Monday, September 18, 2017

Fahamu Kwanini Walio na AJIRA Wanastaafu na Walio na KAZI Hawastaafu


Kama ukifika muda mwajiri wako hakuhitaji tena na ukafika muda wale wote uliokuwa ukiwahudumia hawakuhitaji, hawakuthamini, hawakuheshimu, na hawakujali tena maana yake ni nini? Ina maana kwamba....
wakati wako umekwisha na MUDA wako wa kuwatumikia ukiwa kwenye nafasi hiyo umekwisha— “ume-expire”. Kustaafu ni sawa na kupitwa na wakati au kuisha muda wako. Tunaposema kustaafu ni kupitwa na wakati, yawezekana watu wengi wakajisikia vibaya. Lakini ukweli unabaki pale pale kuwa wewe ulikuwa na uwezo wa kutoa thamani fulani kwa watu wakati huo ukingali bado kwenye nafasi yako ya ajira, na siyo nje ya hapo.

Ewe mtanzania ukiambiwa umepitwa na wakati usivunjike moyo, kwasababu ni kwenye ajira tu ndipo kuna suala hili la eti watu kustaafu. Kwenye ajira kuna umri wa kustaafu, kwasababu muda huo ukifika, wanadhani huwezi tena kutumwa kwa kukimbizwa kimbizwa. Ukifikia muda huo wa kustaafu, inaanza kuwa vigumu kwako kupokea maagizo na amri kutoka kwa wakubwa zako ambao wengi unakuwa unawazidi sana umri—wengine unakuta ni wajukuu zako.

Ukweli halisi wa dhana nzima ya kustaafu siyo kufikisha umri wa miaka 60, bali ni pale unapoacha kutumwa, unapoacha kuambiwa cha kufanya, unapoacha kupangiwa siku za kufanya kazi na muda wakufanya kazi, unapoacha kupangiwa watu wakufanyanao kazi n.k.

Ni vyema kila mwajiriwa akalielewa vizuri suala zima la “kustaafu ajira”. Dhana ya kustaafu ipo zaidi kwa watu waliojiriwa na haipo kabisa kwa watu walio na kazi. Ajira ni kitu tofauti na kazi. Ajira ni kazi ambayo unapewa na mtu mwingine kwa makubaliano maalum na inakuwa na ukomo. Ndiyo maana ukifika muda ule wa ukomo wa makubaliano, inabidi ustaafu. Kazi ni kile unachofanya mwenyewe kwa utashi wako na siku zote unafanya bila kulipwa chochote. Kwahiyo, kwenye KAZI hakuna kitu kinachoitwa kustaafu.

Watu wengi wanaostaafu ajira, tayari wanakuwa na mawazo potofu kuwa wao hawahitajiki tena, hawathaminiwi tena n.k. Ndiyo maana wengi wao miaka michache baadae tangu watoke kwenye ajira wana-expire kwelikweli.

Kama unakaribia kustaafu au umestaafu ajira, ni vyema ukafahamu kuwa, mtu pekee ambaye hakuhitaji tena ni yule tu mwajiri wako—yule uliyekuwa ukimtumikia. Watu wengine waliobaki (huku uraiani) wanachosubili ni wewe kuwapa suruhisho ya changamoto zao ili nawao wakupe pesa.

Endapo umestaafu ajira na bado ukaendelea kujitahidi kuzalisha thamani au kitu chochote chenye uwezo wa kukidhi mahitaji ya waliowengi, nakuhakikishia watu wengi watazidi kukuheshimu, kukuthamini, kukutukuza, kukujali zaidi hata ya wakati ule ulipokuwa bado kwenye ajira.

Lazima “kuanzia sasa tuanze kujiondoa kwenye kustaafu na tufikirie ni lini tutaacha kutumwa”. Watu wengi wanapokaribia kustaafu, wanapata hofu sana. Pengine kinacholeta hofu ni “hisia ya kupitwa na wakati” ambapo wengi wanawaza kuingia katika kipindi kigumu ambacho wanadhani watakuwa hawathaminiwi wala kuheshimiwa. Ukweli ni kwamba, baada ya wewe kustaafu ajira, inawezekana idadi ya watu wanaokujali, kuheshimu na kukuthamini ikaongezeka maradufu endapo utaendelea kuzalisha thamani kwaajili ya watu wengine.

Siku moja nilikuwa nikifuatilia kipindi cha “Economic Club of Washington DC”, na hapa alikuwa anahojiwa Mh. Donald Trump juu ya siri ya mafanikio yake aliyoyapata kupitia biashara ya majumba na viwanja. Katika mazungumzo yake Donald Trump alisema kitu kimoja ambacho nilikipenda sana; alisema kuwa “watu wengi wanaojishughulisha na biashara ya viwanja na majumba ni wazee”, akimaanisha kwamba ukiwa kwenye biashara ya majumba hakuna kustaafu. Nilipotafakari kauli hiyo ya Trump, niligundua kuwa biashara ya majumba ni moja ya biashara nzuri sana ambayo inafanywa na watu wanaoipenda. Pia, watu wanaofanya biashara hii hawatumwi na mtu yeyote kuifanya bali wanafanya kwa utashi wao.

Kauli ya Donald Trump inatufundisha kwamba, huwezi kuacha kufanya kitu ambacho unakipenda na una utashi wa kukifanya. Kwa maneno mengine ni kwamba huwezi kustaafu kazi unayoipenda. Watu wengi wanaopenda kustaafu ni wale wenye ajira, LAKINI wenye kazi hawapendi kustaafu na hawawezi kufanya hivyo hata siku moja, kwasababu kazi wanazofanya hawakupangiwa na mtu yeyote.

Dhana ya KUSTAAFU imehasisiwa na kukolezwa na waajiri pamoja na waajiriwa. Kuanzia tangu unaanza kutumikia ajira unawaza kustaafu. Hivi inawezekanaje mtu unapenda kazi unayofanya halafu ukaiacha? Wakati mwingine yawezekana ukawa bado unaipenda lakini ukalazimika kuicha kwa mujibu wa sheria. Unalazimika kuiacha kutokana na ukweli kwamba kazi hiyo uliyoifanya kwa muda wa miaka mingi “SIYO YAKO”.

Habari mbaya kwa wote wenye ajira ni kwamba pamoja na mapenzi yote uliyonayo kwa ajira yako, lazima ujue kuwa kazi ya ajira “siyo yako”.

Kama kustaafu kwenye ajira kunakukwaza, usihofu hata kidogo kwani bado unayo nafasi ya kujiwekea mazingira ya kutostaafu. Inawezekana kabisa ukaamua kutostaafu endapo utaamua kuwa na KAZI badala ya AJIRA. Kwa binadamu kitu cha kwanza tulichopewa na Mungu ni KAZI, japo kuwa wengi tunaacha KAZI kutafuta AJIRA.
 
Tunaposema kupewa kazi na Mungu, hatumaanishi hiyo ajira uliyopata kwa kuwasilisha vyeti vyako vya taaruma. Kazi tunayomaanisha ni kile kipaji chako au ule uwezo wako wa akiri wa kubadilisha mawazo yaliyoko akirini mwako kuwa suruhisho ya changamoto zilizoko kwenye jamii—hiyo ndiyo KAZI tunayomaanisha.

Hebu jiulize pamoja na ajira uliyonayo kwasasa ni kazi gani unafanya kutatua tatizo mojawapo kwenye jamii? Kumbuka kuwa kila tatizo hapa duniani ni biashara. Kwahiyo usiwe na hofu kuwa endapo nitatumia muda wangu kutatua matatizo ya watu wengine nitakula wapi nitapata pesa wapi. Watu waliopata suruhisho lako watakuletea pesa ili uwape suruhisho lako—hivyo ndivyo utajiri unavyokuja.
 
Ukiwa na KAZI kustaafu ni kashifa, kwasababu ni kupitwa na wakati—lakini kustaafu kwenye AJIRA ni ushindi, kwasababu ndiyo siku unapoacha kutumwa kazi kwa shuruti.

Endelea kujifunza mengi kupitia MAARIFASHOP, ili kuweza kupata Makala mpya kila zinapotoka weka e-mail yako kwa kubonyeza neno: neno hili; MAKALA

No comments: