Saturday, March 19, 2016

Elimu ya Ujasiriamali Haipo Chuoni Iko Wapi?

“Usione aibu kutokana na kushindwa, jifunze kutokana na kushindwa na uanze tena” ~ Richard Branson, mwanzilishi wa kampuni ya Virgin Group.

Mara nyingi shuleni tulifundishwa kutii sheria na taratibu kama siyo kanuni; kufanya vitu kwa kutumia vitabu na kama ukionekana ukikaa mbali na kundi, haraka haraka unasukumwa tena kwenye tanuru ambalo hasa ni......
mfumo wa elimu rasimi, ambao siku zote utuweka na kutuandaa ili tufanane wote. “Shuleni siyo sehemu muhafaka kwa mjasiriamali”.

Mjasiriamali ni mtu anayefikiri tofauti na kiukweli; kila mmoja anafikiri na kujifunza tofauti. Ndiyo maana mfumo wa elimu rasimi ambao unalazimisha watu wote kufikiri sawa unaua kabisa roho na fikra za ujasiriamali. 
Wajasiriamali ni watu ambao wanafanya vitu tofauti na wanakwenda kinyume na mazoea au mtazamo uliozoeleka kwa watu wengi. Mara nyingi, wajasiriamali ukataa kulazimishwa kuishi maisha wanayoishi watu wengine na pia ukataa kufikiri sawa na watu wengine, haijalishi ni wengi kiasi gani.

Mfano: Watu wengine wanaambiwa hakuna kuuza mahindi kuna baa la njaa linakuja, LAKINI kama mjasiriamali yeye hawezi kukaa akaamini yale aliyoambiwa na watu wengine, badala yake atafikiri na kutenda tofauti na alivyoambiwa. Hapa yeye ataamua kuuza mahindi yake na pesa itakayopatikana anaweza kununua mbuzi wenye mimba ambao baada ya miezi kadhaa watakuwa wamezaana na kuongezeka maradufu, pia watakuwa wamepanda thamani kwa kiwango kikubwa wakati huo, kuliko ambavyo angeendelea kutunza mahidi.

Mjasiriamali huyu ukimfikiria haraka haraka unaweza kudhani ni mtu mkorofi, lakini ukimfikiria kwa mtazamo wa kiujasiriamali utamuona ni mbunifu wa kuigwa. Kwa kifupi ni kwamba mjasiriamali ni mtu ambaye anapenda kutengeneza, kuumba, kutenda, kuibua kitu kinachojibu changamoto za wakati huo; siyo kufuata misaafu ya vitabu vya kanuni zilizotengenezwa na mtu mwingine.

Ujasiriamali ni nadra kufundishwa darasani: Leo hii, elimu inabadilika. Wakati watoto wengi katika shule za msingi na sekondari bado hawajifunzi “Pesa na Biashara”; vyuo na hasa vya biashara, vimeanza kufundisha kozi mbalimbali za ujasiriamali kwa wale wote ambao wana malengo ya kujenga na kukuza biashara zao. Jaribio lolote la kuendeleza na kukuza ujasiriamali ni la msingi sana na la kuigwa; lakini kuwa mjasiriamali aliyefanikiwa ni nadra sana kufundishwa darasani. Wajasiriamali lazima wawe ni watu ambao wako tayari kubadilika haraka kulingana na hali au changamoto zilizopo. Lazima wawe na roho ya ujasiri wa kupambana na changamoto kadiri zinavyoibuka bila kukata tamaa. Mambo yote haya hayawezi kutoka shuleni.

Wajasiriamali wanapata elimu wapi? Kama uliwahi kukutana na mjasiriamali aliyefanikiwa, birashaka utakuwa uligundua kuwa huwa hawapendi kupoteza muda hata kidogo. Muda wao una thamani sana, kwani wao wanafanya vitu vingi wao wenyewe. Kwa wajasiriamali walio wengi, kujifunza kutokana na makosa yao wenyewe na wajasiriamali wengine ndiyo njia kuu ya kujifunza.

Kwa maana nyingine ni kwamba, kujifunza kisawasawa kunaanza pale ambapo unathubutu kuanza kufanya kwa vitendo. Hii ndiyo sababu, matukio ya kujenga mtandao na program za kufundwa na wajasiriamali wengine, kujifunza kutoka kwa watu waliofanikiwa, kujisomea vitabu unavyopenda mwenyewe ni sehemu muhafaka ya kupata na kukuza elimu yako juu ya umiliki biashara yako. Siyo tu kuwa sehemu hizi ni muhafaka kwa kwaajili ya kukutana na watu, bali ni sehemu muhimu na muhafaka kwa upatikanaji wa rasilimali kama fedha za mitaji, elimu ya mahesabu na umiliki wa fedha, masoko na teknolojia—vyote hivi ni vitu ambavyo wajasiriamali tunahitaji.

Kwahiyo, wajasiriamali tunahitaji kuwa “makini” ili kufanikiwa? Ndiyo … lakni siyo katika namna au njia ambayo wengi wanafikiri ndiyo “umakini”.

Anza kufanyia kazi mradi wako sasa, kwani huo ndio utakuwa kichocheo cha wewe kujifunza na kupata elimu halisi ya ujasiriamali. Tukutane hapa “MAARIFA SHOP”,kwa elimu na kujifunza zaidi.

No comments: