Sunday, September 9, 2018

Umezaliwa Leo Kama Mimi Unahitaji Kuingia Hapa “Kujaribu House”

HAPPY BIRTH DAY TO ME

"Ukijaribu na Kushindwa Mara Nyingi Sana Kinachobaki ni Kufanikiwa" ~ Cypridion Mushongi
Leo (09/09/2018) ni siku yangu ya kuzaliwa. Siku hii ni muhimu sana kwangu kutokana na ukweli kwamba inanipa fursa ya kujitathimini mwenendo wa maisha yangu na familia yangu LAKINI pia napata kutathimini mchango wangu kwenye jamii. Tangu mwaka 2016 nilianza utaratibu wa kuadhimisha siku yangu ya kuzaliwa kwa kuandika makala maalumu kuhusu mambo mbalimbali. 

Mwaka 2016 tarehe kama ya leo, niliandika juu ya tofauti ya KUKUA na..
KUZEEKA (SOMA; Miaka 45 ya Kuzaliwa Tumezeeka au Tumekua?). Kwamba kuzeeka ni lazima LAKINI kukua ni wajibu na ni hiyari ya kila mmoja. Maana yake unaweza ukaamua kukua au ukaacha. Tangu hapo, mimi nilichagua kukua kwa gharama yoyote na matokeo ya ukuaji huo, mwaka jana (2017), niliweza kugundua kuwa maisha ya pesa ni kama mchezo wa mpira (SOMA; Umezaliwa Leo Kama Mimi Unafikiri Tutashinda Mchezo wa Maisha ya Pesa Lini?). 

Kwamba maisha yetu ya pesa, kama ulivyo mchezo wa mpira tunacheza nayo kwa muda wa miaka 40. Kipindi cha kwanza ni miaka 20 (umri kati ya miaka 25-35 na 35-45) na kipindi cha pili ni miaka 20 (umri kati ya miaka 45-55 na 55-65). Kwa maana hiyo, leo ninaposherekea kutimiza umri wa miaka 46 ya kuzaliwa na kuanza safari yangu ya 47, ni wazi kwamba, tayari nipo katika kipindi cha pili cha mchezo pesa. Nipo katika kipindi hiki nikicheza mechi kwa juhudi kubwa na maarifa mengi. Malengo, nia na madhumuni yangu, ni kushinda mechi zote zilizobaki dhidi ya umaskini. 

Leo ikiwa ni mwaka mmoja tangu nianze kipindi cha pili cha mchezo wa pesa, tayari nimegundua na kujifunza kuwa unaposhindwa mara nyingi, inafika muda fulani kushindwa kunaisha, na unabakia na kufanikiwa tu! Naona kadiri muda unavyokwenda idadi ya kushindwa inaanza kupungua taratibu — kitu cha msingi nikuwa mtulivu na mvumilivu. 

Pia nimejifunza kwamba, katika jamii yetu, kumejengeka hofu na woga mwingi juu ya kushindwa. Kutokana na woga huo, wengi wameamua kutothubutu kufanya chochote, ili kukwepa hatari ya kushindwa, japokuwa wanatamani kufanikiwa! Wachache wanaothubutu na kujaribu, pindi wanapokutana na kushindwa mbele ya safari, mara nyingi wamekuwa wakikata tamaa na kuishia hapo hapo, huku wakiyarudia maisha yale waliyokuwa wakiishi hapo awali. 

Ukifuatilia kwa umakini, utashangaa kuona kwamba, watu wengi waliofanikiwa ni wale walioshindwa mara nyingi. Pengine, hili linatokana na ukweli kwamba, jambo la “kushindwa” au “kufanikiwa” ni matokeo ya kujaribu au kuchukua hatua dhidi ya jambo fulani. Kwa maana nyingine, tunajifunza kwamba, “kushindwa” na “kufanikiwa” vyote viko kwenye nyumba moja na nyumba hii tunaweza kuiita Kujaribu House

Kwa mtu yeyote anayetembelea Kujaribu House, lazima akutane na watu wawili ambao ni “Kufanikiwa” na “Kushindwa”, kwani wote uishi na kukaa nyumba moja. Kwa maneno mengine ni kwamba, ikiwa utakuwa na uhitaji wa mmoja wapo, lazima ujiandae kukutana na wote wawili. Uzoefu wangu unaonyesha kuwa, mara nyingi huwa ukifungua mlango wa nyumba hiyo ya Kujaribu House, mtu wa kwanza kukutana naye huwa ni yule anayeitwa kushindwa. 

Endapo, ukimuogopa ukatoka nje ya nyumba hiyo na kukimbia, huyo “Kushindwa” yeye atakachofanya haraka haraka ni kufunga mlango wa nyumba yao. Mlango ukifungwa maana yake hutaweza kumuona wala kumpata “Kufanikiwa”, na kama itaonekana bado unamuhitaji “Kufanikiwa” itabidi urudi tena kwenye nyumba hiyo—Kujaribu House. Ukishaingia kwenye nyumba hiyo, usitoke na wala usiogope vitisho na maumivu ya “Kushindwa” badala yake endelea kujifunza namna nzuri ya kuishinaye huku ukifanya jitihada za kumpata yule “Kufanikiwa” umpendaye. 

Lazima ujifunze kuvumilia kushindwa na ujitahidi kugeuza kushindwa kuwa ubao wako wa kujifunza njia na mbinu bora za kukuwezesha kufanikiwa. Uzoefu wangu kwasasa unanifanya kuamini kuwa, idadi ya kushindwa inaesabika, nikimaanisha kwamba, unashindwa mara nyingi hadi ile idadi ya kushindwa inapungua na baadae inaisha kabisa na mwisho wake unabakia na kufanikiwa tu! Ndiyo maana, watu waliofanikiwa wanazidi kutuasa na kutusihi kuwa “wavumilivu” pale tunapoanza mchakato wa kutafuta mafanikio ya ndoto zetu. Kwamba lazima tujipe muda, huku tukiendelea kujaribu mara nyingi hadi idadi ya kushindwa iishe na kwamba Ukijaribu na ukishindwa mara nyingi sana kinachobaki ni Kufanikiwa”

Kumbuka kuwa mafanikio hayatakuja hivi hivi, lazima yaambatane na kujaribu mara nyingi na kushindwa mara nyingi. Ukweli ni kwamba ukishindwa mara nyingi mbele ya safari unabaini mbinu na njia ambazo hazifai na wakati huo huo unagundua mbinu na njia mpya zinazofaa kukupatia mafanikio unayoyataka. 

Mpendwa msomaji wa Makala hii, jitahidi kuingia na endelea kuishi na kukaa nyumba hii ya Kujaribu House usithubutu kutoka kaa humo mpaka umpate “Kufanikiwa”. Nasisitiza neema na baraka zote zinapatika Kujaribu House

Mwisho, napenda kuwataarifu watembeleaji wote wa mtandao wa MAARIFA SHOP; hasa mnaoishi Dar-Es-Salaam kuwa leo nimesherekea siku yangu ya kuzaliwa nikiwa jijini Dar-Es-Salaam, kwahiyo, kwa wale wote ambao watapenda kuonana na mimi ana kwa ana, wanipigie simu kupitia namba 0788855409; kuanzia saa 9 alasiri hii hadi 3 usiku. 

Kupata mafunzo kila siku kwa njia ya whasap bonyeza neno MAFUNZO

KARIBU TUONGEZE MAARIFA PAMOJA. 


No comments: