Tuesday, March 31, 2015

Anza Safari ya Mafanikio kwa Kuanza Kujitoa Kwenye Kundi la Watu Wenye Mawazo ya Wastani!



Moja ya sababu kubwa inayofanya watu wengi kushindwa kufikia ndoto za maisha wayatakayo ni kuishi kwenye jamii ambayo  imejaa watu wengi wenye mawazo ya Wastani (watu wa kawaida), na watu hawa, kila mara  wanakulazimisha uwe kama wao. Na kosa kubwa unalolifanya au ambalo unatarajia kulifanya ni kuwa kama wao. Madhara ya kuwa kama wao ni kwamba kila mara unapotaka kufanya kitu chochote kikubwa inabidi upate ruhusa au ushauri kutoka kwao, ukifikia hatua hii basi ujue anayepanga uishije ni wao na siyo wewe tena.

Kila unapofikiria kufanya kitu na mara tu ukagundua kiko tofauti na wenzako, ghafla utapata washauri huria, ambao hawakuwahi kuwazia au kufanya hicho kitu unachopanga kufanya. Watu hawa watakwambia, hicho kitu hakijawahi kutokea na wewe utawezaje? Eti mtu anakwambia husifanye jambo fulani kwasababu hakuna aliyewahi kufanya hivyo. Mtu wa namna hii msikilize mpaka mwisho akimaliza muage na uondoke na kuanzia hapo punguza mazoea naye. Kadili utakavyopunguza mahusiano/mazoe na watu hasa wenye mawazo ya Wastani na hasi, ndivyo maisha yako yatakavyoanza kuboreka.

Jiulize ni mara ngapi umetamani kufanya biashara lakini umeshindwa kwasababu watu wengi unaowajua walifanya biashara wakashindwa? Kwahiyo, na wewe unaogopa hasara! Mara nyingi woga unaoupata unatokana na kuzungukwa na watu wengi wenye mawazo ya Wastani (mawazo yanayofanana) na wengi wao hufanya vitu vinavyofanana. Endapo huko katika hali hii ni wazi kwamba, kila utakapo kuwa na ndoto ya kuwa na maisha ya tofauti na hao rafiki zako waliokuzunguka, utapata majibu ya wewe huwezi!, wakishakwambia hivyo, basi na wewe unapata hofu ya kushindwa ambayo huzaa woga na mwisho unashindwa kuthubutu. Unapaswa kufahamu kuwa unapokutana na mtu na ukamshirikisha ndoto yako akakwambia uwezi basi ujue yeye kwa nafsi yake ndiye hawezi, hivyo jibu lake usilichukulie kama ndiyo jibu lako na usitumie majibu yake kufanya maamuzi ya wewe kutokuanza kufanya mambo yanayokupeleka kwenye ndoto ya maisha uyatakayo.

Watu wengi wanakwama kutimiza ndoto zao kwasababu, walio wengi wanapenda kutazamia majibu kutoka kwa wengine, huku wakisahau kuwa kila mmoja katika safari ya maisha anakuwa na mtihani wenye maswali tofauti na ya mwingine. Kwahiyo, unapojaribu kutumia majibu ya maswali ya mwingine kujibia maswali yako, basi ujue kuwa utashindwa tu! Cha muhimu hapa ni kwamba tujitambue kuanzia leo kuwa kila mmoja ana maswali yake binafsi na mwenye uwezo na ujuzi kuyapa majibu ya kweli ni wewe mwenyewe.

Kumbuka kuwa, ili mafanikio yoyote yapatikane, yanaanza na fikra ambapo unahitaji kuanza kujifikilia na kujiona wewe mwenyewe kama mafanikio. Kinachotakiwa ni wewe kufikiri na kutenda kimyakimya bila kujali wengine wanakuonaje na mafanikio yakipatikana yatapiga kelele ambazo kila mmoja atazisikia. Ukishafanikiwa, watu wataanza kushangaa na wengi watadhani umefanikiwa siku hiyo, kumbe safari ulianza siku nyingi lakini kwasababu ulikuwa unatekeleza ndoto yako Ndiyo maana walikuwa hawakuoni.

Kazi yako kubwa leo, ni wewe kuacha kuwa mfungwa wa kundi hili la watu wenye mawazo ya wastani, na utambue kuwa kulifanikisha hili, unahitaji kufanya maamuzi magumu na kuwa jasiri. Fanya vitu ambavyo ni muhimu kwako siyo kwasababu kila mmoja anavifanya, na huu ndiyo utakuwa mwanzo wa safari yako kuelekea kwenye mafanikio makubwa. Ili uweze kufanya mambo ambayo ni muhimu kwako ni vizuri ukaongozwa na imani ya vitu viwili ambavyo ni: maisha yatakuwa mazuri wakati ujao kuliko sasa na mimi nina uwezo na nguvu wa kuweza kufikia maisha mazuri!

Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO

No comments: