Sunday, January 8, 2017

Je? Wewe ni Mwekezaji au Mfanyabishara



"Soko la hisa ni kifaa cha kuhamisha pesa kutoka kwa watu wasiokuwa na subira kwenda kwa wenye subira” ~ Warren Buffet.

Kwa mwaka huu wa 2017, unahitaji mwanga ili pale palipokuwa hapaonekani paonekane na wewe ikuwie rahisi kupita kwa lengo la kwenda kwenye mafanikio hasa ya uhuru wa fedha (kipato). Ukweli ni kwamba huwezi kufikia maisha ya kiwango cha kupata uhuru wa fedha au kipato kama bado..
ujaelewa tofauti iliyopo na uhusiano uliopo kati ya Mwekezaji na “Mfanyabiashara”. Mwanzo wa wewe kuweza kufanikiwa katika ulimwengu wa wajasiriamali na matajiri, ni pale utakapoelewa lugha ya pesa au maana halisi ya maneno tunayotumia kila siku katika kuwasiliana juu ya masuala yote ya kutafuta pesa, ili kujiinua kiuchumi na kimaisha kwa ujumla.

Kwa maoni yagu, mojawapo ya sababu kubwa inayofanya watu wengi wafirisike ni pamoja na ukweli kuwa watu hawa wamefanya na wanaendela kufanya kazi kama wafanyabiashara huku wakidhani wao ni wawekezaji. Hali ya namna hii inatulazimu tuone umuhimu wa kufahamu na kutambua maana halisi ya maneno haya (mwekezaji na mfanyabiashara) —“lugha ya pesa”.

Ni muhimu sana ukafahamu tofauti iliyopo kati ya kuwa “mwekezaji” na kuwa “mfanyabiashara”. Unakuwa mwekezaji pale tu unapokuwa tayari kununua na kumiliki viingiza pesa viingiza pesa (mf. majengo, hisa n.k.) kama chombo cha kutiririsha pesa mfukoni mara kwa mara na bila kikomo. Wakati mwekezaji anaamua kununua na kusubili pesa ianze kutiririka mfukoni kwake, mfanyabiashara yeye ananunua kwa bei ya chini, ili auze kwa bei ya juu.

Kwahiyo, unakuwa mfanyabiashara pale unapojua unanunuaje na ni mkakati gani wa jinsi ya kuuza kwa faida. Kwa maneno mengine mwekezaji huwa ni mtu wa kununua na kushikiria. Mfanyabiashara yeye ununua ili kuuza. Kama unataka kuwa tajiri mkubwa, “ni muhimu ukafahamu jinsi watu hawa wawili walivyo tofauti na jisi ya wewe kuwa wote wawili”.

Kwa mfano, ukichukulia biashara ya hisa hapa Tanzania, mara nyingi wengi ununua “hisa” kibiashara na siyo kiuwekezaji. Watu wananunua HISA leo kwa bei ya chini na siku hisa hizo zikipanda bei kwa kiwango cha kuridhisha wengi ukimbilia kuuza kwa lengo la kujipatia faida itokanayo na ongezeko la thamani au bei ya hisa.

Kwahiyo, inatosha kusema kuwa wengi linapofika suala la kununua hisa, tunakuwa “wafanyabiashara” badala ya kuwa “wawekezaji”. Mwekezaji wa kweli katika hisa, mara nyingi huwa hapendi kuuza hisa zake pindi hisa za kampuni yake zinapopanda bei, badala yake uendelea kuongeza hisa, ili kuhakikisha anaendelea kupata gawio kubwa la faida.

Ikiwa wewe ni mfanyabiashara, basi ujue kila kazi utakayofanya utapata faida mara moja, lakini mwekezaji yeye uendelea kupata faida endelevu bila kulazimika kufanya kazi tena. Hii ndiyo maana wafanyabiashara wengi wanapata utajiri wa muda mfupi na baadae wanafirisika. Sababu kubwa ya kufirisika ni kwamba, kila wakati wanaanza upya. Juhudi zinazotumika awali kupata faida hazina uhusiano na faida itakayofuata. Lazima kuweka juhudi na nguvu mpya kila wakati, ili kupata faida nyingine. Mwekezaji yeye anatumia nguvu nyingi mwanzoni sawa na mfanyabiashara, lakini faida anayokuja kupata awamu ya pili na kuendelea anatumia nguvu na muda kidogo sana. Ndiyo maana anapata muda mwingi wa kutengeneza vyanzo vingine vya kuingiza pesa (kipato).

Kwenye uwekezaji ni raha yaani pesa yako inarudi na unabaki na kiingiza-pesa chako. Ukiwa mwekezaji, kitu cha kwanza unataka pesa yako uliyonunulia irudi na wakati huohuo uendelee kumiliki kiingiza-pesa au kitegauchumi.


Ndiyo maana ninapenda sana uwekezaji. Nikiwa kama mwekezaji, ninapata fursa ya kubaki na kile nilichonunua na wakati huo huo pesa yangu niliyotumia kununua inarudi yote. Kwahiyo, kitu ambacho mwekezaji anatakiwa kusema wakati anajipanga kuwekeza ni hiki; “Nataka pesa yangu irudi na kubaki na kiingiza-pesa changu”.

SOMA; Ukweli Kuhusu Mwekezaji ni Huu

Tofauti nyingine ya biashara na uwekezaji ni hii hapa: Mfanyabiashara unaponunua kitu na kukiuza pesa yako ni sawa inarudi, lakini kiingiza-pesa au kitegauchumi unakipoteza. Mwekezaji yeye akinunua kitu, pesa yake inarudi na kiingiza-pesa chake kinabaki kikiedelea kutiririsha pesa zaidi mfukoni.


Kama unaweza kuelewa vizuri kanuni hii ya uwekezaji, basi utaelewa nini maana ya mwendokasi wa pesa. Inamaana unataka pesa yako irudi haraka sana iwezekanavyo, ili itumike kutengeneza au kuanzisha “viingiza-pesa” vingine.


Sasa tofauti ya mwekezaji na mfanyabiashara iko wapi? Watu wengi wanaodhani ni wawekezaji siyo, kimsingi ni wafanyabiashara. Kwa ufupi mwekezaji ununua na kumiliki. Mfanyabiashara yeye ununua ili kuuza tena. Nikikutana na mtu akaniambia kuwa “nilinunua kiwanja au hisa kwasababu najua bei itapanda” Moja kwa moja najua kuwa huyu ni mfanyabiashara fika. Wafanyabiashara wananunua kwa lego moja tu la kuuza kwa bei ya juu zaidi ya pesa waliyonunulia. Ndiyo maana nasema kuwa watu wengi ni wafanyabiashara badala ya wawekezaji.


Mfanyabishara, anataka bei ya kitu chake ipande, ili aweze kuuza kwa faida. Mwekezaji, anataka uwekezaji wake urudishe pesa yake haraka iwezekanavyo na wakati huo huo aendelee kubakia na kile kilichosababisha pesa yake ikarudi haraka (kiingiza-pesa). Mfano halisi ni kama huu; mwekezaji ananunua ng’ombe kwaajili ya maziwa na ndama, lakini mfanyabiashara ananunua ng’ombe kwaajili ya kuchinja.


Kama unataka kufanikiwa katika ulimwengu wa uwekezaji, bila kujali ni kwenye hisa, vipande, biashara, majengo, viwanja, n.k. unahitaji kuwa mwekezaji na mfanyabiashara (kuwa wote wawili). Mwekezaji anafahamu kuchambua, kutathmini mambo yanavyokwenda na jinsi ya kuongoza na kusimamia viingiza-pesa au vitegauchumi. Mfanyabishara anafahamu jinsi na wakati gani wa kununua na kuuza. Mwekezaji mara nyingi anahitaji pesa itiririke kutoka kwenye kiingiza-pesa. Mfanyabishara anataka kupata faida inayotokana kununua bei chini na kuuza bei ya juu.

 
Endapo unataka kuwa mtu mmoja mwenye damu ya mwekezaji na ya mfanyabiashara, jitahidi sana kujifunza kila siku kupitia mtandao wa MAARIFA SHOP. Usitumie taarifa za mitaani na vijiweni kufanya maamuzi ya uwekezaji na biashara bali tengeneza taarifa zako binafsi baada ya kusoma makala mbalimbali hapa MAARIFA SHOP na pia kujisomea vitabu hasa vinavyohusu masuala mazima ya ujasiriamali, uwekezaji na biashara.

No comments: