Monday, March 16, 2015

Je? Utamtabuaje Rafiki Yako Mwenye Imani Sahihi Juu ya Pesa?



Wakati fulani ndani ya mwezi mwaka huu, nikiwa kwa mtoa huduma ya kubrashi viatu, nilikutana na jamaa mmoja akiwa akiongelea juu ya mambo ya maisha na mtoa Huduma huyo. Nilipofika waliendelea na stori zao na mimi mara moja moja nikawa naruhusiwa kuchangia hoja iliyokuwa mezani. Wakati huo wote walijadili sana juu ya changamoto za kimaisha, ikwemo tatizo sugu la ukosefu wa pesa na hivyo kufanya maisha kuwa magumu sana. Mimi pamoja ya kwamba nilichangia lakini nilikwa nasikiliza zaidi mjadala ulivyokuwa ukienda ili niweze kujifunza kitu. Baada ya mazungumzo hayo nilipata wazo la kutafakari na kuanza kuandika makala juu ya “Imani Yako Kuhusu Pesa!” wazo hili lilitokana na ukweli kwamba watu wawili hawa walihitimisha mjadala kwa kusema kuwa “Fedha ina Siri Kubwa” wakiamanisha kwamba kanuni au njia ya kupata pesa haijulikani. Ukienda mbele Zaidi unagundua kwamba, tayari kwenye jamii kumekwisha jengeka imani kwamba kupata pesa ni kubahatisha, Kiasi kwamba wengi wao wanaotafuta pesa hawana uhakika kama ipo siku watapata.

Kutokana na hitimisho hilo la kwamba “pesa ina siri kubwa” niwazi kuwa kuna ombwe la uelewa na ufahamu kuhusu maana halisi ya pesa. Na niseme kuwa imani iliyopo kwa sasa juu ya pesa yawezekana siyo sahihi (ni potofu). Upotofu huu wa imani juu ya pesa  unajidhihirisha Katika matukio mengi hapa nchini kwetu Tanzania na nchi za jirani, ambapo kumekuwepo na matukio mengi ya watu kujaribu kutumia ushirikina ili kupata mafanikio ya haraka na hasa mafanikio ya kifedha.

Kama ilivyo imani Katika dini kwamba mwanadamu aweza kuwa na imani potofu juu ya wokovu au akawa na imani iliyo ya kweli kuhusu wokovu na linapokuja swala la upatikanaji wa pesa ni hivyo hivyo, kwani imani yetu tuliyonayo juu ya pesa imetokana kiwango cha uelewa tulionao. Lakini niseme kuwa ni bahati mbaya sana kwamba uelewa wetu juu ya kitu pesa bado ni mdogo sana, licha ya kuwa “Pesa” ni moja kati ya vitu vichache vinavyopendwa sana duniani. Kama ilivyo katika dini zetu, kwa waumini wa madhebu yote, ili waweze kuwa na imani sahihi juu ya muumba wao, wanahitaji kwanza neema ya Mungu, lakini pia wanahitaji watu ambao wako tayari kujitoa na kufanya kazi ya Mungu ili kusaka ukweli na kuupeleka ukweli huo kwa watu wote kwa jina la “Habari njema” Hivyo basi kadili watu wanavyozidi kupata ukweli kuhusu wokovu ndivyo watazidi kujenga imani ya kweli au sahihi juu ya wokovu au kazi ya Mungu.

Kwahiyo, kutokana na mantiki hii ya wokovu, Ndiyo maana wengine tayari tumeanza kuchukua hatua ya kusaka ukweli juu ya “Fedha” ili ukweli huu uweze kusambaa kwa watu wote. Imani yangu ni kwamba, iwapo watu watapata ukweli huu kupitia makala hii au njia nyinginezo, basi ukweli huu, utawezesha wengi kubadili na kujenga imani iliyo sahihi. Kadili watu watakavyozidi kujenga imani sahihi juu ya pesa ndivyo itakavyokuwa rahisi kupata pesa na hivyo kuweza Kuboresha na kuishi maisha ya ndoto zetu.

Katika kutambua nani mwenye imani sahihi juu ya pesa, unaweza kuangalia dhana, misemo, methali na nahau juu ya pesa kwa mtu binafsi au kundi la jamii husika. Hivi vyote, ndivyo vigezo au viashiria tunavyoweza kuvitumia kupima imani ya mtu aliyonayo juu pesa. Kwa kufahamu imani yake iko wapi ni rahisi sana kufahamu iwapo huyo mtu ana imani sahihi au imani potofu. Mfano wa baadhi ya viashiria vya imani ya mtu juu ya pesa ni hivi hapa; ”Pesa ni Sabuni ya Roho” : Dhana hii ya kuamini kuwa pesa ni sabuni ya roho, inatuonyesha kuwa ndani ya fikra zetu tunadhani pesa ndilo hitimisho la kazi tuliyokuwa tukifanya bila kujali tumeifanya na kuumia kwa muda gani. Ukitaka kufahamu nani anaichukulia pesa kama hitimisho, utamuona tu anavyokuwa amechangamka na kuanza hata kubadili mfumo wa maisha ikibidi hata vyakula, vinywaji, mavazi, hubadilika kwasababu mtu huyu anajiona amefika mwisho na roho yake imesafishika. Kama alikuwa akifuga ng’ombe, sasa ataanza kutokuwajali na baadae mradi utakufa na mwisho zile pesa ambazo alikuwa ameishaanza kusahau zilikotoka na zenyewe zitaisha. Iwapo hii ndiyo imani yetu juu ya pesa basi ni wazi kwamba pesa hapa tunaichukulia na kuitumia kama mapato. Tatizo la kuiona pesa kama mapato huwezi tena kwenda hatua zinazofuata ili kukamilisha malengo yako ya kimaisha na badala yake unaishia njiani kabla ya kufika mwisho. Wale waliofanikiwa au wale matajiri, wakipata pesa bado haichukulii kama mapato badala yake utumia hiyo pesa kuanzisha mradi mwingine, na pesa yote inayopatikana Ndiyo utumika tena kuazisha mradi mkubwa zaidi ambao faida yake Ndiyo mtu kuitumia kwenye vitu vya hanasa (luxuries).

Kwahiyo, hili tuweze kuiishi imani hii ya “Pesa ni Sabuni ya Roho” ni lazima kufahamu kuwa ukishapata pesa unafurahi sana, lakini ni vizuri furaha hiyo isitusahaulishe tunako kwenda na tuendelee kuiona kuwa ni makaratasi ambayo tunahitaji kuyatuma kwa wengine ili tupate pesa nyingi zaidi kwaajiri ya kuwekeza kwenye kuzalisha vitu na huduma bila kikomo.

“Kupata pesa ni bahati, na kama ukuandikiwa na Mungu kuzipata hata ungefanyaje! Utapata” Usemi huu unaonyesha kuwa kana kwamba kuna baadhi ya watu ambao wamezaliwa na bahati ya kupata pesa na inaonekana ni wachache sana ukilinganisha na wale wasiokuwa na bahati. Kuendelea kuwa na imani hii vichwani ni janga la kitaifa kwasababu, kila utakapo anza mchakato wa kutafuta pesa fedha na ukakumbana na vikwazo na changamoto mbalimabli ni dhahili utakuwa wa kwanza kukata tamaa na kuingia kwenye mtego wa kutafuta njia za mkato ili kupata pesa.

Hili usiendelee kuamini kuwa kupata pesa ni bahati, ni vizuri ukafahamu kwamba kila mtu amezaliwa na uwezo wa kupata pesa haitakayo. Kinachohitajika kabla ya kutafuta pesa ni kuchukua muda wako ukafikiri na kutafakari majibu ya maswali haya; Je? Pesa ni kitu gani?, Pesa hupatikana wapi?, kwanini wengine kipindi Fulani pesa na baadae kuishiwa?; Je? Pesa inakujaje kwako na inapoteaje? Je? Wewe unatafuta shilingi ngapi mwaka huu? Kwako fedha itafuata nini? n.k. Kadili utakavyoweza kujibu maswali haya wewe mwenyewe itakufanya utafakari kwa kina na majibu utakayopata yatakufanya ubadili imani potofu uliyokuwanayo na baadae kujenga imani mpya kuwa “Kupata pesa ni Kuwa na Kitu au Huduma ambayo itawafanya watu wengine waitume pesa yao kwako kufuata vitu ulivyonavyo pamoja na huduma huliyonayo. Na hili uweze kupata vitu na huduma msingi wake ni kazi na ubunifu, iwapo utavitumia hivi vipaji yaani “Kazi na Ubunifu” sioni sababu nyingine ya kukufanya ukose pesa.

Ewe mtanzania chunguza imani yako juu ya pesa, ili ujitenge na wale wanaotumia njia ya mkato na kutafuta utajiri wa haraka. Kama ukikuta imani yako ni potofu, basi kata shauri leo na kubadili ili uwe na imani sahihi juu ya pesa kabla ya kuanza kuitafuta.

Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO

~KARIBU TWENDE KAZI PAMOJA~

No comments: