·
Watu wengi wanafikiri
kwa kutumia vitu vilivyopo tu!
·
Picha ya maisha
mazuri haipo kwenye akili ya walio wengi!
Maendeleo yaliyopo kwa sasa yametokana
na mawazo pamoja na picha mbalimbali zilizojengeka ndani ya ubongo wa binadamu.
Vitu vyote tunaviona ambavyo vimetengenezwa na binadamu, vilitokana na mawazo na
taswira/picha zilizoumbwa ndani ya ubongo wa mtu. Baada ya kuumba picha au
taswira ya kile kinachohitajika kufanyika ndipo binadamu huweza kutumia nyenzo
mbalimbali pamoja na malighafi nyinginezo kutengeneza vitu halisi, huku
akiongozwa na ile taswira iliyoko kwenye akili ndani ya ubongo wake.
Nyumba ni mfano mmojawapo wa vitu halisi
ambavyo huanza kama wazo. Leo hii tuna nyumba za kila aina, kwasababu mara
nyingi tuna wasanifu majengo ambao kila mara uanza nyumba kwa kufikiria jinsi
itakavyokuwa hata kama haijajengwa na baadae uchora ramani yake ambayo wajenzi
uitumia katika kusimamisha jengo. Kwahiyo, aina mbalimbali za majumba
tunazoziona leo zilitokana na fikra na ujenzi wa taswira ndani ya ubongo wa
watu hao ambao ni wasanifu majengo (architect). Nyumba ikishakamilika ndipo
watu wengine hupata fursa ya kujua kilichokuwa akilini mwa huyo mtu na pindi watoto
wanapozaliwa na kukua ujenga mawazo na taswira ya kurithi kutokana na vitu
vilivyopo tayari. Kwahiyo, mtoto akikua na kufikia wakati wa kujenga nyumba
yake, moja kwa moja anapata picha ya nyumba kwenye ubongo wake ambayo ni ya
kurithi kutoka kwenye nyumba zilizojengwa tayari. Kwa namna moja au nyingine
ile picha iliyobuniwa kwenye ubongo wa mtu wa kwanza anakuwa ameinakiri kutoka
nyumba halisi na kuijenga mara ya pili.
Katika nchi nyingi ikiwemo Tanzania, ambazo
hazijapiga hatua kubwa kimaendeleo; vitu vingi vinavyofanyika vimetokana na
taswira ya vitu halisi ambavyo tayari vipo na vinaonekana. Imejengeka tabia ya
watu walio wengi kuhoji hasa pale mtu Fulani anapojaribu kuibua jambo jipya,
mara nyingi linakataliwa eti! Kwa kisingizio cha kwamba “halijawahi kufanyika popote”. Kwahiyo, watu wanajisikia amani zaidi
wanapoona wanafanya kitu ambacho tayari kinafanyika kwingine. Hali ya namna hii
ndiyo inaendelea kutufanya tuendelee kuwa wategemezi na ombaoma mbele ya jamii
ya kimataifa. Utamaduni huu wa kuendelea kutumia uzoefu na kuzama kwenye vitu
vilivyoko mbele yetu muda wote (hali halisi), ndio unaotusababishia kuendelea
kupata changamoto, matatizo na uzoefu ule ule miaka nenda rudi!. Mara nyingi
uzoefu na elimu juu ya jambo fulani, ni vitu ambavyo vimejengeka kutokana na mambo
yaliyopita au vitu vya zamani, kiasi kwamba, wewe unachofanya ni kuvikariri na
kuvitoa upya, hali ambayo kiukweli kunakuwa hakuna jipya lolote la kutokea.
Misuli ya kuwaza ndani ya ubongo wetu,
ndiyo hubadilisha mawazo na fikra zetu kuwa vitu kamili. Picha na fikra juu ya
kitu tukitakacho, ndivyo vitu muhimu vinavyohitajika katika kujenga maisha
mazuri ya baadae. Ni kwakutumia picha iliyoumbika ndani ya ubongo wetu, ndipo
tunaweza kuona jinsi tunavyotaka maisha yetu ya baadae yawe. Tukishakuwa
tumeyaona maisha mazuri ndani ya ubongo wetu, ndipo tunaweza kupata hari na
shauku kubwa ya kuyatafuta hayo maisha ya ndoto yetu. Kwahiyo, ni wakati
muhafaka sasa kwa kila mtanzania kujenga tabia ya ubunifu na kuendelea kujikita
katika kufikiri mambo mapya na vitu vingine nje ya hivi vilivyopo. Kila mtu aanze
kwa kutengeneza picha ndani ya ubongo wake juu ya maisha mazuri anayoyatamani
na baadae kuweka mikakati ikifuatiwa na utekelezaji. Iwapo tutaweza kupata
picha ya maisha tuyatakayo na jinsi tunavyopenda yawe, basi nguvu kubwa itakuwa
imewekwa kwenye mwendo na mabadiliko makubwa yakiambatana na maisha mazuri yatatokea bila
pingamizi lolote. Kumbuka kuwa asilimia 80% ya mafanikio yako yataletwa na wewe
mwenyewe na asilimia 20% ndiyo inategemea
watu wengine.
Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO.
Kazi ni kwako! Timiza wajibu wako!