Thursday, January 12, 2017

Hii ni Njia Sahihi Kujipatia Uhuru wa Fedha




"Usikae kitandani mpaka pale utakapoweza kutengeneza pesa ukiwa kitandani" ~ George Burns
 
Mchakato ni mpangilio wa shughuli mbalimbali ambazo ufanyika hatua kwa hatua mpaka kufikia hatua ya kutoa matokeo yaliyolengwa. Kwa maneno mengine, kitu mchakato ni zaidi ya kukamilisha shughuli moja na hii ndiyo tofauti kubwa kati ya mchakato na shughuli.

Kwa mfano; ukiambiwa kuwa kutajirika ni mchakato, basi fahamu moja kwa moja kuwa utahitajika kufanya shughuli nyingi hatua kwa hatua kwa kipindi kisichopungua miaka
mitatu na kuendelea kutegemea na ukubwa wa ndoto yako. Mchakato siyo kitu cha kukamilika siku moja, lazima ujipe muda kama kweli umedhamilia kwa dhati kutajirika (uhuru wa kifedha).

Siku zote watu wengi hawapendi kufanya vitu ambavyo vinapitia mchakato mrefu na ambavyo uchukua muda mrefu kuleta mafaniko. Wengi wanakimbilia vitu vya haraka na ambavyo mchakato wake ni mfupi.

Kutokana na uzoefu wa watu wengi waliofanikiwa duniani, inaonekana kwamba, mambo mengi yenye kuleta mafanikio katika maisha yanapitia mchakato mrefu na lazima yafanyike hatua kwa hatua kila siku. Hii ni kutokana na ukweli kwamba shughuli moja inapokamilika inachangia mafanikio kidogo kidogo.

Mafanikio kidogo kidogo unayopata kila siku ndiyo mwishoni yakiunganika yanaleta mafaniko makubwa siku za mbeleni. Kwahiyo, ni vema kila mmoja akatabua na kufahamu kuwa ni muhimu unapokuwa umeanza mchakato wa kutajirika ni lazima kujitahidi na kukamilisha shughuli zote zinazotakiwa kufanyika ndipo usubilie matokeo.

Kutajirika au kupata uhuru wa fedha ni “mchakato”, siyo jambo la kufanya kwa siku moja, mwezi au mwaka mmoja, halafu ukaacha ukafikiri utajiri wa uhakika utapatikana hivi hivi—haiwezekani! Utajiri wa uhakika kama ulivyo mchakato, ni kitu kinachopitia hatua mbalimbali kabla ya kupatikana. Hatua ya kwanza kabisa ni mapinduzi ya fikra.

Watu wengi tunahangaika kutafuta uhuru wa kifedha (kipato) au utajiri bila mafanikio, kwababu kubwa moja ambayo ni kutobadirika kwa fikra zetu miaka yote. Tumeshindwa kutengua fikra na mawazo ya zamani, ambayo kimsingi tulilishwa na familia, marafiki zetu, watu tuliosoma nao na wale wote wanaotuzunguka kila siku.

Kuna mawazo mengine potofu tunaendelea kuyafuata na wakati huo huo hatujui kama tunayafuata. Mfano: mawazo kama vile "usifanye makosa" au "pata kazi nzuri yenye kukuhakishia usalama"; "hakiksha udaiwi – deni ni kitu kibaya"; kama ukoo wenu siyo matajiri hata ufanyeje huwezi ukatajirika" n.k. Yote hayo ni baadhi ya mawazo mabaya na yenye kukupoteza kama wewe ni mtu ambaye unataka kutajirika haraka iwezekanavyo.

Gharama za kuwa tajiri ni pamoja na gharama za kuchunguza na kutathimini mawazo yako ya zamani, ili kutafuta ni mawazo yapi uyabadilishe. Pale unapokuwa umebadirisha fikra moja, ni lazima pia kubadirisha hisia na imani ili vyote viendane na mawazo mapya. Kama nilivyowahi kuandika huko nyuma, maisha ni mabadiriko.

Lakini, unabadirikaje? Unabadirika kwa kuanza mchakato wa kujifuza vitu vipya. Unaweza kujifunza kwa njia tofauti tofauti. Mfano unaweza kujenga tabia ya kusoma vitabu, kushiriki semina za mafunzo na kusoma chini ya uongozi wa kocha au “mtu ambaye amefanikiwa kwenye jambo unalotaka kujifunza au kulifanya”.

Kama ulivyo utajiri, elimu na hasa ya ukubwani nayo ni mchakato. Nasema elimu ya ukubwani kwasababu, elimu tuliyoipata tukingali wadogo au vijana, mchakato wake ulijikita katika kutuandaa ili tuwe waajiriwa wazuri. Ndiyo maana watu wengi upenda kusema kuwa “nenda shuleni ukasome ili upate kazi nzuri”.

Watu wengi hawajawahi kuhoji utamaduni huu kwenda shule kwa lengo moja tu la kuajiriwa au kuwa mtumishi wa ndoto za watu wengine. Kwa mtu ambaye ni mdadisi, angeweza kuuliza, “Itakuwaje kama sitaki kuwa mwajiriwa?

Kwa jinsi hali ilivyo hapa Tanzania, kama mtu siyo mwajiriwa au hana mpango wa kuwa mwajiriwa, anadhani hakuna haja ya kusoma. Lakini, ukweli ni kwamba, suala la kusoma na kujifunza mambo mapya halina mjadala kama tunataka kuwa wawekezaji na wafanyabiashara wakubwa.

Uzoefu unaonyesha kuwa usiposoma na kujifunza mara kwa mara, kuna uwezekano mkubwa wa biashara yako unayofanya kurudi nyuma kwa kasi ya ajabu. Hii ni kutokana na ukweli kwamba katika mazingira tunayoishi sasa, kuna mabadiriko mengi yanayoibuka kila siku katika nyanja nyingi za kijamii na kimaisha.

Rai yangu kwako ni kwamba usiache kujifuza. Hakikisha suala la kujipa elimu au maarifa liwe ni ajenda ya kudumu na liwe ni sehemu muhimu katika mchakato wako wa kutafuta utajiri na uhuru wa kipato.

Kama ambavyo nimetangulia kusema “kwamba kumtumia mwalimu au kocha mahili ni mojawapo ya njia ya mkato kuelekea kwenye mafanikio makubwa". Na kwasababu hiyo hiyo, nakualika uendelee kuwa karibu na MAARIFA SHOP ambako elimu na maarifa yenye kukuwezesha kupata mafanikio makubwa ni halali yako.

No comments: