Tajiri mkubwa na mashuhuri duniani, Bwana Warren Buffet aliwahi kusisitiza kuwa, kama unataka kujenga mtaji kutoka kwenye akiba yako binafsi ni sharti ujitahidi kuacha tabia ya “kuweka akiba baada ya kutumia na badala yake utumie kile kinachobaki baada ya kutenga pesa ya akiba”.
Katika maisha ya umilikaji pesa duniani, kuna makundi ya aina mbili......
Kundi la Kwanza ni la wale wanaoweka akiba ya kile kinachobaki baada ya wao kutumia na kundi la pili ni wale wanaoweka akiba kabla ya kutumia. Kwa mfumo wetu wa mapato na matumizi ya pesa, tunaona kuwa kundi la waweka akiba baada ya kutumia ni wengi sana na ndilo kundi la watu ambao ni walalamikaji juu ya ukosefu wa mitaji ya kufanyia biashara au shughuli nyingine za kiuchumi.
Katika ulimwengu wa biashara, mtaji ndilo suruhisho la uwekezaji wowote wenye tija. Hatahivyo, mtaji umekuwa ni adimu kuupata na umekuwa ni kikwazo namba moja cha watu wengi kushindwa kuwekeza na hatimaye kuwa wajasiriamali.
Ili kuweza kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa mitaji, watu wengi wamezidi kuhamasishwa kujiweea akiba binafsi kidogo kidogo kutoka kwenye mapato wanayopata.
Lakini pamoja na kwamba njia hii ya akiba binafsi ni rahisi na ya uhakika, bado suala la kuweka akiba limekuwa gumu kutekelezeka. Sababu kubwa ya kushindwa kujiwekea akiba ni kwamba watu wengi tumejenga utamaduni wa “kutumia kwanza na akiba baadae”.
Ukweli ni kwamba, pindi tunapopata pesa, kitu cha kwanza kufanya ni kutumia kwanza kwa lengo la kumaliza eti shida zilizopo. Hapa kipaumbele kinakuwa ni kumaliza shida na siyo kuweka “akiba”.
Uzoefu umeonyesha kuwa, ukipata pesa na ukaanza kutumia kabla ya kutenga akiba, inakuwa siyo rahisi kubakiza pesa yoyote kwasababu shida ni nyingi na mahitaji ya wakati huo ni mengi, ukilinganisha na kiasi cha pesa unachokuwa umepata.
Ukipata pesa na ukatumia kabla ya kutenga akiba, basi ujue umelipa watu wengine kwanza kabla ya kujilipa wewe. Utamaduni wa kulipa watu wengine kwanza pindi tupatapo pesa umezidi kukua siku hadi siku na tumeendela kuulithisha kwa watoto wetu.
Pesa yoyote unayojilipa kwanza ndiyo hiyo hugeuka kuwa “akiba”. Tunahitaji kujenga utamaduni wa kujilipa kwanza kabla ya kufikiria kununua kitu chochote kile pindi tunapoingiza pesa mifukoni mwetu.
Nimeshindwa kujiwekea akiba kwahiyo…. Kwakuwa nimeshindwa kujijengea nidhamu ya kuweka akiba ili hatimaye nipate mtaji, basi nimeamua kwenda kukopa mtaji ili nianzishe biashara yangu. Maeneo ambayo watu wengi ukimbilia ili kupata mikopo ni pamoja na ndugu, jamaa na marafiki; mabenki, n.k.
Hatahivyo, utumiaji wa mikopo kama chanzo cha mitaji, bado haujaweza kuwanufaisha kwa kiwango walichotarajia. Hii ni kutokana na upungufu mkubwa wa elimu juu ya mtiririko wa pesa (inayoingia na kutoka) au uelewa mpana juu ya mapato na matumizi ya pesa.
Kukosekana kwa uelewa wa kutosha juu ya utunzaji na utumiaji wa mikopo, wanufaika wengi wa mikopo, wamejikuta wakigeuka kuwa mawakara wa kudumu wa mabenki ya biashara.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba, mikopo mingi imekuwa ikitumika zaidi kununua vitu ambavyo si vya kuingiza pesa mfukoni "assets", bali vimekuwa ni vitu vya kupeleka pesa nje ya mfuko.
Wapo watu wengi ambao tumeshuhudia wakishindwa kabisa kurudisha mikopo na hapa wakopeshaji wa pesa, wanalazmika kunadi mali zao na hivyo kujikuta wakifirisika ghafla.
Lakini chanzo cha kushindwa kurejesha mikopo kukosekana kwa nidhamu ya matumizi ya pesa ambayo haikujengeka huko nyuma. Bila kuwa na nidhamu na tabia ya kujilipa kwanza kutokana na mapato yako binafsi, huwezi kuwa na nidhamu ya kutumia pesa ya mkopo (ambayo siyo ya kwako) kwa umakini unaostahili.
Kwahiyo, tabia ya kutenga akiba kabla ya kutumia (kulipa watu wengine), ndio inatuwezesha kujenga nidhamu ya matumizi stahiki ya pesa yetu binafsi na hata ile ya mkopo.
Akiba binafsi imeshindikana….! Wengi wetu tunashindwa kabisa kujiwekea akiba binafsi licha ya kwamba tunapata pesa ya kutosha.
Kila wakati tunapopata pesa kitu cha kwanza tunachowazia na kukipa kipaumbele ni “MATUMIZI” yaani kununua mahitaji (kuwalipa wengine) na pesa inayobaki ndiyo mara nyingi watu ukumbuka kujiwekea akiba. Haipiti wiki moja, ile akiba tuliyoweka mwanzoni baada ya kutumia nayo tunaitumia kwa mambo mengi ambayo ufanyika kwa mtindo wa dharura.
Suala la kupenda kutumia haliishii hapo bali watu wengine uenda hatua ya mbele zaidi ambayo ni ya kutumia vitu kwa mkopo ambapo mtu ulipa pesa baadae baada ya kupata pesa.
Unapomkuta mtu yuko busy anatafuta pesa, husidhani mtu huyo anasukumwa na kutaka kutoka kimaisha laasha! Bali huyo mtu anatafuta pesa za kulipia madeni ya vitu alivyokwisha tumia siku za nyuma.
Kwahiyo, itoshekusema kuwa mtu huyo alikula bila kufanya kazi, na adhabu yake ni kwamba matunda yote ya kazi yake, lazima yalipe madeni tu maana hamna namna nyingine.
Unapanga mipango ya kutumia baada ya kupata pesa? Tabia hii ya kutumia kwanza na akiba baadae ndiyo inawafanya watu wengi kuamini kwamba huwezi kupanga mipango yoyote kabla ya kupata pesa.
Watu wa namna hii kwa kipindi ambacho hawana pesa wanakaa tu bila kupanga na kufanya chochote cha maana. Kwa maana nyingine, watu hawa bila kusukumwa na pesa waliyonayo mifukoni hawawezi kufanya jambo lolote la maendeleo. Hii ni hatari na lazima umaskini huwe halali yako.
Iwapo msukumo wako wa kufanya kitu chochote unategemea au kusukumwa na pesa tasilimu uliyonayo mfukoni ni wazi kwamba ikishapatikana, lengo la kuweka akiba kwanza haliwezi kupewa kipaumbele au wakati mwingine haliwezi kufanyika kabisa.
Matokeo yake ni kwamba kila wakati utajikuta hubakizi chochote kwasababu kila mara utakapopata pesa, lazima utaipangia kulipia mahitaji (lipa wengine) alafu itaisha.
Hali hii itakapoendelea na baadae kuwa tabia yako basi uje kuwa kila wakati wewe utakuwa ni mtu wa kukosa nidhamu ya kujiwekea akiba ambayo ndiyo ingezaa mtaji wa kutimiza ndoto zako.
Waliofanikiwa wanaweka akiba kwanza kabla ya yote: Kwakuwa akiba binafsi ndiyo chanzo cha uhakika wa kupata mtaji binfsi, ni lazima tuanze kubadilika kwa kuanza kujifunza tabia ya wale watu waliofanikiwa.
Watu waliofanikiwa, mara nyingi wanapopata pesa yoyote hile, kitu cha kwanza kwao huwa ni kutenga kwanza asilimia fulani ya pesa kama akiba na baada ya hapo ndipo ufikiria suala la matumizi mengine.
Unapoweka akiba kwanza kabla ya kitu chochote ndipo unaweza kudhibiti tamaa yako, kwa maana utatakiwa kuwa na nidhamu ya kutumia kulingana na kile kilichobaki.
Kwahiyo, jijengee tabia ya kutanguliza kujilipa kwanza kabla ya kulipa watu wengine; kwani kwa kufanya hivyo, utapata mtaji wa kutosha na hatimaye kufikia mafanikio makubwa maishani.
Ili kuendelea kupata makala hizi moja kwa moja kupitia e-mail yako bonyeza “TUMA MAKALA” Na kujiunga na kundi la whatsap bonyeza neno MAFUNZO KILA SIKU.
No comments:
Post a Comment