jambo kubwa, moja kwa moja tunakimbilia kuiambia nafsi kuwa MUDA ni tatizo.

Kila mara unakabiliwa na manun’guniko huku ukizidi kujisemea moyoni “ningependa kufanya jambo hili lakini linahitaji muda wa kutosha”. Kila siku unaendelea kujisemea hivyo miaka nenda rudi bila kuchukua hatua, utadhani kuna siku labda alihaidiwa kuletewa muda ili akafanye jambo hilo………….Nasema “haitakaa itokee upewe muda wa kufanya mambo unayoyataka wewe”

Neno “TATIZO NI MUDA” ni baya zaidi kuliko kauli ya “HAPANA”. Kwetu sisi tunaofahamu maana ya hapana, tunajua kuwa ni sawa na kusema “SIYO SASA HIVI”. LAKINI anayekwambia TATIZO NI MUDA maana yake ni kwamba huyo mtu haitakaa itokee siku hata moja apate huo muda. Tusikae tukadhani kuwa muda ni kitu ambacho tutakipata hivi hivi bila sisi wenyewe kuamua kufanya hivyo.

Kupitia makala hii, napenda kukufahamisha kuwa kitu kinachoitwa MUDA ni kitu cha kufikirika tu na ni kitu ambacho kipo kwa wingi sana. Yaani ni rasilimali ambayo ipo kwa kila mmoja, ni wewe tu kuitumia vyovyote unavyotaka.

Kwa taarifa yako ni kwamba suala zima la muda linakuwepo kama binadamu anazo shughuli ambazo zinahitajika kukamilika mapema iwezekanavyo. Endapo mtu ukiamua kutokuwa na chochote cha kufanya, basi kwako wewe dhana ya muda haina maana yoyote.

Kama huna cha kufanya, kwako wewe dakika hazipo, masaa hayapo, siku hazipo, miezi haipo na hata miaka haipo bali upo wewe tu! Kwa maana nyingine ni kwamba, kadili unavyotakiwa kukamilisha shughuli nyingi kwa mara moja ndipo suala la MUDA linakuwepo kwani unajikuta unalazimika kuhesabu kila sekunde inayopita.

Wakati umefika sasa wa kujenga mtazamo mpya juu ya suala zima la muda. Muda umefika wa kutumia muda kufanikisha ndoto zetu. Tunahitaji kufaidi rasilimali hii “MUDA”, na ili tufaidi ni lazima tujifunze kupanga kazi zetu tunazofanya kila siku kulingana na umuhimu wake katika kufikia doto zetu za maisha. Huu siyo muda wa kuendelea kusema “napenda ujasiriamali au kitu fulani, lakini kwangu tatizo ni Muda”.

Hizi ni zama za kusema “Ninatenga Muda” tarehe, wiki, mwezi, mwaka……….kwaajili ya kufanya kazi 1,2,3……..n.k. Kuliko kila mara kulalamikia muda kana kwamba muda ni kitu ambacho kipo tu kama maji ambayo ukitaka unajichotea. Lazima tufikie mahala tuache kulaumu “uhaba wa Muda”.

Ni muda wa kukili kuwa sisi ndio tumekuwa kikwazo cha kutofanyika kwa mambo fulani fulani.Tukisha kili udhaifu huu, mara moja sasa tuwe watu wa kutenga muda wa kufanya chochote tunachokitaka, kwani sisi wenyewe ndio wamiliki wa kiwanda cha kutengeneza “Muda”.

Katika hili la “Muda” unahitaji kuendelea kujifunza kila wakati hasa kupitia mtandao huu wa “MAARIFA SHOP”, kama una dhamira ya kuelimika kwa lengo la kubadili maisha yako gonga maneno ya “KARIBU MAARIFASHOP, hapa utakuwa tayari kupata moja kwa moja mambo mapya ya mtandao huu.

No comments: