Monday, September 25, 2017

Kama Unaamini Pesa ni Sabuni ya Roho Soma Hapa


Ukweli ni kwamba watu wakipata pesa wanakuwa na furaha sana, kiasi kwamba ukikutana nao unaweza ukadhani ni watu wazuri sana, wanajali sana watu wengine, wana upendo kwa kila mtu. Kumbe yote mabaya yao mengi yanajificha ndani ya furaha itokanayo na kupata pesa. Kutokana na watu kuwa wachangamfu pindi wapatapo pesa, jamii yetu ya kitanzania ina msemo usemao..
“pesa ni sabuni ya roho”.  

Fikra ya “pesa ni sabuni ya roho” ndiyo imechangia kwa kiasi kikubwa watu wengi kushindwa kupata uhuru wa pesa. Fikra za kuiona pesa kama sabuni ya kusafisha uchafu ulioko rohoni mwako, ndiyo kisababishi kikubwa cha wewe kukosa nidhamu binafsi ya pesa. Sababu ya msingi kwanini watu wazima wengi tuna matatizo ya pesa, siyo kwasababu tunapata pesa kidogo, bali sababu kubwa ni ukosefu wa nidhamu binafsi na kutokuwa na uthubutu wa kuweza kuchelewesha furaha kwa muda fulani.

Lakini fikra ya “pesa ni sabuni ya roho” imetokana na imani ambayo imejengeka tangu tukiwa watoto wadogo. Ulipokuwa mtoto na ukapewa pesa (zawadi, posho n.k), kitu cha kwanza ulichofikiria kufanya ilikuwa ni kununua vitu vitamu kama pipi na peremende; nakumbuka enzi hizo peremende kwa lugha ya Kinyambo ilikuwa inaitwa “e’kerementi”. Pipi au peremende ni vitu vitamu sana ambavyo tulivipenda tulipokuwa wadogo, na pengine ilikuwa ni nadra kupata za kutosha. Nadhani utakubaliana na mimi kuwa watoto wengi wanakula pipi mpaka wanaugua meno, kwasababu ni tamu sana.

Kutokana na utamu huu wa pipi, kisaikolojia tulijenga tabia ya kupokea pesa kutoka chanzo chochote kile, hasa kutoka kwa wazazi na ndugu na kisha kununua vitu vitamu. Sasa tumekuwa wakubwa na tunawajibika kujitafutia pesa. Utamu ule wa pipi bado unatuandama hadi leo. Ndiyo maana pamoja na kwamba sisi ni watu wazima, unashangaa pindi unapopata pesa, kifikra unatokwa mate na unawaza kuitumia kwa kununua vitu ambavyo vinakufurahisha japo muda mfupi.

Usemi wa “pesa ni sabuni ya roho” unaonyesha watu wana picha ya namna gani kuhusu pesa. Kwa maana nyingine ni kwamba watu wengi tunalinganisha FURAHA na PESA tuliyonayo. Watu wengi wakishapata pesa unaona kuwa wanachangamka na mara moja tu wanabadili hata mtindo wao wa maisha ya kawaida. Kwa watu waliowengi kupata pesa kunaambatana na sherehe. Kwahiyo, wanahusisha furaha yao na pesa waliyonayo mfukoni. Maana yake ni kwamba, mtu akiwa hana pesa mfukoni anakuwa hana furaha kabisa; ikiwa unazo pesa kidogo unakuwa na furaha kidogo; na ikiwa mtu anazo pesa nyingi mfukoni, furaha inakuwa ni kubwa—ndiyo maana sherehe ni nyingi wiki ya mwisho wa mwezi.

Kutumia pesa kunakufanya uwe mwenye furaha. Unapokuwa mtu mzima na ukapata au ukapokea pesa, hisia hizi za kuwa na furaha pindi upatapo pesa zinaendelea. Kila unapopata pesa, fikra yako ya kwanza ni “namna gani nitatumia pesa hii kupata furaha ya haraka? Unapoajiriwa kwa mara ya kwanza, kitu cha kwanza unachofikiria ni namna gani utatumia pesa ya mshahara hasa ule wa kwanza; yawezekana ukawa ni kwaajiri ya kununua nguo, magari, vipodozi, kuchangia harusi, kusafiri na mengine mengi.

Wewe unayesoma makala hii utakuwa ni shahidi juu ya mikopo mingi inayotolewa na baadhi ya makampuni, mabenki na hata mifuko ya hifadhi ya jamii hasa kwa waajiriwa wapya eti! Kwa lengo la kuwawezesha kununua samani (furniture) za ndani, wengine wanaita mkopo wa kuanzia maisha—japokuwa maisha yalishaanza.

Watoa mikopo hiyo, tayari wamekwishafanya utafiti na wanajua wewe kama mwajiriwa mpya unayo kiu ya kutumia pesa bila kujali chanzo chake. Wanajua pia kuwa wewe kama mwajiriwa mpya huna huwezo wa kuchelewesha furaha ipatikanayo pindi unapopewa pesa ya siku 14 na mwajiri kwaajiri ya kujikimu, wanajua tu lazima utawashwawashwa kununua samani za ndani ya nyumba. Yote haya yanatokea kwasababu, tangu zamani hatukujengewa tabia ya kukaa na kuishi na pesa kama tunavyoweza kukaa na vitu vingine, matokeo yake ni kwamba mara unapopata pesa tu! inakuwa vigumu kudhibiti mihemuko itokanayo na pesa iliyo mfukoni mwako.

Tabia ya kupata pesa na kununua pipi inaendelea hadi unapokuwa mkubwa, kiasi cha fikra zako kunasoma hivi: “PESA = FURAHA” au “PESA = SABUNI YA ROHO”. Kwahiyo, kama tayari una mtazamo huo, inamaana kuwa tayari umejenga tabia ya kulinganisha furaha na utumiaji wa pesa. Jinsi unavyokuwa na furaha ndivyo unajikuta bila kujua unalazimika kwenda kutumia pesa kununua chochote kile kilichoko machoni mwako. Wengi wanahusisha furaha na kununua chochote. Ikitokea kile walichotarajia kununua hakipo, basi watanunua chochote kile.

Ikiwa wewe ni mtu mwenye kuhusisha pesa na furaha, basi ujue kuwa kila utakapopata pesa haijalishi ni mshahara au mkopo, moja kwa moja, akiri yako itakutuma kwenye mipango ya kuitumia—na hapa ni kununua vitu ambavyo unapata furaha. Katika kutumia pesa hatuwazi tena kama matumizi yetu ni kwa vitu ambavyo vinazaa pesa au vinameza pesa japo kuwa matumizi yetu kwa sisi ambao pesa ni sabuni ya roho, huwa ni kwa vitu vinavyomeza pesa—ikitoka imetoka hairudi tena.

Furaha yako inapanda kadiri unavyotumia pesa. Pesa inapoisha tu na furaha yetu nayo inaisha kwa kiwango kile kile—pesa ikiisha roho zetu zinachafuka. Na tunazisafisha kwa kutafuta pesa (sabuni) popote pale, hata kama ni kukopa. Kwahiyo, maisha yetu siku zote yanatawaliwa na utafutaji wa pesa (sabuni), kwaajili ya kusafisha roho zetu. Tukipata pesa kidogo (sabuni), tunapumzika kwanza ili kupunguza uchafu rohoni, sabuni ikiisha wakati uchafu bado upo, tunaendelea kutafuta sabuni nyingine—utaratibu huu wa maisha hautufai tunahitaji kubadilika.

Kwa maisha haya hatuwezi kupata furaha ya muda mrefu, hadi hapo tutakapoacha kuhusisha pesa na furaha. Lakini pia mpaka pale tutakapojifunza kuchelewesha furaha hizi za muda mfupi—yaani kujizuia kupata furaha kwa maksudi ya kujijengea uwezo wa kufurahi siku za baadae kwa muda mrefu. Fikra ya “pesa ni sabuni ya roho” lazima twende nayo kwa tahadhari, kwasababu bila kufanya hivyo inatupoteza kiasi cha kushindwa kuichukulia pesa kama mbegu au nyenzo ya kuzalisha mali na pesa zingine.

Hakika tunahitaji kubadili fikra juu ya pesa na kuachana na dhana nzima ya “pesa ni sabuni ya roho. Wakati umefika sasa wa kuacha kuhusisha furaha yako na pesa. Ili kuachana na tabia hii, inabidi kuanzia sasa utambue na uanze kuichukulia pesa yako kama mbegu iliyo na uwezo wa kuzaa na kuongezeka. Ni muhimu kuanzia sasa tuache kuichukulia pesa kama mapato au hitimisho. Tukipata pesa tusishangilie badala yake tushangilie na kufurahi, pale tunapoiwekeza pesa yetu kwenye
VIINGIZA-PESA".

Tukishangilia na kufurahi baada ya kuwekeza pesa na tukaacha kufanya hivyo tunapopata pesa, hapo tutakuwa tumepiga hatua na tutaanza kufanana na watu waliofanikiwa au matajiri. Watu waliofanikiwa wanapopata pesa hawaichukulii kama mapato badala yake wanaichukulia kama nyenzo ya kuzalisha pesa na mali nyingine. Furaha yao ni kuona pesa na mali nyingi zaidi ya ile waliyokuwanayo hapo awali. Wanatumia pesa kuanzisha vyanzo vingine vya pesa na hivyo kujiepusha na utegemezi wa chanzo kimoja cha pesa.

Endelea kujifunza mengi kupitia neno hili; MAARIFA SHOP, ili kuweza kupata makala mpya kila zinapotoka weka e-mail yako kwa kubonyeza neno hili: MAKALA.

No comments: