Monday, November 30, 2015

Kisa cha Wewe Kuitwa Bahili ni Hiki

“Watu wengine wameitwa wabahili kwasababu wameamua kudhibiti pesa zao zisichukuliwe kiholela na watu wengine”.

Imekuwa ni kawaida kusikia watu wakilalamikia wenzao kuwa ni wabahili. Wengine wanasema eti hawa wanaoitwa wabahili ni wagumu sana kupata pesa yao!; pia inasemekana kwamba watu hawa hawapendi pesa yao itoke kwenda kwa watu wengine ~hawataki kutoa riziki.
Pengine ni vizuri tujiulize ni kwa namna gani mtu anaitwa bahili?

Saturday, November 21, 2015

Sababu ya Wewe Kutopata Mtaji Imebainika

“Ukipata pesa na ukaitumia kabla ya kutenga akiba, basi ujue umelipa watu wengine kwanza na wewe umesahau kujilipa” 
Tajiri mkubwa na mashuhuri duniani, Bwana Warren Buffet aliwahi kusisitiza kuwa, kama unataka kujenga mtaji kutoka kwenye akiba yako binafsi ni sharti ujitahidi kuacha tabia ya “kuweka akiba baada ya kutumia na badala yake utumie kile kinachobaki baada ya kutenga pesa ya akiba”. 

Katika maisha ya umilikaji pesa duniani, kuna makundi ya aina mbili......

Saturday, November 14, 2015

Kupata Mapato Makubwa Kunahitaji Jambo Moja Muhimu

“Hakuna aliyewahi kulipwa pesa nzuri kwa kugundua matatizo, isipokuwa wale wanaotatua matatizo ya watu wengine wengi”
Pesa huwa inatiririka zaidi kuelekea kwa mtu yeyote aliye na suruhisho la matatizo au changamoto mbalimbali zilizoko kwenye jamii.

Kwa kawaida ni kwamba, thamani ya suruhisho lako ni......

Tuesday, November 10, 2015

Ni Marufuku Kuwa Mjasiriamali

"Fahamu Sababu 5 Kwanini Wewe Hutakiwi Kuwa Mjasiriamali"

Mpendwa msomaji wa mtandao huu wa MAARIFASHOP, utakumbuka kuwa ni mara nyingi nimekuwa nikiandika sana juu ya ujasiriamali, na sababu za kufanya hivyo kwa sehemu kubwa ni kwamba ujasiriamali ndiyo njia ya uhakika ya mtu yeyote kuweza kuwa kiongozi wa maisha yake. Lakini...

Saturday, November 7, 2015

Saturday, October 31, 2015

Fahamu Mambo Sita Kuelekea Kwenye Mabadiliko Chanya



1. Acha kuamini yale uliyodhania ni kweli: Bahati mbaya, kuna mambo mengi ambayo huwa tunayakukubali na kuamini kadiri tunavyozidi kukua ambayo yanaweza....

Tuesday, October 27, 2015

Fanya Mambo 5 Leo Kufaidi Nguvu ya Fikra Zako

Fanya Mambo 5 Leo Kufaidi Nguvu ya Fikra Zako


Fikra zetu kutoka ndani ya akiri zetu ndiyo kila kitu. Fikra ndilo dirisha unalotumia kuangalia dunia na mambo yake yote. Ukishakuwa umelitabua hili utakubaliana na mimi kuwa unahitaji kuanza mara moja kujitathimini juu ya mwenendo wako. Unahitaji, kujenga na kuinua heshima yako juu na hii ikiwa ni pamoja na kupanua dirisha lako la fikra ili kuona zaidi fursa za mafanikio. 

Ili kupanua dirisha la fikra, inabidi kutunza  kujiamini na kujikinga dhidi ya athari zitokanazo na changamoto mabalimabali za kimaisha. 

Na hapa unahitaji kufahamu mambo 5 yatakayo kuwezesha kufanya uchunguzi wa undani ya fikra zako na hatimaye kupata msingi imara wa kuweza kuzijenga upya, ili ziwe katika mwelekeo ambao ni chanya. 

Ninatumaini kuwa, ukishakuwa umefahamu nini cha kufanya, basi utaweza kufahamu ni kitu gani unatakiwa kufanya na ni kwanini ni muhimu kwako.
Katika kuchunguza undani wa akiri yako na hatimaye kupanua dirisha lako la fikra zako, unahitaji kufikiria mambo 5 ya msingi:

1.      Jua Kuwa Maisha Yako, Yanatengenezwa na Fikra Unazozipa Kipaumbele Kila Siku.
Ukisoma kitabu cha Bwana James Allen kiitwacho “As a Man Thinketh” anatoa mafundisho ya kwamba, wewe binadamu ndiye unayetengeneza au kuharibu maisha yako mwenyewe kutokana na fikra juu ya fikra ulizonazo akirini mwako. Na pale unaporuhusu mawazo yatokee unakuwa ni muhanga wa maelfu ya mawazo hasi na imani finyu zinakuzunguka kupitia duara lenye taarifa hizo kila muda unaopita.

Unapokuwa mfikiriaji mahili wa mawazo (mtu mwenye kufikiri na kuchagua kile unachofikiria), basi jua kuwa hapo una uwezo wa kujenga maisha ambayo ni chanya na kutembea kila siku kuelekea kwenye ndoto yako ya maisha mazuri.

2.      Jua Kuwa Kubadili Kitu Chochote Nje ya Wewe, Lazima Ubadili Fikra Zako Kwanza.
Kama unataka watu wengine wabadili mtazamo wao wa jinsi wanavyochukulia au kukuona, lazima uanze kujibadili wewe kwanza. Kama unataka kubadili uchumi, jibadili wewe. Kama unataka kubadili hali ya maisha, jibadili wewe mwenyewe. Kama unataka kubadili dunia, jibadili wewe mwenyewe. Hiyo ndiyo kazi ya ndani yako ambayo utengeneza upenyo halisi na kuelekea kwenye mafanikio.

3.      Jua Kuwa Fikra Chanya Hazijengwi kwa Siku Moja.
Mwelekeo wa fikra ulizonazo ziwe chanya au hasi, zinajengwa ndani ya mzunguko wa siku 30. Baada ya siku 30 za kufanya kitu fulani, jua kwamba imekuwa tabia yako. Na maoni yako juu ya mwenendo wa maisha uliyonayo, pia ni matokeo ya tabia ya fikra zako za kila siku. 

Kwahiyo, usifanye kitu hiki siku ya Jumatatu peke yake na kutarajia kuwa millionia siku ya jumanne. Tambua kwamba ukiweka siku 30 za kufikiri mambo chanya fikra zako zitabadilika kwa kiasi kikubwa sana. Na baadae unapanda viwango kwenda hatua nyingine ya juu zaidi na kuendelea…

4.      Jua Kuwa Unatengeneza Maisha Mazuri kwa Kujenga Taswira Nzuri Mwenyewe.
Taswira yako inatengenezwa na picha ya iliyoko kwenye ubongo na ambayo inachezesha fikra zako kwa siku nzima. Ni jinsi gani unavyojiona wewe mwenyewe kufanikiwa au kutofanikiwa. Ndiyo sababu, jambo namba moja hapo juu ni muhimu sana.

5.      Jua Kuwa Kile Unachokiamini Ndicho Kinawezekana
Kama kweli unaamini unaweza kufanya chochote na ukafanyia kazi imani hiyo, basi kwa hakika utaweza kufanikisha ndoto yako. Ni lazima uamini kuwa unaweza kufanya kitu chochote. Unaweza kuimba kwamba “unaaamini unaweza kupaa,” lakini hauamini kwamba unaweza kufanya hivyo na kwahiyo, sheria ya uvutano bado inafanya kazi. 

Na inaweza kuwa kukuhamasisha ukajikuta unapendekeza kuwa unaweza kusogeza mlima kwa kutumia mbegu ya ndogo sana ya zao la ulezi, lakini wote tunajua kuwa hicho ni kitu ambacho hakiwezi kutokea. Lakini unapokuwa umeweka malengo, unaweza kwa dhati ukayatimiza kwa kwenda kuyafanyia kazi, na ikawezekana kuwa hivyo. Hakikisha kuwa unafanya kazi na kutimiza majukumu yako ya kila siku yanayohusu maendeleo yako binafsi.

Jitahidi kuweka fikra chanya na kujua kwamba sehemu yako ya ubongo inayoitwa subconscious itakuongoza wewe kuchukua hatua moja baada ya nyingine hadi kufanikisha hicho ulichokipanga kukifanya kuwa dhahiri. Endapo utakuwa umenielewa nazungumzia nini juu kuchukua hatua dhidi ya ya mambo 5 hapo juu, basi hapana shaka unaweza kuishi ndoto zako. Na hiki ndicho ninachokutakia ukifanye.

Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO

Monday, October 19, 2015

Chimbuko la Umaskini kwa Waajiriwa ni Hili Hapa



  • Waajiriwa wengi wanauza nguvukazi ikiwa bado “ghafi”
  • Ukiuza nguvukazi ghafi umeuza “mtaji” na kuuza mtaji ni “kufirisika” jumla
Umaskini ndani ya kundi la wasomi unazidi kuingia kwa kasi ya ajabu kadili siku zinavyozidi kwenda. Kundi la watu ambao wako kwenye hatari kubwa zaidi ni hasa wale tulioko kwenye “ajira”. Ukweli ni kwamba watu wengi walioko kwenye ajira, kitu pekee wanachouza ili kupata kipato ni nguvukazitena ambayo bado ni “ghafi”.  

Uzoefu unaotokana na tafiti zilizofanywa, unathibitisha kuwa zipo sababu nyingi zinazosababisha waajiriwa na hasa wasomi wengi kuwa maskini. Lakini kubwa zaidi ni utamaduni wa wasomi kuendelea kuuza nguvukazi ikiwa bado ni “ghafi” (nguvukazi ambayo haijachakatwa). Katika ulimwengu wa “uwekezaji” nguvukazi ghafi ni mtaji muhimu sana, ambao ukichanganywa na mitaji mingine kama vile mashine, una uwezo wa kuzalisha bidhaa na huduma zenye thamani kubwa kwa watu wengine.

Ukiuza nguvukazi ghafi unakuwa umeuza “mtaji” wako: Waajiriwa wengi tumeendelea kukumbwa na adha kubwa ya umasikini kutokana na kushindwa kutambua ukweli kwamba mara nyingi kwenye maisha yetu ya ajira tumekuwa tukifanya zaidi biashara ya kuuza mtaji tulionao (nguvukazi) kwa matajiri wenye hitaji la mitaji.
Ikumbukwe kuwa, ili uweze kuzalisha bidhaa na huduma unahitaji mitaji ya aina mbalimbali ikiwemo nguvukazi ghafi. Ndiyo maana matajiri wengi wanapendelea zaidi kununua mitaji kwaajili ya kuzalisha bidhaa na huduma, ambazo huwapatia faida kubwa sana. 

Katika biashara yoyote duniani, kuuza mtaji ni kufirisika jumla. Kwahiyo, umasikini tulionao umetokana na kuuza mtaji wetu kila siku tunapotumikia ajira zetu. Kwa maana nyingine waajiriwa wengi tunafirisika kila siku ya Mungu tunapokwenda kazini.

Watu wanaouza zaidi nguvukazi ghafi wanabaki kuwa maskini kutokana na ukweli kwamba thamani ya nguvukazi ghafi huwa ni ndogo sana, kwasababu inapatikana kwa wingi na haina usumbufu kuipata. Kwa mfano: ukijifanya kutoza bei kubwa nguvukazi yako; waajiri wengi watakukimbia na chapuchapu watapata watu wengine wenye kuuza nguvukazi ile ile kwa bei nafuu sana.

Hivi ndivyo unavyouza nguvukazi ghafi: Unauza nguvukazi ghafi pale unapotumia nguvu yako kufanyakazi ya kuzalisha bidhaa na huduma ambazo siyo mali yako bali ni mali ya mtu aliyekuajiri (mwajiri). Unahitaji kufahamu kuwa, mwajiri amekuajiri ili umpatie (umuuzie) nguvukazi ambayo ni mtaji wa kuzalisha bidhaa na huduma ambazo ni mali yake binafsi. 

Kwakuwa bidhaa zinazozalishwa ni za thamani kwa watu wengine, basi ni wazi kwamba watu hao watampatia pesa mwajiri wako ili kupata bidhaa; LAKINI hawatakupatia pesa wewe, kwasababu wewe unayo nguvukazi peke yake, ambayo siyo hitaji muhimu kwa wateja wenye pesa zao. 

Ukiuza nguvukazi ghafi unauza “muda” wako: Kwakuwa umeajiriwa kwa madhumuni ya kutoa nguvukazi kwa mwajiri wako, basi thamani yako inapimwa kwa kuangalia muda unaoutumia kufanya kazi. Ili uweze kulipwa ni lazima kila siku ufike kazini na kusajiri muda wako. Usipoonekana kazini hakuna malipo yoyote, kwasababu muda wako utakuwa hujauwekeza kwa mwajiri. 

Kwahiyo, unapouza nguvukazi ghafi basi ujue umeuza “muda” na binadamu wa kawaida hawezi kufanya kazi zaidi ya masaa nane kwa siku. Masaa yote haya unafanya kazi bila kupumzika na kuzalisha vitu vyenye thamani kubwa kuliko mshahara unaolipwa na mwajiri wako. 

Haijalishi, thamani ya vitu vilivyozalishwa ni kubwa kiasi gani, mshahara wako unaolipwa unaendelea kubaki pale pale kila mwezi. Hali hii ndiyo inakufanya wewe mwajiriwa kukosa muda wa kufanya vitu vyenye kukuletea faida kubwa na mafanikio maishani, na hivyo kuzidi kuwa maskini kadiri umri wako unavyoongezeka.

Ukiuza nguvukazi ghafi huna cha kurithisha familia yako: Kama unauza nguvukazi ghafi siyo rahisi kuirithisha kwa watu wako wa karibu, kwasababu nguvukazi kama ilivyo haihamishiki kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine. Kama kitu hakihamishiki ni vigumu pia kukibadilisha kwa urahisi kuwa pesa.

Hali hii inazidi kutukumba wasomi na waajiriwa tuliowengi kutokana na ukweli kwamba unakuta umeajiriwa kwenye kampuni kubwa na una cheo kikubwa lakini ukifukuzwa au kufariki, haitokei mke au mtoto wako akapewa nafasi kama uliyokuwa nayo na wala familia haiwezi kutumia vyeti vyako vya elimu kuomba kazi. Lakini kama ungekuwa kwa mfano umeandika vitabu, hata ukifa hakimiliki ya kuendelea kuvichapisha na kuviuza inahamishiwa kwa warithi wako na wanaendelea kufaidi sawa na wewe ulivyokuwa ukifaidi.

Ukiuza nguvukazi ghafi unapata hasara: Hasara kubwa unayoipata kutokana na kuuza nguvukazi ni pale unapoishia kuuza kitu kimoja tu! Nacho ni nguvukazi. Hali hii inakubana kiasi kwamba unajikuta unalazimika kumtegemea mteja mmoja ambaye ni “mwajiri” na inakuwa siyo rahisi kubadilisha mteja kadiri unavyotaka.
Endapo ukiamua kuchakata nguvukazi yako na hatimaye kuzalisha bidhaa na huduma za thamani ni rahisi kupata wateja wengi, ambao ndio huleta mapato makubwa.

Hasara nyingine unayopata pindi unapouza nguvukazi ghafi ni kuendelea kubaki kwenye kundi la watu maskini ambao wanapata kipato hai (active income), yaani unapata pesa unapofanya kazi tu, ukiacha pesa hakuna. Endapo, ikitokea unaumwa au umesafiri basi ujue hakuna pesa itakayoingia.

Ndiyo maana unakuta mtu ni tajiri leo kwasababu anafanya kazi ya kibarua, lakini baada ya muda mfupi unakuta ni maskini na kwa waajiriwa ni hivyo hivyo wanakuwa na pesa wakiwa bado kazini LAKINI wanapostaafu ajira wanarudia kwenye hali ya umaskini jambo ambalo huwafanya watu wengi kufa miaka michache baada ya kustaafu.

Washindi dhidi ya umaskini ni wale walioamua kuchakata nguvukazi yao: Ukweli ni kwamba kila mchakato wowote lazima utoe matokeo. Matokeo ya kuchakata nguvukazi ghafi ni “bidhaa au huduma” zenye thamani kubwa kwa watu wengine. Kitendo cha kuchakata nguvukazi kinatokana na matumizi ya nguvu ya akiri pamoja na nguvu ya mwili kwenye rasilimali kama ardhi, maliasili, ujuzi, pesa n.k, kwa lengo la kupata mali au bidhaa kwaajili ya watu wengine. 

Ukishapata bidhaa zenye thamani (manufaa) kwa watu wengine, basi mara moja watakuletea pesa ili kujipatia bidhaa na huduma muhimu kutoka kwako. Kadiri utakavyotengeneza bidhaa nyingi na zenye thamani kubwa ndivyo utakavyopata pesa nyingi ambayo haina kikomo. 


Ni wakati sasa tuamke na tujibidishe sana kwa kuandaa mazingira yatakayotuwezesha hasa sisi wataka mafanikio kuuza “matokeo” ya nguvukazi badala ya utamaduni wa sasa wa kuuza nguvukazi ghafi. Ukweli ni kwamba, unapokuwa mtu wa kuuza matokeo ya nguvukazi ambayo ni bidhaa na huduma mbalimbali, tayari unakuwa umemaliza kazi, kinachofuatia ni kuendelea kuuza bidhaa hizo na wakati huo huo unakwenda kuwekeza muda wako huo kwenye kuzalisha vitu vingine, huku akiendelea kufaidi matunda ya kazi aliyoifanya mwanzo.

Kwa watu wote na hasa waajiriwa tunaotaka mafanikio makubwa, ni lazima kila mmoja wetu ajiwekee tarehe ya mwisho ya kuacha kuuza nguvukazi ghafi. Kila mmoja akifikia tarehe yake ya mwisho kuuza nguvukazi ghafi, mara moja aanze kujikita katika kubadili nguvu ya akiri na hisia kuwa bidhaa na huduma zenye kuwa suruhisho la kudumu kwa matatizo na changamoto mbalimbali zinazowakabili watu wengine.

Kwakuwa utazalisha bidhaa na huduma zenye kuwa na manufaa makubwa kwa watu wengine, basi na wao watakupatia zawadi ambayo ni pesa, ili kujipatia kila kilicho bora kutoka kwako. Tukiweza kufanikisha azima hii, basi tutatajirika kutokana na ukweli kwamba watu wengi kwasasa wanataka bidhaa na huduma ambazo ni suruhisho ya changamoto zao. 
 
Wateja ni wengi ambao wako tayari kununua kila kitu kitakachozalishwa ilimradi kina thamani kwao ~ kwahiyo soko ni kubwa. Nchi yetu inapokaribia kuingia uchumi wa kati, mahitaji ya bidhaa na huduma zitokanazo na nguvu ya akiri/fikra zitazidi kuongezeka. 

Bidhaa zenyewe ni kama vile muziki, sanaa, vitabu, program za mafunzo ya ujasiriamali/biashara/afya/kilimo/majengo pamoja na machapisho juu miongozo mbalimbali ya uwekezaji katika mambo ya utalii, uwindaji, gasi, mafuta, madini, kilimo n.k.

Uchumi wa watanzania ukizidi kuongezeka na idadi ya wasomi ambao ndio wahitaji wakubwa itazidi kuongezeka huko tuendako ~ Kwahiyo ewe mtanzania mwenzangu, anza kuchukua hatua leo, wakati ni sasa.

Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO

Saturday, August 29, 2015

Uhuru wa Kipato Unaletwa na Mchakato Siyo Shughuli



  •  Ukifanya kazi ki-shughuli ni sawa na mtu anaye sukuma mkokoteni kwa kulizunguka duara
  • Uhuru wa kipato (pesa) unawezekana tu kama utafanya kazi zako “Ki-mchakato

Watu wenye busara waliwahi kusema kuwa “maisha ni safari ndefu”, na kawaida ya safari ya maisha, ni pamoja na kukutana na vitu vingi njiani. Bila kuwa tumejipanga, vitu vingi tunavyokutana navyo safarini, vina uwezo mkubwa sana wa kutukwamisha na hatimaye kushindwa kufikia mwisho wa safari yetu.

Ili tuweze kumudu safari yetu maisha na hatimaye kufikia yale maisha ya ndoto zetu; kitu kimoja muhimu ni namna gani tunavyojipanga pamoja na mitazamo yetu juu ya kile tunachofanya kila siku.

Ukiangalia utaratibu mzima ambao watu wanautumia katika kufanya kazi zao, utaona makundi ya aina mbili. Aina ya kwanza ni kundi linalofanya kazi “ki-shughuli” na kundi la pili ni wale wanaofanya kazi “ki-mchakato. Kwa maana nyingine makundi haya mawili yanafanya kazi kwa kufuata mitazamo tofauti, ndiyo maana leo hii tuna watu wachache waliofanikiwa huku wengine wengi wakibakia pale pale miaka yote ya maisha yao.

Shughuli Hasa ni Kitu Gani? Shughuli ni kitendo kinachotakiwa kufanyika au kinachofanyika ili kukamilisha sehemu fulani ya kazi. Pia, shughuli inasimama kama kitu kimoja na ni cha kipekee, ikimalizika imemalizika, huna haja ya kuirudia. Ukiweza kufanya na kukamilisha shughuli moja peke yake haitoshelezi kutoa bidhaa husika. Lazima zifanyike shughuli zaidi ya moja ndipo bidhaa iliyokusudiwa iweze kupatikana.

Mfano: kama wewe shida yako ni kula chakula, lazima ujue kuwa, ili chakula chako kiwe tayari, lazima shughuli zaidi ya moja zifanyike, kutegemea mtu na mtu. Kuna mwingine ataanza kwa kununua mkaa, mwingine ataanza kwa kuwasha moto, na mwingine ataanza kwa kununua mchele n.k.; mpaka shughuli ya kupakua na hatimaye shughuli ya mwisho ya kula chakula.

Kwahiyo, endapo utakamilisha kufanya shughuli mojawapo na ukaishia hapo ni wazi kwamba hutaweza kula, kwasababu chakula kitakuwa hakijawa tayari. Kwa maana nyingine tunaweza kusema kwamba, hakuna bidhaa inayoweza kupatikana kwa kukamilisha shughuli moja peke yake, lazima shughuli zote muhimu zikamilike, ndipo matokeo au bidhaa tarajiwa ipatikane.

Kwa malengo ya kupata matokeo tarajiwa, inakubidi hujitahidi kukamilisha shughuli zako zilizopangwa, ili kupata matokeo tarajiwa. Endapo utaishia kukamilisha shughuli moja kati ya zote zinazotakiwa kufanyika, basi ujue kuwa hutaweza kupata au kuzalisha kitu chochote chenye thamani inayokusudiwa na wateja.

Mchakato Hasa ni Kitu Gani? Mchakato ni  mpangilio maalumu wa matukio au shughuli zaidi ya moja kwaajili ya kutoa/kuleta matokeo yanayokusudiwa. Ili mchakato uwepo, ni lazima shughuli husika ziwe na uhusiano wa karibu. Shughuli moja ikikamilika inakuwa ndio kianzio cha shughuli inayofuata na hatimaye kunakuwa na mwendelezo maalum hadi kufikia matokeo tarajiwa.

Kwahiyo, uzalishaji wa bidhaa yoyote unafuata utaratibu wa ki-mchakato. Ili uweze, kukamilisha kazi fulani au uweze kuzalisha bidhaa fulani, kunakuwapo na matukio au shughuli zaidi ya moja ambazo ziko kwenye aina fulani ya mnyororo. Na mnyororo huo ndio unakuwa na vipingiri pingiri ambavyo kila kipingiri, unaweza kusema ni shughuli au tukio moja. Kwa maana nyingine ni mchakato tu ndio una uwezo wa kukamilisha bidhaa.

Kazi ya kusaka mafanikio makubwa na hasa uhuru wa kipato (pesa) inawezekana tu kama utafanya au kuratibu kazi zako “Ki-mchakato  badala ya kuendelea na mfumo wa watu waliowengi, ambao utafuta eti! maisha bora “Ki-shughuli”. Na shughuli nyingi za utafutaji tunazofanya hazina uhusiano, mpangilio wala mwendelezo wenye tija.

Pia, shughuli hizi, hazina uratibu wowote wala uhusiano na ndoto zetu au malengo yetu ya muda mrefu. Matokeo yake tumejikuta tunapata matokeo hafifu, hali ambayo imeendelea kutukatisha tamaa na kudhania kuwa kupata uhuru wa kipato au pesa ni jambo ambalo haliwezekani na kama likiwezekana basi ni bahati.


Weka mpango wa kufikia malengo yako: Unapoanza safari yako ya kutafuta uhuru wa kipato (pesa) ni lazima ujipange, ikiwa ni pamoja na kufikiri kwa kina juu ya maisha yale unayotamani kuyaishi. Ukishajua ndoto yako ni ipi au mafanikio unayotarajia ni yapi, basi inakuwa rahisi kufahamu mchakato utakaopitia hadi kufikia kile unachotaka.

Ubainishaji wa mchakato kwaajili ya safari yako ya kwenda kwenye ndoto zako, unaambatana na zoezi la kuainisha shughuli zote muhimu zitakazotakiwa kufanyika hadi kufikia maisha ya ndoto yako. Pia, inakupa fursa ya kuweza kufahamu ni muda gani utautumia kufika hapo unapotaka kwenda.

Ukifanya kazi ki-mchakato ni rahisi sana kutathimini maendeleo ya kazi yako na unaweza kupima na kuona uko mbali au karibu kiasi gani na ndoto zako. Kwahiyo, inatosha kusema kwamba “mafanikio yoyote ni mchakato”. Na mchakato ndio unazaa mpango kazi, ambao ukifuatwa una uwezo wa kukutoa pale ulipo hadi pale unapotaka kwenda.

Ukifanya kazi ki-shughuli ni sawa na mtu anayesukuma mkokoteni kwa kulizunguka duara. Kwa mtu yeyote anayezunguka duara, siyo rahisi kufika anapotaka kwenda, kwani muda wote atakuwa anazunguka na kurudi aliko toka. Kwahiyo, maisha ya kufanya kazi ki-shughuli ni sawa na mtu anayezunguka mduara.  

Ndiyo maana unaweza ukakuta mtu kwa mfano anafanya biashara ya kununua na kuuza vitu na unakuta miaka nenda rudi yuko pale pale wakati kila siku anakwenda ananunua vitu na vinanunuliwa basi.

Sababu inayomfanya awe hivyo ni kwamba mtu huyo anafanya biashara yake kama shughuli na anajikuta kila mara anarudia shughuli ile ile miaka yote bila kupiga hatua yoyote. Yote haya yanatokea kwasababu “mtazamo wa biashara yako ni wa ki-shughuli badala ya mtazamo wa ki-mchakato”.

Unapoanza kufanya kazi au biashara yako kwa mtazamo wa ki-mchakato inakusaidia sana kupambana na changamoto. Lakini pia uvumilivu pale matatizo yanapojitokeza, ni rahisi kuvumilia kwakuwa unakuwa unafahamu ni wapi unaenda na utafanya kila liwezekanalo, ili kuweza kufikia malengo au ndoto zako. Ukiwa na mchakato wako ambao umeandikwa, unakusaidia kutokuangalia wengine wanachofanya badala yake, wewe unakomaa na jambo moja tu la kukamilisha mchakato wako.

Kufanya kazi Ki-mchakato kunahitaji umakini mkubwa sana, na umakini huu hauji hivi hivi, bali ni kwa kujenga tabia ya kujisomea vitabu na kujifunza kutokana na watu waliofanikiwa. 

Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO

KARIBU TWENDE KAZI PAMOJA