Wednesday, October 12, 2016

Biashara Yako Inakutaka Ufanye Yafuatayo



 "Kila utakapoona biashara iliyofanikiwa ujue kuna mtu alifanya maamuzi ya kijasiri" ~ Peter F. Drucker

Watu wengi tunatamani sana kuwa matajiri, lakini wengi wanakata tamaa. Mojawapo ya njia muhafaka itakayotufikisha kwenye utajiri ni “biashara”. Biashara ni
kundi mojawapo la “viingiza-pesa” mfukoni. Ziko aina nyingi za biashara, ambazo unaweza ukafanya kulingana na chaguo lako.

Biashara siyo lazima iwe ile tuliyozoea yaani “kununua vitu kwa bei ya chini na kuuza kwa bei ya juu” BALI ni zaidi ya hapo. Hapa ninamaanisha kuwa “biashara” ni hali yoyote ile ambayo unaweza ukaunganisha nguvu, nyenzo na vitu mbalimbali, kutengeneza mfumo wa uzalishaji wa bidhaa au huduma mbalimbali. Mwisho wa siku, mfumo huu wa uzalishaji ndio ambao uvuta au kutiririsha pesa nyingi kuingia mfukoni mwako. Mara nyingi pesa hii ambayo utiririka kuja kwako, huwa ni nyingi zaidi ya ile uliyowekeza awali.

Biashara imara inajengwa na aina ya wamiliki ambao wako tayari kufanya kazi bila ya kudai malipo (wanafanya kazi bure). Mojawapo ya sababu za kukufanya wewe ufanye kazi bure au bila kudai malipo, ni kukuwezesha wewe kujifunza tabia ya kujitolea kwa muda na kujenga VIINGIZA-PESA kabla ya kupokea au kupata faida.

Biashara yenye kuleta mafanikio makubwa inajengwa na vitu vitano muhimu, yaani: kiingiza pesa, wafanyakazi, wataalam, wawekezaji na mmiliki wa biashara.

Katika vitu 5 vinavyounda mfumo wa biashara kuna vitu vinatakiwa kulipwa kwanza na kuna vingine vinalipwa mwishoni. Hapa chini kuna orodha ya nani anatakiwa kulipwa kwanza na nani anatakiwa kulipwa akiwa mwisho:

1. Viingiza-Pesa (Biashara au Uwekezaji)
2. Wafanyakazi (Uliowaajiri)
3. Wataalam (Wahasibu, Wanasheria, Mtaalam mwelekezi)
4. Wawekezaji (wenye hisa)
5. Mmiliki wa biashara (wewe)

Wewe kama mmiliki wa biashara lazima ukilipe “Kiingiza-Pesa” kwanza. Maana yake ni kuendelea kuwekeza pesa kiasi cha kutosha na rasilimali, ili kutunza na kufanya Kiingiza-Pesa chako kuwa imara na kukua zaidi.

Wamiliki wengi wa biashara, mara nyingi ujiweka mbele kuliko au zaidi ya kiingiza-pesa, wafanyakazi, na watu wengine wote. Ndiyo maana biashara nyingi ushindwa kuendelea na hatimaye kufa.

Mmiliki wa biashara ni mmojawapo wa watu wanaotakiwa kulipwa mwishoni. Hii ni kutokana na ukweli kwamba lengo kuu la yeye kuanzisha biashara ni kulipwa zaidi ya mtu yeyote. Lakini, ili kuweza kulipwa zaidi ya wengine, lazima mmiliki wa biashara ahakikishe watu wote na vitu vingine vinalipwa kwanza.

SOMA; Mwajiriwa Jilipe Kwanza Mjasiriamali Ufanye Nini?

Lengo la kuandika makala hii, ni kukufundisha wewe usije kufanya kazi kwaajili ya kulipwa pesa. Nataka ujifunze tabia ya kuchelewesha ujiko, heshima, sifa n.k. Pia, ujifunze kufanya kazi kwaajili ya kujenga VIINGIZA-PESA ambavyo thamani yake huwa inakua. Nataka ujifunze kujenga VIINGIZA-PESA na siyo KUFANYA KAZI kwaajili ya pesa.

Biashara nyingi zinazoanzishwa huwa zinashindwa kufuata orodha hii au ushauri kama huu ninaoutoa leo. Nimekutana na watu wengi ambao huwa wanaanzisha biashara kwa kukopa pesa au kupata michango kutoka kwa marafiki, familia na kwa wawekezaji wengine. Mara moja huwa wanakodi ofisi kubwa, wananunua magari ya kifahari, na kujilipa mishahara mikubwa kutoka kwenye mtaji wa wanahisa au wawekezaji badala ya faida inayotoka kwenye biashara yenyewe.

Matokeo yake anajikuta kumebaki pesa kidogo sana, hapo ndipo ujaribu kulipa biashara, wataalam kiasi kidogo sana cha pesa. Katika biashara ya namna hiyo, ni mara nyingi wawekezaji ndio ukwama kwa kushindwa kulipa gharama za uendeshaji wa biashara kama ilivyo biashara nyingi zinazoanza siku hizi.

Ukilipa wengine kwanza kwenye biashara unayomiliki, ni kwamba pesa yote uliyowalipa wengine pamoja na faida lazima zirudi. Lakini ukijijali wewe kwanza na kulipa wengine mwishoni, basi ujue kuwa pesa nyingi uliyotumia haitarudi kamwe na huo ndio utakuwa mwisho wako kwenye ulimwengu wa biashara.

Ukweli ni kwamba, watu wote ambao huwa ni lazima kulipwa kwanza, mwisho na mwisho huwa ndio wanalipwa kidogo. Mmiliki wa biashara lazima ujilipe wa mwisho, kwasababu huko katika biashara kwa lengo la kujenga KIINGIZA-PESA. Kama huko katika biashara kwaajili ya kupata mshahara mkubwa, basi usiwe katika biashara. Kwa maneno mengine ni kwamba unatakiwa kuanza kutafuta kazi ya “kuajiliwa”.

Kama mmiliki wa biashara amefanya kazi nzuri na kutimiza majukumu yako yote ya kulipa wengine wote kwanza, ili wakujengee VIINGIZA-PESA, tunategemea kwamba kiingiza pesa kilichojengwa na wengine waliolipwa kwanza kitakuwa na thamani kubwa zaidi kuliko pesa ambayo angepata kama angeamua kujilipa kwanza kabla ya wengine.

Uzoefu unaonyesha kwamba “watu wengi hawako kwenye ulimwengu wa biashara ili kujenga au kupata VIINGIZA-PESA. Watu wengi wapo katika ulimwengu wa biashara kama “waajiliwa au wataalam waliojiajili” kwasababu wanapeda maisha ya mshahara na ujira. Hii ndiyo mojawapo ya sababu kubwa ya kuwa na matajiri wachache (chini ya asilimia 5) nchini Tanzania na kwingineko duniani. Ni asilimia 5 ya watu katika jamii wanaotambua thamani ya VIINGIZA-PESA kuliko MSHAHARA.

Mmiliki wa biashara au mjasiriamali upata pesa nyingi mwisho wa siku kwasababu mwanzo wa siku ni lazima awe mtu wa kujitoa kwaajili ya wengine (mwenye roho nzuri). Mmiliki wa biashara, ndiye uchukua au kukabiliana na hatari kubwa na pia kuwa wa mwisho kulipwa.

Kama wamefanya kazi nzuri, kiasi cha pesa kinaweza kuwa kikubwa ajabu. Ndiyo maana ni muhimu kufuata orodha hii (kiingiza-pesa, wafanyakazi, wataalam, wawekezaji na mwisho ni mmiliki), kila wakati unapoanzisha biashara ni lazima uendelee kufanya kazi bila malipo (bure) kwanza.

Siku hizi, napendelea mtindo wa kufanya kazi bure, kwasababu ninataka pesa kubwa mwisho wa siku. Watu wengi ambao bado tuko kwenye ajira na waliojiajiri tuna kikomo au mipaka juu ya ni watu wangapi tunaweza kuwahudumia. Kwahiyo, pesa au kipato chetu kina ukomo na ni kidogo sana.

Mjasiriamali au mfanyabiashara ambaye anaelekeza nguvu zake kwenye kujenga biashara ambayo inatoa suruhisho kwa watu wengi zaidi, atazidi kuwa tajiri zaidi na zaidi. Wafanyabiashara wa aina hii wanapata zawadi kubwa kwasababu wao ujenga “mfumo au Kiingiza-pesakwaajili ya kuhudumia watu wengi zaidi na zaidi. Ndiyo maana wamiliki wa biashara wanaweza kuwa matajiri wakubwa kwa haraka sana, na watu amabao ufanyia mshahara, upata utajiri kwa mwendo wa kinyonga.

Katika maisha kuna sheria inayosema kwamba “pokea halafu na wewe utoe kwa wengine” Ni sheria ambayo imekuwepo kwa miaka mingi na itaendelea kuwepo kwani bado inakidhi mahitaji ya sasa. Leo hii, kuliko ilivyowahi kutokea, ni muhimu kutaka kujijali mwenyewe na wale unaowapenda.

Lakini, kama unataka kuwa tajiri ni lazima kwanza ufikirie kutoa mchango wako wenye kukidhi mahitaji ya watu wengi kadiri unavyoweza kwanza. Ni sheria. Ninaamini katika sheria ya msaada sawa kutoka pande zote mbili na wazo la kutoa msaada bila kuhitaji malipo ni njia nzuri sana ya wewe kuwa tajiri mkubwa.

Tunakumbushwa kuwa watu wema na wenye kujali wengine ndio watapata neema ya utajiri. Hii ni sawa na kusema kuwa “kama unataka kutabasamu, kuwa wa kwanza kuachia tabasamu. Kama unataka mapenzi, kuwa wa kwanza kutoa mapenzi. Kama unataka kueleweka basi kuwa mtu kwanza kuwaelewa wengine.

No comments: