Saturday, September 9, 2017

Umezaliwa Leo Kama Mimi Unafikiri Tutashinda Mchezo wa Maisha ya Pesa Lini?



Leo tarehe 9/9/2017 ni siku yangu ya kuzaliwa ambapo nimetimiza umri wa miaka 45 tangu nilipozaliwa. Baada ya siku ya leo, nitaanza safari yangu ya mwaka wa 46, nikiwa mwenye furaha hasa ninapoona kufikia hadi siku ya leo niko hai. Wakati huo huo, nazidi kuyalinganisha maisha yangu kama “mchezo wa mpira”. Maisha ni
kama mchezo wa kubahatisha, unaweza kufaulu au kushindwa. Kila siku tunakutana na changamoto ambazo zinaweza kutupelekea kuwa washindi au tukapoteza. 

Kujifunza masuala ya pesa kunaweza kukuza uwezo wako wa kushinda mchezo wa maisha. Leo hii nayaangalia maisha yangu kwa jicho la maisha ya pesa. Hapa naugawa umri wangu katika vipindi vinne vya miaka kumi kumi. Nikitizama vipindi vyote vinne, najiuliza swali gumu ambalo ni; “Kipindi kipi nitashinda mchezo wa pesa kwa kuutandika umaskini magoli matatu bila?”

Katika hali ya kawaida, watu wengi uanza kufanyakazi za kujitegemea wanapofikisha umri wa miaka 25 ya kuzaliwa na kustaafu pindi wanapofikisha miaka 65 (ingawa walioajiriwa serikalini-TZ, ustaafu pindi wanapofikisha umri wa miaka 60). Siku ya leo nasherekea siku yangu ya kuzaliwa kwa kutazama kile ambacho kimefanyika ndani ya vipindi vya miaka kumi kumi kuanzia mwaka 1997, nilipokuwa na umri wa miaka 25.

Miaka 25-35 (1997-2007): Katika kipindi hiki niliweza kufanya mambo mazuri mengi ikiwa ni pamoja kusoma chuo kikuu cha Makerere, Kampala-Uganda, ambapo nilitunukiwa shahada ya kwanza—sayansi ya kilimo (BSc. Agriculture). Ndani ya kipindi hiki pia niliweza kuoa na hivyo kuongoza familia ya watu 4; Nilipata ajira na pia nilijiendeleza kitaaluma kwa kusoma kozi fupi fupi hasa katika masuala ya Utafiti wa kiuchumi, masoko, biashara, ujasiriamali pamoja na masuala ya ufuatiliaji na tathimini kwa miradi ya maendeleo (Monitoring & Evaluation).

Miaka 35-45 (2007-2017): Ndani ya kipindi hiki ambacho kinakwisha leo 09/09/2017, nimeweza kufanya mambo makubwa pia. Nimeweza kuongeza elimu na nimefanikiwa kupata Shahada ya pili Uzamili katika fani ya Uchumi-Kilimo, Biashara na Masoko (MSc. Agricultural Economics) kutoka chuo kikuu cha Sokoine (SUA), Morogoro-Tanzania. Naendelea kuongoza familia ya watu 8; Nimefanya biashara kwa ubia; nimejiendeleza na kubobea katika fani ya ufuatiliaji na tathimini hasa kwa miradi ya kilimo-biashara; Nimeendelea kujisomea na kukuza kipaji changu katika masuala ya uandishi wa makala na vitabu (https://maarifashop.blogspot.com); Nimeweza kujisomea takribani vitabu 40 vinavyohusu pesa, uwekezaji, na jinsi ya kupata na kumiliki mali nyingi, vitabu vyote hivi vimeniwezesha kukuza akiri na fikra juu ya utafutaji na umiliki wa pesa (financial IQ); Nimeweza kutoa mafunzo mbalimbali kwa makundi tofauti tofauti ya jamii— masuala yote yanayohusu pesa, uongozi, biashara, uwekezaji na ujasiriamali.

Miaka 45-55 (2017-2027): Hiki ni kipindi ambacho nitakianza rasimi kuanzia siku ya kesho tarehe 10/09/2017 hadi 09/09/2027. Nikipindi muhimu sana kwangu; ni kipindi ambacho natarajia kufanya mambo makubwa kwa mpangilio maalum; ni kipindi ambacho ninaingia nikiwa nimejitambua, tofauti na vipindi vya nyuma ambapo nilikuwa sina mpango maalum. Pia, vipindi vya nyuma hakukuwa na mpango mkakati wa muda mrefu (“the 10-year plan”). Mambo mengi yamefanyika kwa kubahatisha na hivyo kusababisha muda wangu mwingi kupotea katika mambo ambayo siyo ya kuingiza pesa mfukoni.

Yawezekana na wengine mmekuwa mnaishi maisha yasiyo na mpangilio kama mimi. Wengi hatuna utamaduni wa kuwa na mipango ya muda mrefu, kwasababu pengine hatuoni haja ya kufanya hivyo. Mipango yetu mingi haiunganiki, kila mpango unajitegemea na hauna uhusiano lengo letu la muda mrefu. Mambo mengi tunayofanya hayaongozwi na ndoto moja ya muda mrefu (miaka 10). Muda mwingi tunacheza mechi bila mpango maalumu. Kila wakati tunagusagusa hiki na kile yaani tunafanya nusu nusu.

Nilichojifunza kwa miaka 20 (miaka 25-35 na 35-45) Somo kwa wale ambao ndio kwanza wanatarajia kuanza au wameanza kazi ya kujitegemea na kwa sasa wako katika kipindi cha kwanza cha mchezo wa maisha ya pesa (miaka 25—35), kipaumbele kiwe ni kutenga na kuweka akiba kutoka kwa kila pesa inayoingia mfukoni—anza kwa kutenga 10% ya kila kipato unachopata.. Jifunze njia mbalimbali za uwekezaji, ambapo unaweza kuwekeza kipato chako kinachobaki baada ya kuwa umekata 10% ya akiba (soma: Maana ya kujilipa kwanza). Unaweza kuwekeza kwenye hisa, vipande (UTT), hatifungani, viwanja na majumba. Jenga utamaduni wa kusoma vitabu vinavyohusu mambo unayopenda kufanya na zaidi wekeza kwenye elimu juu ya pesa. Pia, wekeza sana kwenye masuala yote yahusuyo afya na lishe, kwasababu ni kipindi ambacho unatakiwa kufanya kazi kwa bidii sana.

Kwa wale wanaoingia kwenye kipindi ambacho mimi nimemaliza (miaka 35-45), ni kuhakikisha unakuwa na mpango maalum juu ya watoto wako; unahitaji kuwa na mfuko wa fedha kwaajili ya dharura kama matibabu n.k. mfuko huu lazima kuwa unatenga pesa kidogo kidogo ili kuhakikisha unakuwa na pesa ambayo itakusaidia wakati unapopatwa na majanga. Kipindi hiki ndiyo muhafaka kuwa na biashara (SOMA; Pesa Inaingia Mfukoni Ukijua Lugha Yake—Fahamu aina zipi za biashara zinakufaa).

Jitahidi makala hii iwe chachu kwako ili hatimaye uwe na mpango mkakati wa miaka kumi ambao utakusaidia sana katika kukupa uwezo wa kuupangia muda majukumu badala ya muda kukupangia wewe cha kufanya. Kwa kipindi cha nyuma muda ndio umekuwa ukinipangia cha kufanya na sasa nimeamua kubadili mfumo wa kucheza mchezo wa pesa. Kuanzia sasa (miaka 45—55), nitajitahidi kadiri ninavyoweza kuupangia muda majukumu ya kufanya ili kufikia ndoto yangu kwa haraka zaidi.

Baada ya kipindi cha miaka 35-45 kuisha nitakuwa katika kipindi cha mapumziko ambacho kwenye mchezo wa mpira wa miguu kinaitwa “Half time”. Kwangu mimi nimeamua kipindi cha mapumziko kiwe ni miezi 3 (septemba—Desemba 2017). Nitatumia kipindi hiki cha mapumziko kuuweka mpango mkakati wa miaka 10 ijayo (2017—2027) katika maandishi. Natoa wito kwa wale wote ambao mngependa kuandaa mipango mikakati yenu ya miaka kumi ijayo, kuweka email zenu kwa kubonyeza neno hili; MALENGO hapo nitaweza kuwatumia vitabu 2 vizuri sana, ambavyo vinafundisha namna nzuri ya kufanya hivyo kwa mafanikio.

No comments: