Monday, September 4, 2017

Unajua ni Kwanini Tunalipa Pesa Kusoma kwa Lazima?


Katika kufikiria kwangu leo nimegundua kuwa kitu kinachoitwa chuo siyo majengo, viti, vitanda, godoro, walimu, nguo, chakula n.k. Vitu vyote vilivyotajwa vinapatikana majumbani mwetu. Lakini cha kushangaza bado tunakwenda chuoni, licha ya kwamba vitu vyote hivi bado vipo majumbani kwetu. Najiuliza ni kwanini tunaambiwa ni lazima
twende chuo? Je? Chuoni kuna nini cha zaidi mpaka tulazimishwe?

Nahisi kuna kitu fulani kipo chuoni ambacho hakipatikani nyumbani. Inaonekana mchakato mzima unaofanya watu wengi kuingia na kukaa chuo chochote duniani si mwingine bali ni “kusoma vitabu”. Msingi na kigezo kikubwa cha wewe kulipa KARO kwenye chuo ni ili chuo kikukubalie kuanza kusoma, maana yake “unalipa kusoma vitabu”.

Kwanini unalipia kusoma vitabu? Kutokana na mfumo wa maisha ulivyo ni kana kwamba watu wengi hawana nidhamu ya kutosha kuweza kusoma vitabu wao wenyewe—mpaka awepo mtu wa kuwasimamia ndipo waweze kusoma. Kwahiyo, lazima umlipe mtu (chuo), ili akuhimize au ikibidi akulazimishe wewe kwenda maktaba kusoma vitabu na hicho ndicho kinaitwa “CHUO”.

Yote haya yanadhihirisha kuwa, vitabu ni vitu muhimu sana kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii, ndiyo maana wengi wetu tuko tayari kukopa pesa, ili tulipe chuo kitakachotulazimisha kusoma vitabu.

Ukweli ni kwamba mtu anazaliwa akiwa hajui vitu vingi, lakini taratibu taratibu anajifunza kadiri anavyozidi kukua. Zipo njia nyingi za kupata maarifa mbalimbali, lakini kubwa kabisa nikupitia VITABU. Unaposoma vitabu ukiwa chuoni unazidi kupata nguvu ya fikra. Kwenda chuo, maana yake ni kwenda kupata mawazo mapya.

Baada ya kupata mawazo mapya, chuo kinakuthibitisha endapo utakuwa umepata kiwango fulani cha maarifa au mawazo mazuri. Uthibitisho wa chuo kuwa na wewe ni mtu mwenye maarifa fulani, ambayo kimsingi yametoka vitabuni ndio unaitwa CHETI, DIPLOMA, SHAHADA. Kwahiyo, ndiyo kusema kuwa maarifa yanayotambulika rasimi ni yale yaliyoandikwa vitabuni nje ya hapo inabakia kuwa hisia tu. Hii ndiyo sababu unalazimika kuilipa taasisi ili ikushinikize kusoma vitabu, kwasababu bila kufanya hivyo hutasoma vitabu, matokeo yake utakasa maarifa ya kupambana na mazingira yako.

Kwahiyo, kwenye vitabu kuna nini?
Kitu kikubwa kinachopatikana kwenye vitabu ni maarifa, mawazo mazuri na suruhisho kwa changamoto mbalimbali zilizoko kwenye jamii. Mawazo bora yanajengwa kwa kusoma na kisha kuandika vitabu. Vitabu vinakufanya uongee hata baada ya wewe kwenda kaburini. Vitabu vinaongeza uwezo wako wa kuinua kiwango cha maisha ya watu wengine.

Kuna ulazima gani wa kusoma vitabu baada ya maisha ya chuo?
Vitabu vingi tulivyosoma chuoni, tulisoma kwa lazima, hutukusoma kwa utashi wetu kwasababu, lengo lake lilikuwa moja tu nalo ni kufaulu mtihani, nje ya hapo havina manufaa tena kwetu. Changamoto ya vitabu vya chuoni ni kwamba unapangiwa usome vitabu gani, haijalishi vina manufaa au havina manufaa kwako, ilimradi tu nia na madhumuni ya serikali husika yanatimia. 

Serikali nyingi duniani zimeweka utaratibu wa kuandaa watu wake ambao watatoa huduma mbalimbali za kitaaluma. Kwa huduma za kitaaluma, serikali husika inakuchagulia vitabu utakavyosoma kulingana na fani unayotaka kusomea. Kwahiyo, inabidi usome vitabu vya aina moja inayoendana na fani uliyochagua kusomea.

Ukweli ni kwamba tunapomaliza chuo, kazi yetu ni moja tu “kutafuta mafanikio kimaisha”, hasa mafanikio ya kiuchumi, kwasababu suala la ukuaji wa uchumi wa mtu binafsi ndio una uwezo wa kugusa pande zote za maendeleo ya binadamu. Kufanikiwa kiuchumi na kijamii kunahitaji watu wengi wawe na akiri ya kuona fursa ndani ya matatizo yanayoikabili jamii wanayoishi.

Ili tuweze kuwa na akiri, tunahitaji kuwa na utashi wa kushibisha bongo (akiri) zetu, kwasababu, ubongo wetu ukishiba vingine vinakuja vyenyewe. Ubongo wako unashiba siyo kwa kula chakula tu bali ni kwa kusoma vitabu unavyovipenda. Tunasema ubongo wetu unashibishwa na vitabu, kutokana na ukweli kwamba siri za mafanikio ya kila aina hapa duniani zipo ndani ya vitabu.

Ukitaka kukua kiimani lazima usome vitabu kama Biblia, Kuruani na vitabu vingine vya dini; Ukitaka kuimarisha ndoa na kulea watoto wako vizuri ni lazima usome vitabu vya mahusiano, lishe bora n.k. Ukitaka kutajirika, kuwekeza, kuwa jasiri wa kufanya maamuzi sahihi, lazima usome vitabu. Matatizo na changamoto nyingi tunazopitia kwasasa, kuna watu waliozipitia huko nyuma na wameweka wazi suruhisho zake kwa maandishi—yaani vitabuni. Maisha ni marudio, hivyo ukiwa unasoma vitabu vya watu mbalimbali, unagundua siri nyingi za kutatua changamoto zinazokukabili wewe na jamii.

Ukitoka chuoni, usiingie maisha ya uraiani kichwa kichwa, tafuta waliopita unapotaka kupita, waliwezaje au walifanyaje, yote hayo wameandika. Ukitoka chuoni na ukapuuzia kusoma vitabu utaishia kulalamika kila siku bila kupata suruhisho kwa matatizo uliyonayo sasa.

Siri zote zimo vitabuni, usiposoma nafasi yako ya kuhangaika zaidi ni kubwa sana. Kwahiyo, hapa kikubwa ni kuanza mpango wa elimu binafsi—ambayo ndiyo maisha halisi baada ya chuo.

Lazima usome vitabu bila kulazimishwa, na kwa kufanya hivyo utaweza kupata umahili mkubwa wa kupambana na changamoto zinazokukabili wewe na jamii kwa ujumla. Pia, kusoma kutawezesha ubongo wako kuwa na uwezo wa kuona fursa pale ambapo wengine hawawezi kuona.

Mwisho ni kwa wale wote ambao wangependa kusoma vitabu, ninavyo vitabu vingi sana lakini leo nitakushirikisha kitabu kimoja cha “THE MASTERY OF DESTINY” By James Allen. Kama ungependa kupata nakala tete (softy copy) ya kitabu hiki bonyeza neno hili la KITABU na kisha ujaze email yako. Baada ya hapo nitakutumia nakala hiyo. Pia, endapo utapenda kupata vitabu vingine niambie unapendelea mada gani ili nikutafutie vitabu husika.
  

No comments: