Tuesday, February 9, 2016

Muda wa Ziada Utakukwamua Namna Hii


“Yale unayofanya wakati wa muda wako wa ziada ndiyo yanakuweka huru au utumwani” ~Jarod Kintz
 

Utafiti uliofanyika duniani umeonyesha kuwa wengi wa wajasiriamali waliofanikiwa, walianza biashara zao kwa kutumia muda wao wa ziada. Ni mara ngapi umesikia mtu akisema “ningependa kufanya biashara hii LAKINI tatizo sina muda?” Unapoona mtu akwambia sina muda maana yake ni....
kwamba huyo mtu hana motisha, nia wala shauku ya kufanya hicho kitu ambacho umemshirikisha.

Majuzi nilipata kuongea na mzee mmoja kati ya wale waliosoma zamani zile za miaka ya 86 katika chuo kikuu cha kilimo Sokoine, Morogoro. Katika mazungumzo yetu alimtaja sana muhadhiri Profesa Mmari juu ya kauli yake kuhusu MUDA, anasema profesa huyu alizoea kusema darasani “Huwezi kukosa muda wa kufanya kitu unachokipenda”.
Kwa maana nyingine ni kwamba ukiona hujapata muda wa kufanya jambo fulani, basi ujue kuwa bado hujapenda au hujataka kufanya hivyo. Wakati mwingine ni vizuri tukatambua kuwa kitu kinachoitwa muda ni kitu kinachotengenezwa na sisi binadamu na kiuhalisia ni kwamba mara nyingi mpangilio wa shughuli zetu ndio unaotufanya ama tuwe na muda au tusiwe na muda kabisa.

Kwa mfano: Katika kila wiki kuna masaa 168. Je? Uliwahi kujiuliza masaa yote haya huwa yanakwenda wapi? Hapa utaona kuwa matumizi ya masaa 168 ya wiki nzima yanatofautiana kulingana na mfumo wako wa maisha.

Katika ulimwengu wa MUDA tunaweza kusema kwamba kuna mifumo ya maisha aina mbili. Moja ni lile kundi la watu wengi wanaofuata mfumo wa maisha ya KUUZA muda na wapo watu wengine wachache wanaofuata mfumo wa maisha ya KUWEKEZA muda wao.

Mfumo wa maisha ya KUUZA muda au “kubadilishana muda na pesa”, unafuatwa zaidi na watu ambao ni waajiriwa pamoja na wale waliojajiri au kuajiriwa na biashara zao. Wewe kama ni muajiriwa, biashara yako kubwa ni kuwapa muda watu wengine halafu wao wanakupa pesa na maisha yanakwenda.

Mgawanyo wa matumizi ya muda kwa wale wote wanaofuata mfumo wa maisha ya KUUZA muda ni kama hivi:

Katika wiki moja kuna masaa 168:

  • Masaa 56 – kulala
  • Masaa 42 – kula, kusafiri, muda na familia n.k.
  • Masaa 40 – Kazi ya ajira
  • Masaa 30 – muda wa ziada, starehe, n.k.
Kwa kuangalia mgawanyo wa matumizi ya muda hapo juu ni kwamba, sisi wenyewe tunao uwezo wa kubadilisha matumizi ya muda uliopo. Kwa mfano: tunaweza sana kubadilisha matumizi ya masaa 30 kwa wiki ambayo ni ya ziada na starehe, yakawa ni masaa ya kufanya kitu kwaajili ya kutimiza ndoto yako au kukuletea utajiri siku za mbeleni.

Katika maisha tunaambiwa kuwa kitu ambacho huwatofautisha matajiri na watu wengi wa kawaida (masikini) ni kwamba; watu masikini utumia zaidi “muda wao wa ziada” kwenye starehe. Matajiri wao, utumia sehemu kubwa ya muda wao wa ziada katika kujenga biashara zao. Hakika hali hii ndiyo imeleta mgawanyiko mkubwa na tofauti kubwa kimaisha kati ya walionacho na wasiokuwanacho.

Tafiti nyingi zilizowahi kufanyika duniani, zinaonyesha kuwa mtu wa kawaida anatumia zaidi ya masaa matano kwa siku kwenye starehe. Starehe tunazosema ni kama vile kuangalia runinga, kuangalia mambo mbalimbali kwenye simu yako ya “smart phone”, movies kwenye tablet, kuangalia michezo, kuangalia video za michezo mbalimbali, vikao vya harusi n.k.

LAKINI, hiyo haina maana kwamba usifurahie starehe yoyote, BALI inabidi kufanya hivyo kwa wastani au kiasi. Kimsingi starehe hazitakiwi kula muda wako wa karibu moja ya tatu ya muda wako wa kufanya kazi kila siku. Usifanye hivyo hata kidogo.

Kila wakati ujiulize ni gharama kiasi gani unazilipa kutokana na tabia yako ya kuendekeza starehe? “million 1 kwa mwaka? million 5 kwa mwaka? au Milioni 10 kwa mwaka? Au zaidi? Je utajisikiaje kama kuachana na tabia ya kuendekeza starehe itakufanya utajirike?.

Hapa tunaona kuwa tunapata hasara mara mbili; kwanza tunapoteza rasilimali muda na pili tunapoteza pesa wakati vitu hivi viwili tunavyovipoteza kila siku ndivyo vinahitajika sana katika kujenga mtaji wa kufanya mambo makubwa mazuri tunayoyatamani kila siku

Anza biashara katika muda wako wa ziada (masaa 30/wiki)’…

Ukweli ni kwamba, kama unataka kutajirika, utatakiwa pengine kuanza biashara kwa muda wako wa ziada. Huitajiki kuacha ajira au kazi yako ya ajira mara moja na pengine unaweza ukaamua kutokuacha ajira yako. Anza leo kujiambia maneno haya kila siku “sasa hivi ninafanya kwa muda wa ziada kwenye ndoto yangu na muda wote kwenye ajira yangu, lakini haitachukua muda nitaanza kufanya muda wote kwenye ndoto yangu. Fikiria maisha yatakuwaje?

Kwahiyo inatosha kusema kuwa masaa 30 kila wiki yanapotea na wakati huo huo tunaendelea kuwa masikini na kuishi maisha ya kubangaiza kila siku. LAKINI ni masaa hayo hayo 30 kwa wiki ambayo yakiokolewa na kuwekezwa vizuri yatakuweka huru na mwisho wake utakuwa mtu wa kusema, “biashara yangu ya muda ilifanya vizuri kiasi kwamba niliweza kuacha ajira”.

Wakati kuanza harakati za uokoaji wa masaa 30 yanayoangamia kila wiki ni leo. Endapo tukiacha masaa hayo yakaendelea kuangamia basi, tujue kuwa hatutabaki salama.

No comments: