"Sisi kama wajasiriamali wa kweli lengo letu la kuanzisha biashara sio kwaajili ya kupata MSHAHARA bali ni kujenga VIINGIZA-PESA” ~ Cypridion Mushongi
Sifa kuu ya mwajiriwa huwa ni kulipwa “mshahara au ujira”. Maana yake ni kwamba yule aliyekuajiri anawajibika kukulipa muda wako ambao umeutumia kwenye biashara yako. Haijalishi mshahara wako ni mkubwa au mdogo kiasi gani bali mshahara wako ni..
sehemu ya gharama za biashara ya mwajiri. Kama mshahara wako ni sehemu ya gharama ambazo mara nyingi ulipwa na mwajirii, maana yake ni kwamba wewe unalipwa sehemu ndogo tu ya kile unachozalisha.
Kwa maneno mengine kupata mtaji wa kufanya mambo makubwa kwa waajiriwa walio wengi ni changamoto kubwa. Kwahiyo, ikiwa wewe unapata mapato kutokana na mshahara peke yake, ni vigumu kutajirika kwasababu, mapato yako yanakuwa na ukomo.
Watu wengi tulioajiriwa hivi sasa tunakabiliwa na changamoto ya umaskini, kutokana na tabia ambayo si rafiki wa maisha bora. Tabia yenyewe ni ya “kulipa watu wengine kwanza kila tunapopata pesa huku sisi tukijilipa mwishoni”. Tabia hii inatufanya tukose mitaji ya kuwekeza na hivyo kujikuta tukishindwa kabisa kujenga na kuendeleza Viingiza-pesa.
Kwa mwajiriwa ambaye unaona maisha unayoishi huyapendi, ni sharti ujijengee tabia ya “kujilipa kwanza” kila upatapo pesa au kuingiza pesa mfukoni.
Kwa maana nyingine ni kwamba lazima matumizi yako yote yapangwe na kufanyika kulingana na kiasi kile tu kinachobaki baada ya kutoa akiba (kujikata kodi). Utaratibu huu wa kutenga akiba kwanza kabla ya kununua kitu chochote ndio tunaita “kujilipa kwanza” au “kujikata kodi kwanza”.
Ni muhimu kujiwekea akiba kila upatapo pesa. Jenga tabia ya kuweka akiba kwa kuanza kujizoesha kukaa na pesa kwanza kwa muda fulani, bila kufanya matumizi yoyote.
Ukishaweza hilo, hatua ya pili ni kuanza utaratibu wa kutenga asilimia (%) fulani kama akiba. Akiba ni suala nyeti na muhimu kwa mwajiriwa yeyote mwenye kujitambua, na linatakiwa kupewa kipaumbele namba moja kila tunapopata pesa.
Kwenye uliwengu wa ujasiriamali na biashara, mambo ni tofauti na watu walioko kwenye ulimwengu wa ajira. Katika ulimwengu halisi wa ujasiriamali na biashara, tabia ya kujilipa kwanza ni sumu kali na mara nyingi imekuwa ikiua sana Viingiza-Pesa au vitegauchumi vingi.
Ukiwa kama mjasiriamali wa kweli na mmiliki wa biashara unatakiwa kujilipa ukiwa mtu wa mwisho. Unashauriwa kujilipa wa mwisho kwasababu, lengo la kuanzisha biashara sio kwaajili ya kupata mshahara BALI ni kwaajili ya kujenga “Kiingiza Pesa”.
Endapo wewe umeamua kuanzisha biashara kwa malengo ya kupata mshahara mkubwa, basi ujue kuwa muda wowote kuanzia sasa, biashara yako inaweza kufa. Biashara zetu nyingi zimeshindwa kuleta mafanikio kinyume na matarajio yetu, kutokana na ukweli kwamba watu wengi wako kwenye biashara kama “waajiriwa”.
Kuendelea kufanya biashara kama muajiriwa ni miongoni mwa sababu kubwa ambazo zinawafanya wajasiriamali na wafanyabiashara wengi kupata mafanikio hafifu.
Wajasiriamali wengi wameshindwa kubadilika kwanza kifikra na kitabia, ili kuishi maisha halisi ya mjasiriamali. Watu wanaendesha biashara na miradi mingine ya kiuchumi kwa kufuata mfumo wa ajira na tabia za waajiriwa.
Kwahiyo, mwajiriwa anatakiwa kushikilia sana dhana ya “kujilipa kwanza” pindi anapolipwa mshahara, mambo mengine yanayobaki amwachie mwajiri.
Mjasiriamali (Mmiliki wa biashara), yeye ni lazima awe mtu asiyekimbilia kujilipa kwanza, kwasababu, mambo yote yanayohusu ustawi wa biashara wakiwemo wafanyakazi (waajiriwa), yote yanamtegemea kwa kiasi kikubwa.
Watu wegine wanapolipwa kwanza, mjasiriamali inabidi akubali kupokea kile kilichosalia ndicho ajilipe hata kama ni kidogo. Kwakufanya hivyo, atasaidia kukuza na kuimarisha Kiingiza-Pesa.
Kiingiza pesa kikishakua vyakutosha, itakuwa ni fursa kwa mjasiriamali kuanza kuvuna mapesa yasiyokuwa na kikomo. Na itakapofikia hatua hii, mmiliki wa biashara ndiye atakayekuwa anapokea pesa nyngi kuliko mtu yeyote, japokuwa ataendelea kulipwa mwishoni.
No comments:
Post a Comment