Monday, March 23, 2015

Suruhisho Pekee la Kuweza Kupata Mafanikio Makubwa kwa Kila Jambo Unalofanya ni Kufanya Vitu Vichache Ambavyo ni Muhimu



Kwa sasa, watu wengi duniani wanakabiliwa na tatizo la msongo wa mawazo katika maisha, sababu mojawapo ikiwa ni pamoja na tabia ya kuendekeza kufanya kila kitu kila wakati. Tabia hii inatokana na hulka ya walio wengi kutaka kila mara kufanya kazi ili kumfurahisha na kumridhisha kila mtu, jambo ambalo limekuwa likichangia kwa kiasi kikubwa katika kupunguza sana ufanisi na ubora wa kazi tunazofanya kila siku na hivyo kutumbukia katika umaskini. Endapo una tabia ya kufanya kazi kwa kumridhisha mtu ni rahisi sana kuwa “mbabaishaji”; kwasababu kila kazi yenye kuhitaji uharaka, utarundikiwa wewe na ukiweza utapewa motisha au posho nyingi. Mwisho wake ile nguvu yako unaitawanya kidogo kidogo katika kukamilisha kazi zote zinazokujia. Ukiwekeza kidogo kidogo kwa kazi nyingi zitakazokujia, mwisho utapata matokeo ya kiwango cha chini sana! Na huu utakuwa mwanzo wa wewe kuitwa “mbabaishaji. 

Tabia ya kutaka kufanya kila kitu, inatokana mafundisho tokea utotoni, ambapo uhamasishwa kusema “NDIYO” kwa kila jambo. Kumbe ni muhimu tangu mwanzo watoto wetu tuwafundishe kusema "HAPANA" na siyo kuwapongeza kila mara kwa kusema "NDIYO" peke yake. Mara nyingi hata watu wazima, unapofanya kazi ukapongezwa anavutiwa na kuhamasika sana na hivyo kuingia kwenye mtego wa kutaka ufanye na kumaliza kila kazi iliyopo mbele yako. Kutokana na tabia hiyo ya kuvutiwa na pongezi unajikuta kila kazi unaikubali hata kama ulikuwa unafanya kazi nyingine za muhimu. Kwahiyo, ni vizuri ujifunze tabia ya wachapakazi hodari ambapo wao uhamini sana falsafa ya “kidogo lakini kizuri” (Less but Better).

Watalamu wanatwambia kuwa ili mtu aweze kufanya kazi kwa kiwango cha juu, ni lazima ajifunze au tujifunze na tuache tabia ya kufanya shughuli nyingi tena ndogo ndogo. Kwani, hii Ndiyo sababu watu wengi anaposhirikishwa fursa Fulani Fulani za Biashara mara nyingi hutoa visingizio vya kuwa hawana muda (busy) au utasikia mtu anakwambia nina mambo mengi sana. Kwa watu walio wengi, hili la kuwa na kazi au mambo mengi sana wanalichukulia kama ni sifa ya uchapakazi na uwajibikaji hodari. Kwahiyo, wanatumia U-Busy kama kipimo cha utendaji bora wa kazi hata kama vitu wanavyofanya havina tija.

Watu waliopata mafanikio makubwa kwa njia halali, mara nyingi wanashauri kwamba, mafanikio makubwa yanahitaji sisi kuwekeza katika vitu vichache ambavyo inakuwa rahisi kuweza kuvipa muda wa kutosha na kuvifanya kwa ufanisi mkubwa. Na katika kulitekeleza hilo, wanatuhasa pia, tuanze mara moja kujijengea utamaduni wa kuweka vipaumbele katika maisha, kwani tusipo fanya hivyo, mtu mwingine atatuwekea vipaumbele ambavyo tutapoteza muda wetu kutekeleza vipaumbele hivyo ambavyo hatuvipendi.

Mara nyingi unapokabiliwa na suala zima la kutekeleza vipaumbele vya watu wengine ni wazi kwamba utafanya kazi hiyo huku ukiwa huipendi na kama huna mapenzi ya dhati kwa hicho unachokifanya basi itakupelekea kufanya kazi hiyo chini ya kiwango. Na iwapo utaendelea kufanya kazi zako chini ya kiwango ni lazima uwe maskini, kwasababu kwa muda mrefu ambao utafanya kazi chini ya kiwango ndani mwako itajengeka tabia ya uvivu hasa ule wa kufikiri. Ukiwa na uvivu wa kufikiri, huwezi kuwa mbunifu na matokeo yake mbinu zako za kupambana na changamoto za maisha zinakuwa zimepitwa na wakati. Kwahiyo, safari yako ya kuelekea umaskini wa kutupa inakuwa imeanza hapo. Ewe mtanzania jitahidi kuwa mjasiri, ili uweze kufanya maamuzi magumu juu ya vitu vichache ambavyo ukiwekeza nguvu zako zote utaweza kufikia haraka maisha ya ndoto yako.

Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO

KARIBU TWENDE KAZI PAMOJA

No comments: