Mara
zote tunapenda kuhitaji bidhaa ambazo tayari tumeziona zipo au tumezizoea. Utafiti
umebaini kuwa mahitaji ya binadamu huwa hayana kikomo, kiasi kwamba kila mara
anhitaji ama kitu kipya au kile alichokizoea. Ukweli ni kwamba, bado maisha
yetu ni magumu kwasababu bado tunatumia nguvu nyingi kufanikisha mambo
mbalimbali yanayohitajika katika maisha yetu kwa ujumla. Ugumu wa maisha
unatokana na kiwango kidogo sana cha ubunifu na uzalishaji wa bidhaa. Hapa
Tanzania, bado tunazidi kutegemea mbinu zile zile za zamani ambazo wazee wetu
walizitumia wakati huo kupambana na maisha. Maana yake ni kwamba katika zama
hizi hatujatoa jipya sana lenye kuendana na kasi ya mabadiliko yanayoendelea
kutokea duniani kote.
Kwa
sasa Tanzania, tuna mahitaji makubwa sana ya ubunifu na teknolojia katika
nyanja mbalimbali za maisha. Yawezekana watu wengine wako tayari kulifanya hili
lakini wanaogopa au wana hofu na mashaka juu ya kukosekana kwa soko la bidhaa mpya
ambazo zitatokana na ubunifu au teknolojia mpya. Kamahiyo, kama hiyo ni
mojawapo ya sababu, basi tunatakiwa kuondoa hofu na kuanza kufikiria “tutaipatia nini dunia”, yaani tuwe na
mtazamo kama wa watu wa sanaa (craftsman mindset). Watu katika fani ya sanaa ni mfano wa kuigwa,
kwani wao huwa hawasubili watu wawambie nini wanataka, bali wao uchukua muda
wao na kuwaza ni kitu gani kinaweza kuwafurahisha watu basi! na kweli kama ni
mziki ukitoka, unaona kila mmoja anajaribu kusaka CD ili kununua.
Hapa
Tanzania, katika kipindi cha miaka kumi iliyopita kuna vitu vimeibuliwa ambavyo
havikuwepo huko nyuma. Lakini baada ya wabunifu mbalimbali kuvileta kwetu,
tumejikuta tunavihitaji sana kiasi cha kwamba, kuna watu wengi ambao hawawezi
kufanya mambo yao yakaenda sawasawa bila kutumia vitu hivyo. Mifano ni mingi
sana, lakini tuangalie michache tu kama ya usafiri wa pikipiki, chakula cha
ndizi na matumizi ya simu za mkononi
Usafiri wa
pikipiki:
Huduma ambayo haikuwepo huko nyuma hii ya usafiri wa pikipiki maarufu kama “BODA BODA”. Ebu jiulize kabla ya ujio wa
usafiri huu, watu walikuwa wanatumia nini kusafiri? Najua utasema magari,
lakini walio wengi, magari yalikuwa hayawezi kufika majumbani kwao. Kwa wale
wanaofanya kazi hasa sehemu za starehe, wanalazimika kutoka kazini wakati wa usiku
wa manane, usafiri huu wa pikipiki umekuwa mkombozi kwao. Kumbe kwa muda wote ambao
hakukuwepo na usafiri wa pikipiki, watu waliendelea na maisha kama kawaida na kwa
wakati huo hakuna aliyewahi kufikiria
juu ya mahitaji makubwa ya usafiri huu. Kwa maana nyingine ni kwamba, tangu
zamani tulikuwa na mahitaji makubwa ya huduma hii, lakini hatukujua kabisa kama
tulihitaji kitu hicho, mpaka kilivyoletwa na wabunifu wetu, ndio tukaanza
kujisikia kuwa na mahitaji ya Usafiri wa pikipiki.
Chakula cha
ndizi:
Hapo zamani tulikuwa na makundi manne ya ndizi (kupika, mbivu, kuchoma/kukaanga
na pombe). Aina ambazo zilikuwa kwenye kundi la ndizi za kuchoma na kukaanga,
kwa hapa Bukoba zinafahamika kama “e’nkonjwa/gonja”
na huko Karagwe ni “e’ngarambi”. Kutokana
na matatizo mbalimbali, aina hii ya ndizi ilianza kupungua na hivyo kuadimika.
Kutokana na kuadimika kwake, ndipo wajasiriamali hasa kutokea miji ya kanda ya
ziwa, walipoamua kujaribu kukaanga aina
nyingine kutoka kundi la ndizi za kupika,
lengo likiwa ni kuhakikisha wanawapatia wateja wao angalau ndizi wakati wanapo kula
nyama choma. Baada ya watu kuonja aina nyingine ya ndizi hizi za kupika, walitokea
kuzipenda pia na ndipo mahitaji ya ndizi za kupika yakaongezeka mara mbili
yaani zikawa zinakaangwa na wakati huhuo zikawa zina pikwa. Hivyo, tunaona
kwamba watu kwa sasa wanahitaji sana ndizi zilizokaangwa bila kujali ni aina
ipi ya ndizi, japo wakipata ile ya aina ya “gonja”
wanafurahi zaidi. Watoto waliozaliwa hivi karibuni na kukulia kanda ya ziwa
hawatajua kuwa kulikuwa na aina fulani ya ndizi ambayo ni maalumu kwaajili ya
kukaanga, bali watapokea kilichopo au kitakachokuja baadae na hicho ndicho
watazidi kuhitaji.
Matumizi ya simu
za mkononi:
Tualiowengi hawakujua kama wanahitaji mawasiliano ili kuweza kufanya biashara
na shughuli nyingine za kimaisha. Wale wagumu walianza kuwasema wenzao kwamba
wanapoteza pesa kwa kupiga simu lakini kwakuwa simu tayari zilianza kuonekana
kila mahali basi na wale waliofikiri kuwa hawazihitaji baadae waliona umuhimu
wa simu. Baada ya watu wengi kumiliki simu za mkononi, sasa kuna aina mpya
zijulikanazo kama “Smartphone” aina
hizi za simu kwa Kagera zinajulikana kwa jina maarufu kama “tachi”. Tunaona kuwa kadiri siku
zinavyokwenda watu wengi wanazidi kuona umuhimu wa simu za aina hii, kwasababu wale
ambao hawajaamua kuwa nazo, wanaona wenzao wenye simu hizo wanavyofaidika na Huduma
zipatikanazo kwenye simu za “Smartphone”.
Mfano: wale wenye magari wanaweza kupiga picha spare na vipuli vya aina
mbalimbali na kuvituma kwa wenye maduka ili kujua kama vinapatikana na ni bei
gani, wengine wanaweza kupata taarifa kwa picha juu ya aina za nguo na mitindo
mbalimbali n.k. Tokea huko nyuma hatukujua kama tulihitaji huduma za namna hii
kwasababu tulikuwa hatujaziona, lakini baada ya kuona umuhimu wa matumizi ya
simu, sasa tuna mahitaji makubwa sana.
Kwakuwa watu wanapenda kuona kitu kwanza alafu ndio wanahitaji, basi hali hii inatoa fursa ya kufanikiwa haraka kwa
wale wote ambao wako tayari kufikiri, kubuni na kugundua vitu vipya, kwasababu,
soko lipo la kutosha kwa wazalishaji wote. Kinachotakiwa ni kwamba kitu kipya
ulicholeta kiwe na manufaa makubwa kwa watu waliowengi. Ni muhimu kwa wapenda
mafanikio kukaa muda wote katika hali ya utafiti kwenye jamii. Kwakufanya hivyo,
ndipo tutaweza kugundua mahitaji muhimu ambayo ni mapya.
Ili kufanikisha hili, ni
vyema tukajifunza jinsi ya kutumia macho ya ubongo kuona fursa badala ya
kutumia macho ya kawaida kama tulivyozoea. Pia, tunahitaji kuwekeza muda mwingi
kufikiri na kuchambua hali ya maisha yetu na tunatakiwa kuwa wadadisi kila
mahali tunapokuwa, na hatimaye tuchukue hatua na kuanza kuzalisha bidhaa mpya
na zenye manufaa makubwa kwa jamii.
Wito
kwa wajasiriamali; ni muhimu sana tuanze sasa kutumia muda mwingi tulionao kufikiri
na kuongeza kasi ya ubunifu katika kila nyanja ya maisha. Likifanyika hili, tuna
uhakika wa kupiga hatua kubwa sana kimaendeleo hasa ya kiuchumi na kijamii. Wito
pia ni kwa wale wote waliokabidhiwa majukumu ya kuweka mazingira wezeshi
kuendelea kulisimamia hili, kwani tunaanza kuona ongezeko la vijana ambao wako
tayari kufikiri na kubuni vitu vipya ambavyo hatimaye vitarahisisha maisha na
hivyo kuendelea kuifanya Tanzania kuwa mahali pazuri pa kuishi.
Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO.
1 comment:
This awesome Mr., its really educative
Post a Comment