Tuesday, March 17, 2015

Siri ya Waliofanikiwa ni Kuwekeza Kwao Zaidi Kwenye Aina ya Mapato Yasiyokuwa na Kikomo (Tuli)




Unapoanza safari yako kuelekea kwenye mafanikio makubwa ni vizuri ukafahamu ni aina gani ya kipato unachopata kwa sasa? Kwahiyo, ili kuweza kufahamu sifa na aina za vipato, ni muhimu kujua kuwa zipo aina kuu tatu za vipato ambazo ni: Mapato ya Ajira (mshahara); Mapato Hai (kujiajiri); Mapato yasiyo na kikomo au Tuli, (Passive Income).
1.      Mapato ya Ajira (Earned Income)
Haya ni mapato yanayotokana na kufanya kazi ya kuajiriwa (mshahara), ambayo mtu huyapata kutokana na ajira yake. Katika aina hii ya kipato, vigezo vya kukuwezesha ulipwe ni pamoja na aina ya kazi na wadhifa au cheo chako. Pia, mapato haya yanajumuisha mapato yoyote yatokanayo na ajira binafsi (kujiajiri), biashara ndogondogo na shughuli nyinginezo ambazo unapata kipato kutokana na juhudi na muda uliotumika. Kwa maana nyingine, ni kwamba kama husiposhugulika au ukasimama kufanya kazi na kipato kinakoma pale pale.
Ø  Uzuri wa Mapato ya Ajira
·         Mapato yanaongezeka zaidi kulingana na muda na ukubwa wa shughuli inayofanya
·         Hauitaji mtaji kuweza kupata mapato haya
·         Mtaji ni nguvu au ujuzi wako mwenyewe
Ø  Ubaya wa Mapato ya Ajira
·         Uwezi kupata utajiri wa kudumu kwa aina hii ya mapato yanayotokana na mshahara. Kwasababu mshahara unapata, unakula na unanaisha.......Unapata unakula zinaisha.....
·         Siyo mapato endelevu, ukiacha kufanya kazi mapato yanakoma.
·         Mapato haya ya ajira yanatozwa kodi kubwa kuliko aina nyingine zote za mapato na Waajiriwa wanalijua vizuri hili.
Mfano; kwa mtu anayelipwa mshahara wa kiasi cha 1,350,000/- anakatwa kodi hivi:
Aina ya Makato
Kiasi (TSh)/Mwezi
Kodi (Income Tax)
260,400.00
Bima ya Afya
40,500.00
Chama cha Wafanyakazi
27,000.00
Mfuko wa Pensheni
67,500.00
Jumla
394,900.00
Sasa, ebu fikiria mtu anakatwa karibu Shilingi 400,000/- kila mwezi, kiasi ambacho kwa mwaka kinafikia karibu shilling 4,800,000/-. Unaweza kukuta mtu ana biashara yenye mtaji upatao shilingi million 15, siajabu kukuta analipa kodi kiasi kisichozidi shilingi 500,000/- kwa mwaka.
2.      Mapato Hai (Active Income)
Aina hii ya mapato, kwa kiasi fulani inafanana na mapato ya ajira yanayo jumuisha mishahara, kwani mapato haya yanatokana na kuuza na kununua bidhaa kubwa kubwa kama magari, nyumba, kiwanja n.k. Mchakato huu ni kwamba, unanunua kitu halafu unakiuza kwa faida, halafu basi. Ili uweze kupata mapato mengine inakubidi, utafute kitu kingine au ununue kitu kingine haraka ndipo upate tena pesa. Maana yake ni kwamba lazima uwe kazini (active) muda wote huku ukiendelea kuchakarika ndipo upate mapato. Kama ilivyo kwa mapato ya mshahara, pindi unapoacha kununua na kuuza vitu, mapato nayo yanakoma mara moja.
Ø  Uzuri wa Mapato Hai
·         Mapato haya hayahitaji watendaji kazi wengi ili kufanikisha shughuli ni wewe tu mwenyewe. 
·         Kodi yake ni ndogo kulinganisha na ile ya mapato ya ajira
·         Unapata zaidi kutokana na jitihada zako za kutafuta na uchangamkia fursa.
·         Unaweza kufanya na kupata pesa hata pasipokuwa na mtaji. Mfano, unachukua mali (sema gari), Unamwambia jamaa utamletea pesa yake baada ya siku mbili hivi, kumbe wakati huo umeisha tafuta mteja tayari unampelekea, unauza unamlipa jamaa wewe unabaki na faida. Tayari umeisha tengeneza pesa bila hata kuwa na mtaji ~ yaani ni ujanja ujanja tu!
Ø  Ubaya Wake
·         Inahitaji utaalam na ujanja wa hali ya juu na kufahamika pia, unaweza kupewa vitu feki, kuzurumiwa, kuibiwa, kupata hasara n.k.
·         Unaendelea kushughulika wewe mwenyewe ndipo unapata faida
·         Unaweza kupata hasara kutokana na kubadilika kwa hali ya mambo juu ya bidhaa husika. Mfano: mitindo/fasheni, msimu, bei n.k.
3.      Mapato Yasiyo na Kikomo (residual or passive income).
Ni mapato mtu anayoyapata pasipokuwa na ulazima wa kushughulika/kufanya kazi kwa wakati huo au kwa maana nyingine ni mapato “Tuli”. Mapato haya mara nyingi yanatokana na kazi au shughuli uliyokwisha kufanya kitambo na kuendelea kupata mapato haya “Kimya Kimya”. Unayapata kutokana na vitega uchumi ulivyoweka. Mfano: kama umenunua nyumba na kupangisha na kila mwisho wa mwezi unapewa kodi ya pango, basi mapato hayo ndiyo yanaitwa yasiyo na kikomo au TULI.
Unashughulika mara moja tu na kisha unaendelea kupata pesa kwa muda mrefu bila hata wewe mwenyewe kushughulika tena/ zaidi. Pia mapato yatokanayo na Mtandao,  nakala za albamu ya muziki, filamu au vitabu n.k. ni hayana kikomo. Unaendelea kutoa nakala na kuuza miaka na miaka.
Ø  Uzuri MapatoYasiyo na Kikomo (Tuli).
·         Unaendelea kupata pesa kwa muda mrefu baada ya kazi/shughuli ya awali
·          Unakuwa na MUDA  wa ziada kufanya mambo mengine. Unabaki  kucheza gofu na kutalii huku pesa zinaingia
·         Hayatozwi kodi kubwa kama mapato ya aina nyingine.
Ø  Ubaya wa MapatoYasiyo na Kikomo (Tuli)
·         Wakati mwingine hugharimu sana kuwekeza katika hatua ya awali.
·         Huitaji uvumilivu (patience) kwani yaweza kuchukua muda mrefu kabla ya kuanza kupata mapato haya. “Lakini Yakianza Kuingia Unatumia Hadi Unasahau”.
Hizi ndizo aina kuu tatu za mapato yatokanayo na shughuli mbalimbali katika maeneo makuu manne ya mafanikio ya kifedha - Biashara, sanaa, michezo, uvumbuzi wa kisayansi au teknolojia, utunzi wa vitabu pamoja na kujenga mtandao (Network Marketing Business). Kwahiyo, kama una ndoto ya kupata mafanikio makubwa kimaisha, unashauriwa kufanya shughuli zinazopelekea kupata mapato “Tuli”.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba mapato Tuli, ndiyo mapato pekee ambayo ni imara, endelevu na yanarithika. Sababu nyingine inayotufanya tukushauri kupata mapato haya ni kwamba, watu wengi waliofanikiwa (matajiri) duniani, wamejipanga na kujikita katika kupata mapato haya. Ili kuendelea kujielimisha zaidi juu ya undani wa mapato haya - "tuli", kupitia mtandao wako wa maarifashop, tutaendelea kukuletea mafunzo juu ya aina hii ya mapato, ili hatimaye kila mmoja wetu aweze kuchukua hatua za maksudi tayari kuelekea kwenye maisha ya ndoto zetu.

Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO

~TWENDE KAZI PAMOJA~!

No comments: